NDC yashiriki Maonesho ya Wakulima (NANENANE)

Mfanyakazi wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Florian Mramba akitoa maelekezo kwa wahudhuriaji wa Maonesho ya Nanenane walio tembelea banda la NDC.

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limeshiriki kwenye Maonesho ya 27 ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika mkoani Simiyu kwenye viwanja vya Nyakabindi.

Katika maonesho hayo yaliyofunguliwa tarehe 1 na Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limejizatiti kuonesha miradi miwili ya kimkakati inayolenga kuwainua Watanzania kiuchumi.

Miradi hiyo ni matrekta aina ya Ursus ambayo yanaunganishwa na Shirika hilo eneo la Kibaha mkoani Pwani. Mradi wa pili ni viuadudu vya kuangamiza viluwiluwi wa mbu waenezao magonjwa hatarishi kama malaria, dengue, zika na mengineyo yanayotokana na mbu ambavyo huzalishwa na kiwanda cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL).

Kupitia matrekta ya Ursus, Shirika limelenga kuwainua Watanzania kwa kuwakopesha matrekta kwa bei nafuu ya Shilingi 4,537,000/= tu.

matrekta yanayokopeshwa ni ya Horse Power (HP) 50 ambayo unapata jembe pamoja na haro na hakuna riba yoyote wakati wa marejesho.

Kupitia kiwanda cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL), Shirika limelenga kutokomeza malaria na magonjwa mengine yanayo sababishwa na mbu kupitia viuadudu vya Bactivec na Griselesf.

Viuadudu hivi vinapatikana katika ujazo tofauti, Bactivec kikiwa kwenye ujazo wa mililita 30 ambayo hutumika kwa matumizi ya majumbani na Griselesf yenye ujazo wa lita 20 ikitumika kwa matumizi makubwa.