MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA 5 KUPITIA SHIRIKA LA TAIFA LA MAENDELEO (NDC)

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Prof. Damian Gabagambi akizungumza na waandishi wa habari alipofanya nao mahojiano, Makao Makuu ya Shirika, jijini Dar es Salaam.

Katika kuhakikisha Tanzania inafikia adhma ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linajivunia mchango wake katika ujenzi wa taifa kwa kipindi cha miezi 18 kutoka April 2018 hadi Disemba 2019.

Kwa kuzingatia juhudi, na nia ya dhati ya Mheshimiwa Rais wetu kipenzi, Dr. John Pombe Magufuli ya kujenga uchumi imara usio tegemezi, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) liko nyuma yake likifanya kazi kwa uadilifu na ubunifu mkubwa.

Shirika limefanikiwa kuongeza tija katika vipengele vifuatavyo.

UKUSANYAJI WA MAPATO:

“Kwa kipindi cha takriban  miaka miwili, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Shilingi 2.6 Bilioni hadi Shilingi 6.9 Bilioni sawa na 164.3% kutoka mwaka 2017 hadi 2019.” hayo yamesemwa na Prof. Damian Gabagambi wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari, mapema leo Makao Makuu ya Shirika, jijini Dar es Salaam.

Ongezeko hilo la mapato limeiwezesha Shirika kutoa gawio kwa Serikali kiasi cha shilingi 174 milioni.Prof. Gabagambi ameeleza kuwa Shirika limefanikiwa kujiendesha lenyewe kwa 100% bila ruzuku ya Serikali. 

UFUFUAJI WA MASHAMBA YA MPIRA:

Mkurugenzi Mwendeshaji, Prof. Damian Gabagambi, pia amegusia ufufuaji wa mashamba ya mpira akisema,  kwa sasa uzalishaji umeongezeka na kufikia tani 86.7 kwa kipindi cha miaka miwili ambapo hapo awali hakuna kumbukumbu zozote kutokana na muwekezaji wa awali aliyekua akisimamia shamba.

“Uzalishaji umeongezeka hadi kufikia tani 86.7 zenye thamani ya shilingi 210 milioni na kuajiri Watanzania 278,” ameeleza Prof. Gabagambi.

UUZWAJI WA MATREKTA:

Shirika limeweza kuuza matrekta 684 yenye thamani ya 30 Bilioni sawa na 83.2% ya matrekta 822 yaliyo wasili nchini.

“Kupitia mradi huu tumetengeneza ajira zaidi ya 2000 za moja kwa moja,” ameeleza Prof. Gabagambi.

UFUFUAJI WA KIWANDA CHA  KMTC:

Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Prof. Damian Gabagambi ameeleza kuwa kwa sasa kiwanda cha KMTC kinatengeneza vipuri vya matrekta na kuzalisha tela za tani 2.5 na 5 kwa ajili ya kuwarahisishia usafiri wakulima. 

Prof. Gabagambi amesema kuwa hadi sasa kiwanda kimetengeneza tela 35 na wanaishukuru Serikali kwa kuwapatia shilingi 500 milioni kama mtaji wa kuongeza uzalishaji.

MAGADI SODA:

Mradi wa Magadi Soda uliopo mkoani Arusha kwa sasa unafanyiwa Upembuzi Yakinifu baada ya Serikali kutoa kiasi cha Shilingi 1.72 Bilioni.

“Upembuzi yakinifu wa mradi wa magadi soda sasa unafanyika kwa kasi,” ameeleza Prof. Gabagambi.

MRADI WA MBAO MBADALA- MEDIUM DENSITY FIBRE BOARD (MDF): 

Prof. Gabagambi ameeleza kuwa Shirika limekuwa likiwaatamia vijana wa kampuni ya Edosama Hardware Limited kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha mbao za MDF.

Ameeleza kuwa kiwanda kitasababisha mchango wa misitu katika pato la taifa kupanda kutoka 3% hadi 15% na kutengeneza ajira zaidi ya 50,000.

Ameendelea kueleza kuwa mchakato wa kutengeneza kampuni baina ya NDC na Edosama umeshaanza na itaitwa Green Gold.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Prof. Damian Gabagambi amewashukuru waandishi wa habari na kuwaahidi kushirikiana nao kila hatua Shirika itakapopiga.