
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mnamo tarehe 18. Machi 2018 alimteua Prof.
Damian Gabagambi kuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo
(NDC). Akitokea Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA),
Morogoro. Toka kuteuliwa kwake Prof. Damian Gabagambi amekuwa kiongozi wa mfano
katika kutekeleza majukumu ya NDC kwa weledi na ufanisi mkubwa akitamani kuiona
NDC kama mkono wa uwekezaji wa Serikali ikifanikisha azma ya Tanzania ya
Viwanda; hakika alipenda kuiona NDC mpya iliyojaa ubunifu.
Wakati
wa utumishi wake akiwa NDC, Prof. Damian Gabagambi alisimamia kwa nguvu zote na
kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo ndio dhima kuu ya Shirika la
Taifa la Maendeleo (NDC).
Miradi
hiyo ya kimkakati ni pamoja na Mchuchuma na Liganga uliopo Ludewa Mkoani Njombe,
Makaa ya Mawe Ngaka yaliyopo mkoa Ruvuma, Magadi Soda, Engaruka mkoa wa Arusha. Miradi hiyo ni kichocheo
kikubwa kwa maendeleo ya viwanda nchini.
Pia,
Prof. Damian Gabagambi alifanya kazi kwa juhudi bila kuchoka na mara zote
alipenda kutuasa kufanya kazi kwa bidii huku tukitanguliza maslahi ya Shirika
na Taifa mbele. Daima atakumbukwa kwa kutuachia Mpango Mkakati wa Shirika wa miaka
5 (5 Years Strategic Plan). Kwa hakika kiu na maono yake ya kutaka kupeleka
jembe la mkono makumbusho ilikua ni kubwa na hili limethibitika kwani, Mpango
huu chini ya uongozi wake umewezesha matrekta kupatikana kwa bei nafuu na
kusambazwa sehemu mbalimbali nchini.
Miradi
mingine iliyotekelezwa katika Shirika kwa ufanisi chini ya uongozi wa Prof.
Damian Gabagambi ni pamoja na ujenzi wa miundombinu katika Maeneo Maalum ya Viwanda
(Industrial Parks), ikiwemo TAMCO Kibaha. Vilevile kuendeleza mashamba makubwa ya kuzalisha
malighafi za viwanda na usindikaji na juhudi mbalimbali za kufufua kiwanda cha
matairi cha General Tyre kilichopo Mkoani Arusha.
Prof.
Damian Gabagambi alikuwa na maono ya kuhakikisha kiwanda cha KMTC kinaboreshwa
na kuwa na uwezo wa kuzalisha vipuri kwa ajili ya matumizi ya mashine na
mitambo mbalimbali kwa lengo la kuongeza tija katika Sekta ya Viwanda nchini
ikiwa ni pamoja na kuokoa matumizi ya fedha za kigeni.
Prof. Damian Gabagambi alitumia muda wake
mwingi katika kuwaendeleza na kuwajengea wafanyakazi ujuzi ili waweze kumudu na
kutekeleza majukumu ya NDC kwa ufanisi mkubwa. Hakika alikuwa Kiongozi wa
Vitendo, Mnyenyekevu, Mwenye Kupenda Watu, Mchapakazi, Mzalendo na hivyo kuwa
mfano wa kuigwa kwa Shirika na Taifa.
Kuondoka
kwake kumeacha pengo kubwa lakini pia kuna mengi ya kujifunza kutokana na kazi
zake. Ingawa hatutakua naye kimwili, daima ataendelea kuishi kwenye mioyo yetu.
BWANA
ALITOA NA BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE.