KAMATI YA BUNGE YATEMBEMBELEA ENEO LA UWEKEZAJI TAMCO

Yatoa maagizo mazito kwa Wizara ya Afya, Halmashauri

Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. David Kienzile wamefanya ziara ya kikazi katika Eneo la Uwekezaji la TAMCO lililopo Kibaha mkoani Pwani, eneo lenye ukubwa wa ekari 201.04 linalo milikiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).

Katika ziara hiyo, kamati hiyo ya bunge ilitembelea viwanda viwili, Kiwanda cha Kuzalisha viuadudu vya kuangamiza viluwiluwi vya mbu cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), kinachomilikiwa na Serikali kupitia NDC pamoja na kiwanda cha Kuzalisha Chanjo za Wanyama cha Hester Bioscience Limited.

Baada ya kupokelewa na baadhi ya Wafanyakazi wa NDC, kamati hiyo ilipata taarifa fupi kuhusu eneo la TAMCO kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa NDC, Bi. Rhobi Sattima, akiwaeleza kuwa eneo la TAMCO lina ukubwa wa ekari 201.04 ambapo Kitalu 645 hadi 646, ni kwa ajili ya viwanda vya dawa, eneo lenye ukubwa wa Heka 4.30.  Kitalu 647 hadi 648 nacho kikiwa ni kwa ajili ya kiwanda cha dawa, eneo lenye ukubwa wa Heka 8.95. Pia vitalu  659 hadi 670, 672, 674 hadi 677, 679 hadi 699 na 700 hadi 704 vikiwa ni kwa ajili ya viwanda vya nguo, eneo lenye ukubwa wa Heka 77.41 huku vitalu  654 hadi 656 na 658, vikiwa ni kwa ajili ya viwanda kwa ajili ya magari, eneo lenye ukubwa wa heka 26.28.

Pia aliwaeleza kuwa kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuangamiza viluwiluwi vya mbu ni cha kipekee Barani Afrika na licha ya kuzalisha viuadudu hivyo pia kinatarajia kuzalisha viuatilifu kwa ajili ya kuangamiza wadudu waharibifu kwenye mazao ya korosho, pamba na mazao mengine.

“Tunatarajia kuzalisha viuatilifu vya kuangamiza wadudu waharibifu na tumeshatengeneza dawa za majaribio,” alieleza Bi. Rhobi Sattima, Kaimu Mkurugenzi wa NDC. Mbali na hivyo, pia aliieleza kamati hiyo ya bunge kuwa wanampango wa kuzalisha mbolea za kibaiolojia kupitia kiwanda hicho.

Baada ya kamati hiyo ya bunge kumaliza kutembelea kiwanda cha TBPL, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira, Mhe. Eric Shigongo, alitoa maagizo kwa Wizara ya Afya pamoja na Halmashauri kununua mara moja viuadudu vinavyozalishwa kiwandani hapo ambavyo vinalenga kutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria. “Wizara ya Afya na Halmashauri zetu lazima zilitazame suala hili kwa umakini na haraka sana waje kununua viuadudu hivi,” alieleza Mhe. Eric Shigongo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira.

Alieleza kuwa anashangazwa na Wizara ya Afya pamoja na Halmashauri kushindwa kununua dawa hizo licha ya maagizo yaliyotolewa. Ikumbukwe kuwa mwaka 2017, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maagizo kwa Halmashauri zote nchini kununua viuadudu hivyo vya kuangamiza viluwiluwi vya mbu kutoka TBPL.

Katika kiwanda cha Hester Bioscience, kamati ya bunge ilielezwa kuwa kiwanda hicho kinatarajia kuzalisha chanjo 26 za wanyama huku jumla ya gharama za ujenzi wa kiwanda hicho mpaka kukamilika inakadiriwa kuw Dola za Kimarekani Milioni 18 sawa na bilioni 42 za Kitanzania.

“Tunatarajia kuzalisha chanjo aina 26 za wanyama kama kuku, ng’ombe, nguruwe, mbuzi nk,” alieleza Tina Sokoine, Mratibu wa kiwanda hicho.

Kutokana na hatua iliyopigwa na kiwanda hicho, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira, Mhe. Eric Shigongo alisema kuwa kiwanda hicho kitasaidia Watanzania kufuga kisasa kwani wana uhakika wa kupata chanjo za mifugo yao pale magonjwa yatakapo jitokeza.