HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA WENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI KWENYE HAFLA YA UFUNGUZI WA MAJADILIANO YA WAJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA CCM TAIFA, MWANZA TAREHE 12 DESEMBA, 2019 Thursday 12th December 2019 Chanzo :Ikulu

Rais John Pombe Magufuli akihutubia

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM- Zanzibar;

Mheshimiwa  Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM – Tanzania Bara;

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa  Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar;

Mheshimiwa Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu wa CCM;

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi;

Ndugu Wajumbe wa Sekretarieti ya CCM;

Ndugu Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa;

Mabibi na Mabwana:

Kidumu Chama Cha Mapinduzi!

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kwa neema zake ametujalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kukutana mahali hapa. Namshukuru pia Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, kwa kunialika na kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi kwenye Hafla hii ya Ufunguzi wa Majadiliano ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nimefurahi pia kuona mara hii, Vikao vya Chama pamoja na Majadiliano haya vyote vinanyika hapa Mwanza. Hili ni jambo zuri kwa kuwa Chama chetu ni cha Watanzania wote; na hivyo, tuna haki ya kufanyia vikao vyetu mahali popote nchini.  Sisi ndio tumeshika hatamu za uongozi wa Dola.

Kabla sijaendelea, napenda kutumia fursa hii kukipongeza Chama Cha Mapinduzi, Wajumbe wa NEC, viongozi wa ngazi mbalimbali pamoja na wanachama wote kwa ushindi mkubwa na wa kishindo kwenye Uchaguzi Serikali za Mitaa. Katika maeneo mengi, baadhi ya Vyama viliamua kukimbia mapema. Na hii ni dalili njema kwa Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Ndugu Wajumbe wa NEC:

Siku mbili zilizopita, tumesheherekea Maadhimisho ya Miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Katika miaka hii yote, Chama Cha Mapinduzi ndicho ki, ukiacha miaka michache ya Uongozi wa Vyama – Mama vya TANU na ASP. Hivyo, kimsingi, tangu tumepata uhuru, CCM imeshika hatamu za uongozi kwa kipindi chote hiki; jambo ambalo ni nadra katika nchi nyingi za Afrika. Kwa hakika, hili ni jambo la kujivunia na kujipongeza sisi wote. Lakini pia imetimia miaka minne (04), tangu Chama chetu kishike hatamu za uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano; na sasa, umesalia mwaka mmoja kukamilisha kipindi cha miaka mitano ya Awamu ya Tano. Lakini, nina uhakika, kila Mjumbe aliyepo hapa angependa Chama chetu kiendelee kushika hatamu za uongozi miaka mingine ijayo. Na hilo litawezekana tu, endapo tutaweza kukidhi mahitaji na matarajio ya Watanzania.

Ni dhahiri kwamba, kama Chama, ili tuweze kufahamu endapo tunakidhi matarajio ya wananchi, hatuna budi kujenga utamaduni na uwezo wa kujitathimini, kujisahihisha na kubadilika. CCM must develop and enhance the capacity to re-invend itself. Tuepuke uongozi wa mazoea. Na kusema kweli, Vyama vingi vinavyojisahau na kuongoza Serikali kwa mazoea, hufikia hatua ya kupoteza imani ya wananchi na uhalali wa kisiasa. Ndicho kilichotokea kwa baadhi ya Vyama vingi vilivyopigania Uhuru Barani Afrika. Ndugu zangu tusifikie huko.

Kwa sababu hiyo basi, ninampongeza sana Katibu Mkuu na Sekretarieti yake kwa uamuzi wa kuandaa Semina hii ya Wajumbe wa NEC. NEC ni Chombo kikubwa cha maamuzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi; hivyo Semina hii itumike kama fursa ya kutathimini utendaji wa Chama na Serikali, kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mahali tulikotoka, mahali tulipo pamoja na mwelekeo wetu kama Chama. Lakini muhimu zaidi ni masuala mapana yanayotakiwa kuzingatiwa kwenye Mwelekeo wa Sera za Chama Cha Mapinduzi kwa Miaka kumi (10) ijayo, yaani 2020 – 2030, pamoja na mipango mahsusi tunayotaka kuitekeleza kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025. Majadiliano haya ya leo yatoe mwelekeo huo.

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Washiriki;

Katika Hafla hii fupi ya Ufunguzi, sikusudii kuzungumzia kwa kina kuhusu mafanikio katika utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja shughuli zingine za Seriakali. Na kwa kweli, hiyo siyo kazi yangu; ni kazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Na hawa wote wapo hapa na watapewa fursa ya kufanya mawasilisho yao. Kwa upande wangu, nitataja baadhi tu ya hatua muhimu tulizochukua ili kukiimarisha Chama; changamoto tunazokabiliana nazo katika jitihada zetu za kuleta mageuzi nchini; na mwisho nitabainisha masuala machache ambayo, kwa maoni yangu, ningependekeza yazingatiwe kwenye Mwelekeo wa Sera za CCM katika Kipindi cha 2020 – 2030 na Ilani ya mwaka 2020 – 2025.

