Bashungwa atembelea TBPL atoa maagizo

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa akitoa maelekezo alipo tembelea Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL)

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amekiagiza kiwanda cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) kuhakikisha kina tokomeza malaria kwa kuongeza kasi ya kutafuta masoko ya viuadudu.


Ameyasema hayo mapema leo alipo tembelea kiwanda hicho Kibaha, mkoani Pwani katika ziara ya kikazi. Amesema kuwa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kupitia kiwanda chake cha TBPL wanaweza kuliteka soko la ndani na la nje hasa la SADC iwapo wataweka mikakati madhubuti. “Nakuagiza Katibu Mkuu Viwanda (Prof. Riziki Shemdoe) uangalie jinsi gani NDC inavyoweza kushirikiana na MSD kuteka soko la SADC,” amesema Bashungwa.


Nae Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Prof. Damian Gabagambi amesema kuwa wanatumia mbinu mbalimbali kutafuta masoko licha ya changamoto ndogo ndogo zinazo jitokeza. Amesema kuwa matarajio yao ni kwamba Serikali itaunda timu ya maridhiano kutatua changamoto zinazo wakwamisha.


Kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu (TBPL) kinamilikiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa 100% na kilizinduliwa rasmi mwaka 2015 na Rais Mstaafu wa Awamu ya 4, Jakaya Mrisho kikwete na Waziri Mkuu wa kipindi hicho wa Ethiopia, Mh. Hailemariam Desalegn.


Pamoja na mambo mengine, Waziri Bashungwa amewataka NDC kupitia kiwanda chake cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL) kuzalisha viwatilifu vya kuangamiza wadudu wasumbufu katika mazao ya biashara. “Teknolojia ni ileile, nawaagiza pia mjikite katika kuzalisha viwatilifu kwa kutumia kiwanda hiki,” amesema Bashungwa.


Lengo ni kuwasaidia Watanzania kujenga uchumi wa viwanda na kutengeneza ajira kwa kupunguza gharama za kuagiza viwatilifu nje ya nchi. “Tunataka fedha tulizotenga kwenye pamba na korosho zibaki hapahapa,” amesema Bashungwa. Kwa kuitikia wito huo Prof. Gabagambi amemshukuru Waziri kwa kuwapa mwanga na ameahidi kujipanga zaidi. “Tunamshukuru Waziri kwa kutupa njia, tutakaa na wenzetu (Wacuba) kuona jinsi gani tunateka soko,” amesema Prof. Gabagambi.