NDC yakabidhi matrekta 7 Wizara ya Kilimo

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limekabidhi matrekta 7 kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) katika hafla iliyofanyika Tamco, Kibaha mkoani Pwani.

Mgeni rasmi kwenye hafla ya makabidhiano alikua Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ( Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel.

Ili kuhakikisha jembe la mkono linaenda makumbusho, wizara yake imechukua matrekta 3 na 4 yakienda Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) iliyo chini ya wizara yake.

Akipokea matrekta hayo, Prof. Elisante Ole Gabriel ameipongeza TALIRI kwa uamuzi wake wa kuchukua matrekta kutoka NDC.

“Msicheze nayo, yatumieni,” alisema Prof Elisante Ole Gabriel.

Aliongeza kuwa wakifanikiwa kurejesha vizuri mkopo huo wa matrekta ataleta taasisi nyingine zilizo chini ya wizara yake kuja kukopa kutoka NDC.

Mpango wa wizara yake ni kuondokana na uhaba wa malisho, hivyo amesisitiza matrekta hayo yataenda kutumika kikamilifu kuzalisha majani katika shamba la Vikuge lililopo Kibaha.

“matrekta ya shamba la Vikuge sio za mkopo, tumeshalipia milioni 192,” alisema Prof. Elisante Ole Gabriel.

Nae Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Prof. Damian Gabagambi alisema, kupitia mradi wa matrekta wamedhamiria kupeleka jembe la mkono makumbusho.

“Matrekta haya yanapatikana hata kwa wakulima wadogo,” alisema Prof. Gabagambi

Ili kuweza kurejesha kwa haraka mkopo wa matrekta aliwasihi wanaochukua matrekta kuyatumia katika shughuli mbalimbali kama kusomba maji, kuni, kulima, kupanda, kumwagilia, na kuzalisha umeme.

“Hiki ni kiwanda,” alisema Prof. Gabagambi.

Alisema kuwa walianza kutoa trekta, plau na halo, ila kwa kuwajali wateja wao wameamua kuwaongezea bidhaa mpya kwani wameona wanahitaji zaidi ya hayo.

“Tumeshatengeneza tela, bado kuzisambaza,” alisema Prof. Gabagambi.

Kwa kuwajali wakulima, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kupitia mradi wake wa matrekta ya Ursus wamejipanga kuongeza bidhaa nyingine kama kisomba nyasi (bellar) kwa ajili ya wakulima wa nyasi, mashine za kupanda (planter), mashine za kupulizia dawa (boom sprayer) na mashine nyingine nyingi za kilimo.

“Tuziombe taasisi nyingine za kilimo na ufugaji zije tuwape matrekta,” alisema Prof. Gabagambi.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC aliwapongeza wafanyakazi wa shirika lake kwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha yote haya yanawezekana.