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Washiriki:

Kama mtakavyokumbuka, nilipopewa ridhaa ya kuongoza Chama katika nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, nilitambua haja ya kufanya mageuzi makubwa ndani ya Chama. Mageuzi hayo yalikuwa ni ya kimuundo, kiutendaji lakini pia kiuchumi. Lengo la kufanya mageuzi haya ilikuwa ni kuongeza ufanisi na kuondoa urasimu; kupunguza gharama za uendeshaji na pia kukijenga Chama kiuchumi. Kwa maoni yangu, mageuzi hayo yalikuwa hayaepukiki ili kulinda uhai wa Chama, kurejesha imani ya wananchi na heshima ya Chama  chetu. Mageuzi hayo yalijengwa kwenye dhana ya Chama imara, Serikali Imara. Na kusema kweli, ilikuwa ni vigumu kuzungumzia mageuzi makubwa ndani ya Serikali, ilihali Chama kilichokabidhiwa Dola kipo hoi bin taaban. Hii ingesababisha mtanziko mkubwa wa kiuongozi.

Mageuzi makubwa tuliyofanya kimuundo na kiutendaji ni pamoja na kupunguza idadi ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kutoka 342 hadi 168, hongereni sana wajumbe kwa maamuzi haya, na pia kuwaondoa Makatibu wa Mikoa katika orodha ya Wajumbe wa NEC. Aidha, tuliondoa kada za Katibu Msaidizi na Mhasibu wa Wilaya na Mkoa ili majukumu yao yatekelezwe na Katibu mmoja wa Wilaya au Mkoa. Vilevile, tuliamua kuunganisha Utumishi wa Chama na Jumuiya ili uwe chini ya usimamizi wa Sekretarieti ya NEC. Halikadhalika, tulifuta nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha kwa ngazi za Mkoa hadi Tawi. Nawapongeza sana wajumbe wa NEC kwa maamuzi haya.

Kiuchumi, tulibaini kwamba, pamoja na uwingi wa rasilimali, mapato ya Chama yalikuwa ni kidogo sana na Chama kilikuwa hakiwezi kujiendesha. Kwa sehemu kubwa mali na rasilimali nyingi za Chama zilikuwa zikiwanufaisha watu binafsi, hususan viongozi wachache waliokuwa wamejimilikisha mali na rasilimali hizo. Chama kikabaki kuwa ombaomba na kutegemea fedha za matajiri wachache waliojiita wafadhili wa Chama. Matajiri hao wachache ndio walikuwa na maamuzi makubwa ndani ya Chama; hakuna mtu aliyefurukuta. Nikasema sitakubali uozo huu uendelee chini ya uenyekiti wangu na chini ua uongozi wenu. Hatuwezi kujenga Serikali na Taifa linalojitegemea wakati Chama kinachoongoza Dola ni tegemezi na ombaomba.

Hatua kubwa niliyochukua kama Mwenyekiti ni kuunda Tume ya Uhakiki wa Mali za Chama, maarufu kama Tume ya Makinikia ya Chama, chini ya Uenyekiti wa Dkt. Bashiri Ally Kakurwa, ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa CCM. Tume hiyo ilifanya kazi kwa weledi mkubwa na kubaini kuwa, kwa miaka mingi, CCM ilikuwa shamba la bibi; kila mtu alikuwa akitafuna mali za Chama mahali alipo. Tukaanza kazi ya kurejesha mali za Chama, ikiwemo vyombo vya habari (kama vile Channel Ten), majengo, viwanja, vitalu vya madini, vituo vya mafuta, nk.

Vilevile, tukaanza kupitia upya mikataba mbalimbali ya biashara na uwekezaji ndani ya Chama, ikiwemo ile ya Vodacom, Jengo la Umoja wa Vijana Dar es Salaam, nk. Lakini muhimu zaidi, tukaanzisha Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi na Uendeshaji wa Mali na Rasilimali za Chama. Aidha, tumeunganisha umiliki wa mali na rasilimali za Chama na Jumuiya zake chini ya usimamizi wa Baraza moja la Wadhamini wa Mali za Chama na Jumuiya zake. Hatua nyingine muhimu tuliyochukua ni kuhakikisha mapato na matumizi ya fedha mikoani yanadhibitiwa na Mkao Makuu.

Jitihada hizi zote kwa pamoja, zimeongeza mapato ya Chama kutoka shilingi bilioni 46.1 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 59.8 mwaka 2018/19, sawa na ongezeko la asilimia 30. Muhimu zaidi, baada ya kuanza kuthaminisha upya (re-valuation) mali za Chama, thamani yake imeongezeka kutoka shilingi bilioni 41.033 mwaka 2016/17 hadi bilioni 974.66 hivi sasa, sawa na ongezeko la asilimia 2275.3. Nimearifiwa kuwa zoezi hili la re-valuation limefanyika katika mikoa 13 tu likijumuisha baaadhi ya mali za Jumuiya.  Zoezi hilo litaendelea kwenye mikoa iliyosalia. Nina uhakika thamani ya mali za chama itakuwa ni ya Mabilioni na Mabilioni ya fedha.

