HATUTAKI YA KARIAKOO YATOKEE NDC

Wafanyakazi wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), leo wamepata mafunzo ya kukabiliana na majanga, hasa janga la moto, mafunzo yaliyo endeshwa na wafanyakazi wa NDC, Sadick Nembo pamoja na Robert William, zoezi lililo fanyika kwenye ofisi za NDC, Posta, jijini Dar es Salaam.

 

Wafanyakazi hao walifundishwa aina za mioto, namna ya kujikinga, tahadhari za kuchukua ili kuepukana na moto, pamoja na namna ya kukabiliana na moto pindi unapotokea. Mbali na hivyo, wafanyakazi wa NDC walifundishwa namna ya kutumia na kutunza vifaa vya umeme wawapo kazini au nyumbani ili kuhakikisha wanazuia matukio yanayoweza kusababishwa na moto.

 

 

Wafanyakazi wa NDC wakifundishwa namna ya kukabiliana na moto wawapo kazini au nyumbani. 


 “Leo wafanyakazi wa NDC wamefundishwa namna ya kukabiliana na moto pindi unapotokea, na elimu hii itawasaidia wawapo kazini au nyumbani,” ameeleza Robert William, mkufunzi wa zoezi hilo.

 

Aliendelea kueleza kuwa janga la moto linaweza kuzuiwa kwa kutumia vizuri vifaa ya umeme kwa kuhakikisha vinazimwa pale ambapo havitumiki na kuvikagua mara kwa mara. “Unapomaliza shughuli zako ni vyema ukazima taa au swichi ya umeme.”

 

Pia, wafanyakazi hao wameoneshwa maeneo wanayoweza kukimbilia pindi moto unapotokea (Assembly point), pamoja na vifaa wanavyoweza kuvitumia moto unapotokea kazini.

 

“Pale moto unapotokea unaweza kutumia vizima moto (fire extinguisher), mchanga au kama moto bado upo hatua za awali unaweza kutumia kitambaa kizito kuuzima,” amee;eza Sadick Nembo, mkufunzi wa zoezi hilo.

 

Sambamba na hilo amewaasa wafanyakazi wa NDC pamoja na umma kutohamaki pale moto unapotokea bali wawe watulivu ili kuipa akili kuweza kufanya maamuzi sahihi ikiwemo kutafuna mbinu za kuzima moto husika na kuwaita Jeshi la Zima Moto na Uokoaji.

 

Mafunzo haya ni sehemu ya kuwajengea ujuzi wafanyakazi wa NDC ambapo hufundishwa stadi mbalimbali zikiwemo; uchumi, maisha ya kazi na nje ya kazi, biashara, afya na mambo mengine mengi.