UWEKEZAJI KATIKA UBUNIFU KUCHOCHEA MAENDELO AFRIKA

Wahudhuriaji wa Kongamano la Ubunifu kutoka nchi mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa ngongamano hilo lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wakati Dunia ikiendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali zitokanazo na kukua kwa ongezeko la watu, ikiwemo za kimazingira pamoja na za kiafya watalaam pamoja na wanasayansi wamekubaliana kwa pamoja namna pekee ya kukabiliana na changamoto hizo ni kuhakikisha Dunia inawekeza katika Ubunifu.

Haya yamebainishwa  leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mwendeshaji wa shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Prof. Damian Gabagambi  katika mkutano wa kimataifa unaowashirikisha wadau kutoka nchi mbalimbali Duniani ambao wanakutana hapa nchini kujadili namna ubunifu unavyoweza kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Dunia kwa hivi sasa.

“Teknolojia inabadilika kwa haraka sana kwahiyo sio vizuri tukawa kama zamani tukawa watazamaji,” amesema Prof. Gabagambi.

Kwa kutambua mchango wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) katika ukuzaji wa teknolojia, Prof. Gabagambi amewakaribisha wahudhuriaji wa mkutano huo kutembelea kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuangamiza viluwiluwi wa mbu (TBPL) kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

   ”hata sisi Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) hatupo nyuma kuhimiza maendeleo, nimewaalika wahudhuriaji wa mkutano huu kutembelea kiwanda chetu cha TBPL kujionea teknolojia iliyopo ya kuzalisha viuwadudu vya kuangamiza viluwiluwi wa mbu,” amesema Prof. Gabagambi.

Akifungua Kongamano hilo kwa niaba ya waziri wa viwanda na biashara Prof Gabigambi amesema ni vyema mitaala ya elimu nchini ikajikita katika kuwekeza maarifa ya ubunifu hali itakayosaidia wahitimu kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili Dunia.

“Ni vizuri mfumo wetu wa elimu ukafanyiwa mabadiliko mabukwa,” amesema Prof. Gabagambi.