Tafsiri yake ni kwamba mapato ya Chama yataendelea kuongezeka kwa kasi zaidi. Na katika hili, nampongeza sana Dkt. Haule na Idara nzima ya Uchumi na Fedha kwa jitihada zao kubwa walizofanya. Ni matumaini yangu, mkiendelea na jitihada hizi, Chama chetu kitaweza kujitegemea kwa asilimia mia moja badala ya kuwategemea watu wanaojiita wafadhili, lakini pia mtaweza kuongeza maslahi ya watumishi wa Chama, ambayo kwa sasa ni madogo sana. Jambo lingine la kujivunia na kufurahisha zaidi ni kwamba, katika miaka minne iliyopita, Chama chetu kimeendelea kupokea wanachama mbalimbali kutoka Vyama vya Upinzani, wakiwemo Wabunge na Madiwani. Hii imepelekea ruzuku ya Chama kuongezeka kutoka shilingi bilioni 12.4 kwa mwaka (mwaka 2015/16) hadi bilioni 13.5 kwa mwaka, hivi sasa.

Hayo ni baadhi ya mageuzi ya kimuundo, kiutendaji na kiuchumi tuliyotekeleza ndani ya Chama. Lakini ninafahamu changamoto zilizopo katika kuyafanya mageuzi haya yashuke chini kabisa hadi kwenye ngazi ya Tawi na Shina. Na hili ndilo jukumu la Sekretarieti ya Chama. Tambueni kuwa Chama ni Mashina na Matawi; elekezeni jitihada zenu huko. Ninaamini, mkifanya hivyo, Chama chetu kitakuwa imara zaidi.

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Wajumbe:

Mwelekeo wa Sera za Chama Cha Mapinduzi, kwa kipindi cha miaka kumi 2010 – 2020, ulijikita katika kujenga uchumi wa kisasa na kuwawezesha wananchi; vivyo hivyo na Ilani ya Uchaguzi ya 2015 – 2020 iliandaliwa kwa kuzingatia Mwelekeo huo. Lakini nikiri kwamba sisi, katika Serikali, hatukuitumia Ilani ya Chama kama Msahafu au Biblia. Ni kweli, tumetumia Ilani katika kutekeleza mambo mengi lakini hatukupenda kujizuia kufanya jitihada nyingine zenye maslahi mapana kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla. Hivyo, pamoja na kutumia Ilani kama mwongozo, tuliona kuna umuhimu wa kuangalia mahitaji halisi ya maendeleo kwa sasa na kuchukua hatua muafaka. Hivyo, tulijadiliana na kukubaliana kwamba baadhi ya hatua za msingi hazina budi kuchukuliwa hata kama siyo sehemu ya Ilani, ili mradi zinalenga kuharakisha maendeleo na kuharakisha utekelezaji wa Ilani yenyewe.

Hivyo basi, mtaona kwamba mafanikio yatakayotajwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, kwa miaka minne iliyopita, baadhi yake yamebainishwa ndani ya Ilani na mengine hayatajwa kwenye Ilani. Hata hivyo, yote yamejielekeza kwenye kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi nchini. Mathalan, mtaelezwa kuhusu mafanikio tuliyopata katika kuleta mabadiliko kwenye Utumishi wa Umma, hususan kurejesha heshima, nidhamu, uadilifu, uchapakazi, uzalendo na ari ya kujitolea kwa Taifa. Vilevile, mtaelezwa mfanikio makubwa katika sekta za kijamii kama vile afya, elimu, maji na umeme. Mtaelezwa pia kuhusu jitihada tulizofanya katika kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji kama vile barabara, reli, maji na anga. Kwa ujumla, hakuna sekta iliyoachwa nyuma, iwe ni kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii, ulinzi na usalama, nk.  Haya yote yatawasilishwa kwenu Waziri Mkuu pamoja na Makamu wa Pili wa Rais na mnaweza kupata muda wa kuyatathimini zaidi. Lakini mafanikio yote hayo yanatokana na jitihada za pamoja na ushirikiano kati ya Chama na Serikali. Nami ninawashukuru sana viongozi wote wa Chama na Serikali pamoja na Watanzania wote kwa ujumla katika kufanisha haya yote.

