SERIKALI KUJIKITA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MCHUCHUMA NA LIGANGA

WAZIRI Mkuu Mhe Kassim Mjaliwa amemtaka waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwaijage kuwekeza nguvu zote katika utekelezaji wa miradi ya umeme wa makaa ya mawe ya Mcguchuma na Chuma cha Liganga ili kuimarisha miundo mbinu chochezi kwa uwekezaji wa viwanda nchini.
Wito huu umebainishwa wakati waziri Mwijage alipokuwa akiongea na waandishi wa habari baada ya kikao na wawekezaji wa ubia katika miradi hiyo kampuni ya Kichina Sichuan Hongda Group (SHG) kwa ushirikiano na serikali kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Wakati nchi ikiendelea kuwekeza katika umeme wa gesi na maji, Mradi wa Mchuchuma utazalisha umeme wa MW 600 kutokana na makaa ya mawe chanzo ambacho hakiathiriwi na mabadiliko ya tabia nchi alisema Waziri Mwijage
Kati ya hizo MW 250 zitatumika katika kiwanda za uzalishaji chuma cha Liganga na MW 350 zitapelekwa kwenye grid ya Taifa ya umeme
Akielezea mahitaji ya mradi Mkurugezi Mwendeshaji wa NDC Bw Mlingi Mkucha amesema miradi unagharimu Dola za Kimarekani bilioni 3 zinazotolewa na SHG kati ya hizo Dola billion 1.3 zitatumika kwenye mradi wa Mchuchuma wakati Dola bilioni 1.7 zitaelekezwa kwenye mradi wa uchimbaji chuma cha Liganga
“SHG wametuhakikishia uwezo wa kifedha kulipa fidia kwa wakazi wa Ludewa mkoani Njome wataoathiriwa na miradi ili kupisha utekelezaji wa mradi “ Alisisitiza Mkucha
Kutokana na taarifa ya tathimini jumla ya wakazi wa vijiji 9 wakiwemo wa vijiji vinne vya Ilongi, Mnyusi A, Myorua na Amani vilivyopo Mchuchuma na vingine vitano vya Nkomang’ombe, Idusi, Ntiule, Mhambalasi na Kilomus vilivyopo Liganga wilaya ya Ludewa watalipwa fidia ya Tshs 13.5 bilioni ili kupisha mradi.
Mradi unatemea kuanza mara baada ya kumalizika kwa taratibu za kulipa fidia alisisitiza waziri huku akiongeza kuwa tayari wawekezaji wana jumla ya Dola billion 300 ambazo zimeshaletwa nchini ili kuanza utekelezaji wa miradi hiyo.
Pamoja na kuchimba chuma, Mradi wa Mchuchuma na Liganga utahusisha ujenzi wa Kinu cha Umeme chenye uwezo wa Megawati 600 alisema Mhe. Mwijage.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayosimamia Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambaye pia ni Mtaalam katika masuala ya madini, Mhe. Dkt. Dalaly Kafumu amesema kuwa, lengo la kuwajengea makazi wakazi wa maeneo ya mradi huo ni kuwawezesha wakazi hao kuwa na uhusiano mzuri na mgodi unaotarajiwa kujengwa.
‘’Serikali imeamua kuwajengea makazi wananchi ambao wanazunguka mradi Ili kuepusha wakazi hao kutumia pesa watakayolipwa kama fidia kwa matumizi mengine na kukosa makazi baadaye kuja kuilaumu Serikali kwamba imewadhulumu kwa kutowapa pesa za kutosha za kujenga nyumba”, alisema Dkt. Kafumu.

Pia katika kuhakikisha nchi inanufaika uwekezaji huuserikali itahakikisha kwa ushirikiano na mwekezaji kutoa mafunzo kwa vijana ili waweze kuajirika kwenye miradi
“Kampuni hii ni ya ubia kati ya Tanzania na China, tuna mamlaka sawa, tuna Wakurugenzi wetu wa Tanzania ndani ya hiyo kampuni hivyo tutashirikiana kuwafundisha vijana wetu wa kitanzania kwa ngazi tofauti za teknologia ili kama nchi tuweze kushiriki na sio kuwa watazamaji”, alisema Mhe. Mwijage.
Pia Mhe. Mwijage amesema kuwa katika mradi huo, Tanzania itakuwa na hisa asilimia 20 na Mwekezaji kutoka China atakuwa na asilimia 80, lakini hisa za Tanzania zinaweza kuongezeka hadi kufikia 45.
………………………..END………………