NDC kuinua kilimo Tabora

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mh. Aggrey Mwanri kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) amekabidhi matrekta 14 kwa vyama vya ushirika vya mkoa huo (Igembesabo) katika hafla iliyofanyika wilayani Igunga mkoani Tabora.

Mbali na vyama vya ushirika, Mkuu wa Mkoa amekabidhi matrekta kwa watu binafsi wakiwemo Mapadri, Maaskofu na Masheikh wa mkoa huo.

Amesisitiza matrekta hayo yatumike katika shughuli za kuleta maendeleo kwa mkoa na taifa kwa ujumla.

“Sio unachukua trekta unaenda kulipaki. Trekta hili linaweza kufanya shughuli nyingi za kimaendeleo, hivyo mfanye maendeleo,” alisema Mwanri

Pia amelishukuru sana Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa utayari wake wa kutoa matrekta.

“Katika hili NDC hawajaleta urasimu, wamekua tayari kutoa matrekta haya kwa mkopo na niviombe vyama vya ushirika, mwaka huu hatutanunua suti mpaka tulipe deni hili,” alisema Mwanri

Amevitahadharisha vyama ambavyo havitoweza kulipa madeni ni heri wasichukue maana atasimamia mpaka mwisho kuhakikisha mkopo huo unalipwa na matrekta hayo yanawaletea maendeleo wana Tabora.

Nae Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora, Mzee Hassan Wakasubi amesisitizia juu ya kuyatumia matrekta hayo kibiashara.

“Mkoa wa Tabora una maeneo mengi mazuri kwa kilimo, sio unachukua trekta unaenda kulalia kisa msimu wa kilimo uneisha, kuna sehemu nyingi tepetepe, kalime mbogamboga, kalime mazao yanayopatikana mkoani humu, kasombe kuni. Huu ni mkopo inapaswa tuurejeshe,” alisema Wakasubi.

Mbali na kulishukuru Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa mpango wake wa kutoa matrekta kwa wakulima, ameliomba shirika hilo kuchangamkia fursa nyingine za uwekezaji zinazopatikana katika mkoa wa Tabora.

“Mkoa wa Tabora una fursa za uwekezaji kwenye wilaya zake zote katika sekta ya nyama, asali, ngozi na tumbaku huku tumbaku ikiongoza kwa 60% kuzalishwa nchini, hivyo nawaomba NDC mje muwekeze kwenye viwanda hivyo,” alisema Mwanri.

Aliendelea kueleza kuwa ngozi inayopatikana mkoani humo ni malighafi nzuri na inakosa soko kutokana na kutokuwepo kwa kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi.

“Nilikuja hapa nikakuta ngozi inauzwa shilingi 500, nikawauliza vijana wakaniambia hamna kiwanda cha kupeleka malighafi hiyo. Hivyo nawasihi sana Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) mje muwekeze,” alisema Mwanri.

Katika zao la pamba Wilaya ya Igunga inazalisha 94% huku wilaya nyingine zilizobaki za Nzega, Uyui, Urambo na Kaliua wakizalisha 6%

Meneja wa Uwekezaji kutoka Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Bwana, Said Tunda amesema kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wanakabidhi matrekta 14, huku saba yakiwa ya vyama vya ushirika (Igembesabo) na 7 yaliyosalia kwa watu binafsi wakiwemo Mapadri, Wachungaji na Masheikh.

Aliendelea kueleza kuwa matrekta hayo yanaweza kufanya shughuli nyingi mbali na kilimo, linaweza kusomba kuni, kuvuta maji na shughuli nyingine nyingi.

Pia amesema kuwa matrekta hayo yakefungwa kifaa maalum cha kuyafatilia ili kuepusha wizi na kufatilia kama mkulima analitumia ipasavyo.

“Matrekta haya yamefungwa kifaa maalum ambacho kinafatilia shughuli zote zinazofanywa na trekta hilo, ukilitoa hapa Igunga ukapeleka Uyui tunaliona na tunaweza kulizima,” alisema Tunda.

Kutokana na minung’uno kutoka kwa washiriki, Bwana Said Tunda alifafanua zaidi kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuepusha matumizi yasiyo sahihi na kuepusha wizi kwani wana uwezo wa kuliona popote linapoenda.

“Ila baada ya kumaliza deni lako, tunakuwekea program hiyo kwenye simu yako na unaweza kulifatilia mwenyewe,” alisema Tunda.

Matrekta yaliyogawiwa kwa vyama vya ushirika na watu binafsi ni aina ya Ursus ambayo yanaunganishwa Mkoani Pwani na kampuni ya Ursus ambayo ni ubia baina ya Serikali ya Tanzania na Poland.