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Wajumbe:

Katika utangulizi, nilisema ningezungumzia baadhi ya changamoto ambazo tumekuwa tukikabiliana nazo kama Serikali katika jitihada zetu za kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi. Kusema kweli, mimi huwa sipendi sana kuzungumzia changamoto; huwa napenda kuzikabili moja moja, head on. Lakini kwa minajili ya hadhara hii, nitazitaja mbili tu. Moja kubwa ni kukosekana kwa utayari, miongoni mwa baadhi wananchi na viongozi pia, wa kukubali na kuendana na mabadiliko, yaani resistance to change. Bado watu wanashindwa au wanachelewa kuelewa kuwa tupo kwenye zama mpya ambapo nia yetu kubwa ni kujenga Taifa linalojitegemea kiuchumi. Hawajaelewa kwamba ni lazima tujenge nidhamu na uadilifu katika kazi na kuelekeza rasilimali zetu kwenye mikakati ya maendeleo inayolenga kuleta ukombozi kiuchumi. Na kwamba ni lazima tupige vita rushwa, uzembe na mambo mengine ambayo yatatuchelewesha kufika huko. Ninachokiona mimi bado kuna uzembe, kushindwa kuchukua maamuzi na kupenda fedha za dezo ambazo hazipo. Haya yote yanatokana na mazoea ya utegemezi na kushindwa kutambua kuwa tunapojenga misingi ya kujitegemea, hatuna budi kufunga mikanda na, wakati mwingine, kupata shida kwa muda ili tujitegemee.

Hiyo ni changamoto ya kwanza kubwa. Lakini ya pili ambayo ni kubwa pia ni hujuma dhidi ya jitihada za Serikali zinazofanywa na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi yetu. Hujuma hizi zinalenga kufifisha jitihada zetu za kujikomboa kiuchumi kwa maslahi yao binafsi. Watu hawa kamwe hawataki kuona tunadhibiti rasilimali zetu ambazo walikuwa wakizivuna na kusafirisha wanavyotaka, bila kuulizwa na mtu. Zaidi ya hapo, watu hawa hawatakubali tutekeleze miradi mikubwa ya kimapinduzi itakayoharakisha maendeleo nchini, ikiwemo Bwawa la Nyerere, SGR au Kufufua Shirika la ATCL, wasingependa tutoe elimu bure, wasingependa tupeleke umeme katika vijiji vyote na mengine mengi. Wangependa tuendelee kuwategemea wao, ilihali wao wanaishi kwa kutegemea rasilimali zetu.

Hivyo, wanatumia kila njia kufifisha jitihada zetu na kupenyeza ajenda zao. Wakati mwingine, wanatumia Asasi za Kiraia (Civil Societies) na Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) na kujifanya wanatufundisha demokrasia na haki za binadamu, ilihali wao wenyewe wanavunja misingi hiyo kwa kujenga mifumo ya kinyonyaji, kuchochea machafuko na kuingilia uhuru wa mataifa mengine. Wakati mwingine, watajenga mazingira ya taharuki na kusema ebola imeingia Tanzania. Ili mradi tu ionekane nchi haiko salama. Inatupasa tutambue kuwa hii ndiyo changamoto kubwa katika mapito yetu kuelekea ukombozi wa kiuchumi; na tusiposimama imara na kujenga uzalendo na moyo wa kujitolea kwa Taifa, hatuwezi kushinda. Ni lazima tujitambue, tujue tulipotoka, mahali tulipo na mwelekeo wetu kwa manufaa ya Watanzania.

Na mimi niwajulishe nyinyi wajumbe wa NEC, nyinyi ndio chombo muhimu cha kuleta mabadiliko katika Taifa hili, hayupo mwingine wa kuwasemea na hatapatikana kwa sababu Serikali hii inaongozwa na Chama Cha Mapinduzi, na kiongozi wa Serikali kupitia chombo kilichopo juu cha mafanikio ama kutokufanikiwa ni nyinyi wajumbe wa NEC mliopo hapa. Na ndio maana najitahidi kuzungumza kwa uwazi sana ili kusudi muelewe, mzijue changamoto lakini pia tujitafakari ni kwa namna gani Taifa tunaweza kulipeleka mbele ama kulirudisha nyuma katika maendeleo ya kiuchumi.

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Washiriki:

Nilianza Hotuba yangu kwa kuwapongeza wana-CCM wenzangu kwa kushinda Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Nimewakumbusha pia kuhusu mageuzi tuliyofanya kwenye Chama chetu na mafanikio yaliyopatikana kutokana na mageuzi hayo. Nimewaeleza pia kuwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne iliyopita yatawasilishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Lakini nimegusia pia kuhusu changamoto tunazokabiliana nazo.

Ninapoelekea kuhitimisha, naomba sasa nipendekeze kwenu baadhi ya masuala ninayodhani ni muhimu yakazingatiwa kwenye Mwelekeo wa Sera za Chama chetu kwa miaka 10 ijayo na Ilani ya Uchaguzi 2020 – 2025. Ingawa nitayataja masuala husika kisekta, msingi wa Mwelekeo wa Sera za CCM na Ilani uwe ni kujenga Taifa linalojitegemea ambalo nguzo kuu ya uchumi wake ni sekta ya viwanda. Tunataka tufike mahali ambapo Taifa letu litakuwa na uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kutekeleza mipango yake ya maendeleo bila kutegemea misaada. Nilikwisha eleza ndugu zangu Tanzania Tajiri, sisi ni Matajiri kwelikweli, na hii narudi ndugu zangu kwa wajumbe wa NEC Tanzania ni Tajiri, ni Tajiri, walamsiwe na wasiwasi na utajiri wa Tanzania, sisi ni Matajiri kwelikweli.

