ZIMBABWE YAJIFUNZA KUTOKA TANZANIA

Balozi wa Zimbabwe nchini Cuba, Mr. Ignatius Graham Mudzimba ametembelea kiwanda cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL) kilichopo Kibaha mkoani Pwani katika ziara ya kikazi iliyofanyika tarehe 10 Disemba 2019.
Ziara hiyo imelenga kujionea na kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanywa na kiwanda cha TBPL hapa nchini katika mapambano dhidi ya Malaria. Balozi Mudzimba aliambatana na wenyeji wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Prof. Damian Gabagambi, Mwenyekiti wa Bodi ya TBPL Prof. Madundo Mtambo na wajumbe wengine kutoka Tanzania.

TBPL ni kiwanda cha kuzalisha viuadudu mahususi kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya Mbu waenezao magonjwa mbalimbali kama Malaria, Dengue, Chikungunya na magonjwa mengine yaenezwayo na Mbu. Kiwanda hiki kinamilikiwa na NDC kwa asilimia 100.