NDC yakabidhi Milioni Moja Uwezo Awards

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Prof. Damian Gabagambi akikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza, Shule ya Sekondari Airwing kwenye mashindano ya kuibua vipaji “Uwezo Awards” yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kupitia Mkurugenzi Mwendeshaji wake Prof. Damian Gabagambi wamekabidhi Shilingi Milioni Moja za Kitanzania kwa shule bora, Shule ya Sekondari Airwing, katika mashindano ya kuibua vipaji “Uwezo Award” yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mashindayo hayo yanaratibiwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Great Hope Foundation ambapo yamefanyika kwa msimu wan ne mwaka huu.

Akikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Prof. Damian Gabagambi ameipongeza taasisi ya Great Hope Foundation kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwasihi wapanue wigo wao.

 “Mradi wa Uwezo Award unaibua vipaji, vijana wanajitambua. Nawasihi wangeenda na elimu ya juu maana vijana wanamaliza vyuo wanakaa miaka mitano hawana ajira,” alisema Prof. Gabagambi.

Naye Mratibu wa mashindano hayo Noela Mauvi amelipongeza Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa zawadi hiyo na kuwasihi wadau wengine wajiunge ili kuwasaidia vijana kuinuka.

Amesema kuwa vijana wengi wana vipaji ila hawajui pa kuanzia au wanakosa msaada wa kuwawezesha kufikia malengo yao.

Naye mwakilishi kutoka Shule ya Sekondari Airwing, Novatus Mjarifu, amelishukuru Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa zawadi yao na kuwa ahidi hawatajutia zawadi waliyoitoa.

“Majaji waliona mradi wetu unafaa (kuwasaidia watumiaji wa madawa ya kulevya) na hivyo kutuchagua kuwa mshindi wa kwanza, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) halitajutia kwa zawadi yao,” alisema Mjarifu.

Hii si mara ya kwanza kwa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kurudisha kile inachokipata kwa jamii kwani imekua ikichangia shughuli mbalimbali za kimaendeleo.