Ndio maana tulipofanya mabadiliko katika sekta ya madini, mwanzoni tu makusanyo yalikuwa shilingi Bilioni 191, kwa taarifa nilizopata jana, makusanyo mwaka huu yatafika karibu shilingi Bilioni 600. Na baada kubadilisha ile sheria, sasa watu wanaotaka kushiriki na sisi katika madini wamejitokeza na wanakuja, ndio maana mmesikia hivi karibuni imetangazwa kampuni ya Twiga ambayo tutashirikiana na kampuni ya Barrick, na wiki hii wanakuja kwa ajili ya majadiliano na kumaliza kila kitu na pale faida tutakuwa tunagawa 50 kwa 50, hisa sisi tutakuwa na asilimia 16 na wao zilizobaki, siku za nyuma sisi ilikuwa sifuri, huu ndio mwelekeo tunaoutaka.

Tanzania tuna almasi nao tunafanya nao mazungumzo, hata jana walikjuwa na mazungumzo Dar es Salaam namna ya kubadilisha zile hisa. Lakini Tanzania tuna kila kitu, ukienda kule Zanzibar kuna mafuta, yale mafuta yakishakuwa Zanziba maana yake hata Bara yapo, tuna gesi ya etheny ipo, tuna helium, ukienda kule kwa Waziri Mkuu kuna graphite, anakanyaga udongo lakini ndani kuna graphite, ndugu zangu Wamwela hawajui ni kama Wasukuma ambavyo walikuwa hawajui almasi wakawa wanacheza nazo kwenye bao mpaka alipokuja Williamson, Tanzania ni Tajiri ndugu zangu. Kwa hiyo wala tusiogope kuyasemea haya na kusimama imara kulinda rasilimali zetu. Dhababu ipo kila mahali, inawezekana hata hapa ukichimba utakuta dhahabu kwenye jengo hili, dhahabu ipo kila mahali.

Ndugu zangu sisi ni matajiri, tuna chuma, yale mashapo ya chuma yaliyopo kule Liganga ni ya Mabilioni na Mabilioni na ndanbi ya kile chuma kuna titanium, kuna makaa ya mawe, yaani unapokwenda, kule kwenu Bukoba kuna madini ya kioo yapo yamejaa pale, kwenye maendeo alipozikwa Profesa Mulokozi ni madini ya kioo tu yamejaa pale, Kisarawe kule kuna madini ya kutengeneza  malumalu bora kabisa duniani, Tanzania ndugu zangu ni matajiri, sisi ni matajiri ila hatujiamini kama sisi ni matajiri.

Mbuga za Wanyama, mpaka sasa tunaongoza tuna Hifadhi za Taifa 22 zina Wanyama wote, hata mti mrefu kuliko yote Afrika upo Tanzania, Mlima mrefu kuliko yote Afrika upo Tanzania Mlima Kilimanjaro, Mungu ametupendelea, Tanzania Hoyee

Kwa hiyo ndugu zangu wanjumbe nataka niwaeleze hili kwamba nchi hii ni Tajiri. Ni lazima Ilani tutakayoitengeneza au mwelekeo wa Chama Cha Mapinduzi ujielekeze ni namna gani tutaweza kuitumia hii rasilimali tuliyopewa na Mungu katika kujiletea mabadiliko ya kiuchumi sisi kama Taifa. Maamuzi hayo wa kuyafanya ni nyinyi wajumbe. Mtakayoyaamua ndio yatailazimu Serikali itakayoingia madarakani baada yam waka 2020 kutekeleza haya maamuzi yenu, nyinyi ndio walimunyinyi ndio viongozi, Serikali ni lazima itekeleze. Ndio maana nasema katika kikao hiki mjadili kwa uwazi kabisa, msimung’unye maneno, kama ni jipu pasua, kama ni mkia ukate. CCM Hoyeee

Hii misaada tunayopata ni ya kutupumbaza, ni ya kutupumbaza, lakini hata idadi yetu ya Watanzania tuliopo, sisi tuna idadi kubwa kuliko nchi yoyote ya Afrika Mashariki, tupo Milioni 55, idadi ya watu ni mtaji, ukitengeneza viatu vyako vitavaliwa na watu Milioni 55 kuliko nchi yenye watu wachache, kwa hiyo unapokuwa nan chi yenye idadi ya watu wengi ni soko, ni uchumi. Ndio maana China ipo juu katika uchumi duniani ni kwa sababu ina watu wengi kwa hiyo soko lipo, ukiuza kahawa hata kama Wachina wangekunywa kijiko kimoja kimoja kahawa yetu yote ingeliwa ni kwa sababu wana soko.

