KAMATI YA BUNGE YATEMBELEA KONGANE YA VIWANDA TAMCO

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira yasifu kazi kubwa inayofanywa na NDC kutafuta wawekezaji

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kama serikali inazichukua changamoto zote zinazozikabili kiwanda cha - GF Assemblers Ltd pamoja na kiwanda cha Hester Bioscience Africa Limited na kuahidi kuzifanyia kazi ili viendelee kuzalisha Kwa tija nchini.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo  alipotembelea Kongane ya Viwanda ya TAMCO, Kibaha Mkoani Pwani wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira ambapo amesema dhima ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona mazingira wezeshi kwa wawekezaji yanazingatiwa na kuondoa changamoto zinazowakabili. 

Dkt. Kijaji Amesema serikali itahakikisha inashirikiana na kamati ya Bunge la Tanzania katika kujadili changamoto za wawekezaji pamoja na kupata majibu ya pamoja ili kuwawezesha kufikia masoko ya nje.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mmwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe amesema eneo hilo la TAMCO lilianzishwa kwa lengo la ujenzi wa viwanda huku shirika hilo likiendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia wawekezaji.

Awali wakiwasilisha changamoto zao mbele ya kamati hiyo Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha Hester Bioscience Africa Limited na Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kuunganisha magari Cha GF Assembers Bw. Ezra Mereng wamesema tatizo la umeme bado ni changamoto kwao.

 Eneo la TAMCO wilaya ya kibaha, Mkoani Pwani limeanzishwa mwaka 1978 likiwa na lengo la ujenzi wa viwanda vya kuunganisha magari huku likiwa na ukubwa wa hekali 230.

Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. David Kihenzile amepongeza kazi kubwa inayofanywa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwani wanesaidia ajira na mapato Kwa Serikali.

Mhe. Kihenzile ameongeza Kwa kusema kuwa changamoto zote zitafanyiwa kazi na kamati yake.