Ndugai aula treka la Ursus

Azma ya kupeleka jembe la mkono makumbusho inazidi kupiga kasi baada ya Spika wa Bunge la Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kukabidhiwa trekta na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) mkoani Dodoma.

Katika hafla iliyofanyika Mbande, Dodoma, Spika Job Ndugai amelipongeza Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa mradi wao wa matrekta kwani unalenga kuwainua Watanzania kiuchumi.

“Niwashukuru Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa kunikabidhi trekta hili aina ya Ursus,” alieleza Spika Ndugai.

Aliendelea kueleza kuwa amechukua trekta la Horse Power 75 kwa njia ya mkopo na kusifu utaratibu huo.

“Niwapongeze NDC kwa utaratibu huu ambao unamuwezesha mteja kulipa kidogo kidogo,” alieleza Spika Ndugai.

Aliwasihi wakazi wa Kongwa kuchangamkia matrekta yanayouzwa na NDC.

“Niwashi wapiga kura wangu wa Kongwa kuchangamkia matrekta haya,” alieleza Spika Ndugai.

Katika kuona umuhimu wa matrekta ya Ursus, Spika Ndugai alieleza kuwa matrekta hayo ni kiwanda kwani yanaweza kufanya shughuli zaidi ya moja.

“Inaweza kupukuchua mahindi, alizeti, kusomba mazao, faida za trekta ni nyingi,” alieleza Spika Ndugai.

Spika Ndugai hakuwa mbali na kaulimbiu ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Prof. Damian Gabagambi ya kuhakikisha jembe la mkono linatokomezwa kabisa.

“Lengo ni kuhakikisha jembe la mkono linaenda makumbusho na tunaweza kufanya hivyo kupitia trekta,” alieleza Spika Ndugai.

Aliwasihi Watanzanja wote kuungana na NDC kukopa matrekta.

“Tukope matrekta na tulipe kwa wakati ili kuwawezesha NDC kuleta matrekta mengine kwa ajili ya watanzani,” alieleza Spika Ndugai.

Nae Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Prof. Damian Gabagambi alieleza kuwa mpaka sasa wameshasambaza matrekta 442 nchi nzima huku mkoa wa Dodoma ukiwa na matrekta 28 na wilaya ya Kongwa inayo ongozwa na Spika Job Ndugai ikiwa na matrekta 11.

Aliendelea kueleza kuwa matrekta haya yakitumika ipasavyo yatasaidia kuwa na chakula cha ziada.

“Matrekta haya yatasaidia kutulisha sisi, viwanda vyetu pamoja na majirani,” alieleza Prof. Gabagambi.

Ili kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wa kati, Prof. Gabagambi aliongeza kuwa hii ni NDC mpya inayolenga kutekeleza miradi yake hasa mradi wa matrekta.

“NDC ya sasa ni ya tofauti na kupitia uzoefu tulioupata katika mradi huu (matrekta) tutatekeleza miradi mingine,” alieleza Prof. Gabagambi.

Huu ni mpango kabambe wa kuhakikisha Tanzania inafikia azima ya uchumi wa kati kupitia sekta ya kilimo, ikumbukwe kuwa mwezi Mei mwishoni, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) iliwakabidhi matrekta 7 Wizara ya Kilimo pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI).

Matrekta ya Ursus huunganishwa na kuuzwa kwa mtu mmoja mmoja pia kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za kifedha nchini Tanzania.