Sisi tuna ng’ombe Milioni 32.5 na ni wa pili katika Afrika, tumeweza kwa sababu tuna soko, lakini mifugo yetu tungeipeleka China kwenda kuliwa na watu Bilioni 1.3 au India watu Bilioni 1.3 ni soko. Kwa hiyo sisi Tanzania tuna soko kwa sababu tuna idadi kubwa ya watu. Na ukishakuiwa na soko wewe ni Tajiri, ukitengeneza nguo zako ukaziuza kwenye soko lako utaweza kuliko yule mwenye idadi ndogo ya watu. Kwa hiyo tutumia fursa ya kuwa na idadi kubwa katika Afrika Mashariki na pia katika Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) tuna watu wengi. Lakini pia tuitumie Ilani ya Uchaguzi tunayoiandaa ili iakisi fursa za nchi yetu ambayo imezungukwa na nchi 8. Kuzungukwa na majirani wa namna hiyo, wengine hawana njia ya kwenda bandarini ni uchumi, kwa sababu wakitaka kusafirisha mizigo yao ni lazima wapiti humu. Kwa hiyo unapaswa kutengeneza miundombinu itakayowalazimisha kupita hapa ili nyinyi mtengeneze fedha, ukishakuwa na bandari 3 kubwa, Bandari ya Tanga, Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Mtwara ni uchumi, bado bandari ya Zanzibar na Pemba, tuna bandari 5 katika nchi moja. Tukivitumia hivi vyote Tanzania ni Tajiri, tukitumia bandari yetu kutoka Moa hadi Msimbati zaidi ya kilometa 1,424, Zanzibar yote na Pemba imezungukwa na maji, Mafia Maji, Mwanza hii imezungukwa na maji, ziwa Victoria asilimia 51 lipo Tanzania, bado ziwa Tanganyika, ziwa Nyasa, bado na mito, sisi ni matajiri. Kwa hiyo ndugu zangu wajumbe tujielekeza katika mwelekeo huo wa kujitambua kuwa sisi ni matajiri, kwa hiyo mipango yetu tunapoipanga ambayo ni lazima itekelezwe na Serikali katika kipindi cha miaka 10 inayokuja iakisi utajiri wetu na ijielekeze kujenga uchumi wa Tanzania, Tanzania hoyeee.

===

Na katika hilo, nianze na sekta za kijamii, yaani afya, elimu na maji ambazo ndio msingi hasa wa kujenga nguvu kazi ya Taifa kwa ajili ya kuendeleza sekta zingine. Katika sekta ya afya, itafaa mwelekeo wetu uwe ni kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi kwa kuhakikisha kila Kata, Kijiji na Mtaa unakuwa na kituo cha kutolea huduma (health facility) na pia kujenga Hospitali za Wilaya kwenye Wilaya zote zilizosalia. Lakini la muhimu zaidi ni kupanua zaidi huduma za kibingwa (specialist services) hadi kwenye Hospitali za Mikoa. Kwenye elimu, tujielekeze kwenye kuinua viwango vya ubora wa elimu ya msingi na sekondari kwa kuongeza maabara na vifaa vya maabara, kuongeza walimu na kuboresha mitaala ili elimu iandane na mazingira halisi ya kitanzania na kuzalisha wahitimu wanaojitegemea.

Aidha, msukumo mkubwa uwe ni kuimarisha elimu ya ufundi na kuongeza zaidi idadi ya vyuo vya ufundi kama kitovu cha uhawilishaji wa teknolojia (technology transfer) na ukuzaji wa sekta ya viwanda. Kwenye Elimu ya Juu, hatuna budi kuhakikisha programu za mafunzo zinatolewa kulingana na mahitaji ya kisekta ya Taifa letu ili kuharakisha mageuzi ya kiuchumi. Vilevile, tuongeze uwezo wa Serikali kugharamia Elimu ya Juu kwa kuhakikisha kila mwanafunzi anapata mkopo. Muhimu zaidi, ni kuhakikisha mfumo mzima wa elimu unajengwa kwa kuzingatia mila na utamaduni wa kitanzania. Kwenye huduma ya maji, tuongeze vyanzo vya maji na kasi ya usambazaji ili kutosheleza mahitaji kwa asilimia mia moja (100), mijini na vijijini. Inawezekana haya ninayoyazungumza wengine wakasema haiwezekani, lakini nataka kuwaeleza ndugu zangu wajumbe wa NEC yanawezekana kwa sababu tupo kwenye Taifa Tajiri na sisi ni Matajiri.

Sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi zipewe msukumo mpya na wa kipekee, kwani ndizo kichocheo cha ukuaji wa sekta ya viwanda. Kuwepo na mikakati madhubuti ya kusimamia mnyororo mzima wa thamani kwa mazao yote ya kimkakati; kuanzia pembejeo, uzalishaji, mavuno, uhifadhi, usindikaji hadi masoko. Na utaratibu huu ufanyike kwenye mazao yote ya kilimo, ufugaji na uvuvi. Kwa sababu kuna wakati inafika hata mbegu za kupanda ni shida, inafika mahali hata mbegu za kupanda mahindi hapa tunaagiza nje. Suala jingine muhimu ni kuondoa kabisa utegemezi katika mbegu za mazao ya kilimo (seed dependency), ambapo kwa sasa, takriban asilimia 70 ya mbegu zinatoka nje. Hii ni aibu. Vilevile, tujenge Mfumo wa Ushirika ambao, pamoja na kuwa wa hiari, udhibitiwe na Serikali ili kumlinda mkulima. Tupunguze utegemezi wa mvua kwenye kilimo na kuongeza maeneo ya umwagiliaji. Kuwe na mikakati ya kuhamasisha na kukuza ufugaji wa samaki. Halikadhalika, tujizatiti kulifufua na kulikuza Shirika letu la Uvuvi la TAFICO na kutumia fursa za uvuvi wa bahari. Suala jingine muhimu liwe ni kukuza na kushamirisha zidi teknolojia ya kilimo (agro-mechanisation) na kuachana kabisa na matumizi ya jembe la mkono.

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Wajumbe wa NEC:

Katika miaka kumi ijayo, sekta ya viwanda iwe ndiyo nguzo kuu ya uchumi na mzalishaji mkuu wa ajira na bidhaa za viwandani (manufactured goods) ili kuchangia zaidi kwenye Pato la Taifa. Mnapokuwa na viwanda tatizo la ajira litapungua, kwa sababu vijana wetu ndio watakaoajiriwa kwenye viwanda hivyo. Jitihada zitaelekezwa kwenye kukuza teknolojia rahisi ya viwanda, hususan viwanda vidogo na vya kati na kuhakikisha kuwa hakuna bidhaa yoyote inayouzwa nje ya nchi bila kuongezewa thamani. Lakini lengo kuu liwe ni kuacha kabisa kuagiza nje bidhaa ambazo malighafi zake zinapakana hapa nchini kama vile nguo, viatu, mafuta ya kula, samani, nk. Ni aibu kwa nchi kama Tanzania imezungukwa na maji kila mahali lakini tunaagiza samaki kutoka nchi, ni aibu kwa nchi kama Tanzania ambayo ni ya pili Afrika kwa kuwa na mifugo mingi lakini bado tunaagiza viatu kutoka kwenye nchi ambazo hazina mifugo mingi, na wakati mwingine tunaagiza maziwa kutoka nje lakini ng’ombe wa Wagogo maziwa yao hatunywi. Sasa tujielekeze katika mwelekeo huo. Vilevile, kuwepo na mkakati mahsusi wa uhawilishaji wa teknolojia (technology transfer) kwa kuzingatia mahitaji mahsusi ya kisekta. Aidha, msukumo mkubwa uelekezwe kwenye ujenzi na uimarishaji wa vyuo vya ufundi na kuvitumia kama njia kuu ya uhawilishaji wa teknolojia, hususan teknolojia ya viwanda.

Katika sekta ya madini, lengo liwe ni kuhakikisha madini yote yanasindikwa na kuongezewa thamani kabla ya kuuzwa nje ya nchi na kuendelea kutoa kipaumbele na vivutio kwa wachimbaji wazawa, ili waweze kumiliki uchumi wa madini. Tusioneane wivu kwamba mzawa hawezi kuwekeza kwenye madini au kwenye nini, Vilevile, tuendelee kudhibiti soko la madini na kuongeza vituo vya mauzo, yaani mineral centres.

Kwenye sekta ya nishati, tujizatiti kuzalisha umeme wa kutosha na wa bei nafuu kwa kutumia vyanzo vyote tulivyonavyo kama vile maji, gesi asilia, upepo, jua, joto-ardhi na makaa ya mawe. Aidha, umeme usambazwe kwenye mitaa na vijiji vyote. Lengo kuu liwe siyo tu kutosheleza kwa ukamilifu mahitaji ya ndani lakini pia kuuza nishati ya ziada nje ya nchi.

Kuhusu sekta ya miundombinu ya usafiri na usafirishaji, tutaendelea kuboresha, kuimarisha, kuboresha na kupanua miundombinu ya barabara, reli, maji na anga. Mtandao wa barabara za lami utaendelea kupanuliwa hadi kwenye wilaya, mitaa na vijiji hili ndio liwe lengo letu katika miaka 10 inayokuja. Tukamilishe ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na Matawi yake yote kwenye ushoroba wa kati yaani kwenda Mwanza, Tabora, Kigoma, Isaka na tuunganishe mpaka Kigali (Rwanda); Lakini pia tufufue maeneo mengine, ile ambayo imefika Moshi tutaiendeleza ifike mpaka Arusha na ile ya Mpanda nayo tuiimarishe ili biashara iweze kufanyika kimkakati kwa manufaa ya Watanzania wote. Tuimarishe Reli ya Kati ya zamani na kuongeza ufanisi wa Reli ya TAZARA. Lengo kuu liwe ni kupunguza kwa zaidi ya asilimia hamsini matumizi ya barabara katika usafirishaji wa mizigo kwenye Shoroba zote kuu za Kati, Kusini na Kaskazini. Tutaendelea kuboresha na kuimarisha ufanisi wa Bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Zanzibar na Pemba ili kuongeza ushindani na Bandari zingine. Tuimarishe bandari kwenye Maziwa yote Makuu pamoja na kuongeza zaidi idadi ya meli ili kuimarisha biashara na nchi jirani. Napenda kuipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kununua meli mpya ambayo inafanya kazi, huu ni mfano mzuri wa kujitegemea wa kweli. Huu ni mfano wa kujitegemea wa kweli, kwa hiyo wakati ujao wanunue meli nyingine ziwe zinazunguka humu baharini zinakwenda Mtwara, zinakwenda Comoro, huu ndio utajiri na huu ndio Utanzania tunaoutaka. Zanzibar hoyee, Shein hoyeeee.

Kwenye usafiri wa anga, msukumo mkubwa uelekezwe kwenye ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege, kuongeza idadi ya ndege na mtandao wa safari za ndani na nje ya nchi, hususan safari za kimkakati zinazolenga kukuza utalii na biashara.

Waheshimiwa Viongozi;

Mabibi na Mabwana:

Katika sekta ya utalii, tujiwekee mikakati ya kuongeza zaidi mchango wake kwenye Pato la Taifa kwa kuboresha miundombinu kwenye vivutio vyetu na kuvitangaza ndani na nje ya nchi, hususan kupitia Balozi zetu za nje. Na kwa kweli, kipimo kimojawapo cha utendaji kazi wa Balozi zetu za nje iwe ni idadi ya watalii wanaowaleta nchini. Tujiwekee malengo ya watalii milioni kumi (10,000,000) kwa miaka kumi ijayo. Idadi ya Watalii Zanzibar imeongezeka na idadi ya Watalii Tanzania Bara imeongezeka.

Halikadhalika, tunataka sekta ya mawasiliano itoe mchango mkubwa zaidi kwenye Pato la Mataifa. Hivyo, hatuna budi kujizatiti na kuhakikisha Kampuni yetu ya Simu ya TTCL inamiliki angalau asilimia 50. Aidha, tuimarishe usalama wa mawasiliano na kusimamia Sheria ya Makosa ya Kimtandao.

Kwa upande wa masuala ya uhusiano ya kimataifa, tuendelee na sera yetu ya kutofungamna na upande wowote. Tuendelee pia kujenga na kuimarisha uhusiano na mataifa mengine lakini, muhimu zaidi, diplomasia ya uchumi iwe ndiyo msingi wa uhusiano wetu kimataifa. We must determine what we want in relating with other nations. Aidha, tutumie jiograifia yetu ya kimkakati na ushawishi wetu wa kihistoria, hususan kwenye Ukanda wa Kusini, katika kupeleka mbele ajenda yetu ya uchumi na maslahi mapana ya Taifa.

Katika sekta ya ulinzi na usalama, tuendelee kuimarisha ulinzi na usalama wa ndani na mipakani. Aidha, majeshi ya Ulinzi na Usalama yahusishwe kikamilifu katika kulinda Miradi mikubwa ya kimkakati. Aidha, majeshi ya JKT na Magereza yajihusishe zaidi na shughuli za uzalishaji pamoja utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kambi za JKT ziongezwe ili kila mhitimu wa Kidato cha Sita apate fursa ya kupata mafunzo ili kujenga uzalendo na moyo wa kujitolea. Vilevile, kila Gereza liwe na shughuli mahsusi ya uzalishaji, kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, ufundi au viwanda, kulingana na maeneo na fursa zilizopo. Wafungwa wote wafanye kazi ili wakidhi mahitaji yao na kuchangia kwenye uchumi wa Taifa.

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Wajumbe:

Natambua kuwa majadiliano haya ya leo ni ya siku moja na mtakuwa na masuala mengi ya kujadiliana. Hivyo, nisingependa kutumia muda wenu mwingi kwa kutoa Hotuba ndefu. Lakini, kama nilivyosema hapo awali, NEC ni Chombo kikubwa sana cha maamuzi. Mnapojadiliana na kufikia maazimio kuhusu Mwelekeo wa Sera za CCM kwa miaka kumi ijayo au Ilani ya 2020 – 2025, mnaamua pia kuhusu mustakabali wa Taifa letu. Hivyo, mtangulizeni Mungu na kuliweka mbele Taifa letu, ili tufikie mustakabali mwema. Baada ya kusema haya, sasa nafungua rasmi kikao cha majadiliano ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi. Nawatakia majadiliano na maazimio mema. Mwenyezi Mungu awabariki!

Kidumu Chama Cha Mapinduzi!