Wizara
ya Viwanda na Biashara kupitia Taasisi yake ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara
Tanzania (TanTrade), inaandaa Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es
Salaam yatakayofanyika tarehe 28 Juni, hadi 13 Julai, 2021 katika Uwanja wa
Maonesho wa Mwl. J. K. Nyerere, Barabara
ya Kilwa, Dar es Salaam.
Lengo
la Maonesho haya ni kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi
pamoja na taasisi mbalimbali kutangaza biashara ya bidhaa na huduma, kujifunza
uzalishaji bora wa bidhaa kulingana na soko la kimataifa na kutengeneza
mitandao ya mawasiliano baina yao itakayowasaidia kukuza biashara na kupata
wabia kwenye biashara zao, ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Kauli
mbiu ya maonesho ya mwaka huu ni “Uchumi
wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu”. Kauli mbiu hii inalenga kutambua mchango
wa Sekta ya Viwanda katika kuchochea uzalishaji kwenye sekta mbalimbali za
kiuchumi ili kukuza biashara ya ndani na nje, kuongeza ajira na hivyo kuchangia
katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Sambamba
na Maonesho haya, Mikutano ya Kibiashara (B2B) itafanyika kwa njia ya mtandao (Zoom
Meetings ) ili kuwakutanisha wadau wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kutafuta
masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini yakiwemo mazao ya kilimo,
mifugo, uvuvi, misitu na madini.
Aidha
kutakuwa na huduma ya Kliniki ya Biashara, kwa wafanyabiashara ili kuboresha na
kuimarisha mazingira wezeshi ya ukuaji endelevu wa biashara nchini ikiwa ni
pamoja na upatikanaji wa teknolojia rahisi na za kisasa.
Pamoja
na maonesho ya jumla ya bidhaa mbalimbali maonesho ya mwaka huu yatakuwa na
maeneo matatu ya upekee kama ifuatavyo:-
Eneo
maalum litakalojulikana kama Kilimo Zone.
Eneo hili litatumiwa na Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Kilimo kama vile bodi
za mazao, wazalishaji wa pembejeo na teknolojia za kilimo pamoja na wadau
wengine wa kilimo walioko ndani ya nchi
ili kurahisisha upatikanaji wao katika eneo moja na kuwaunganisha wazalishaji
wa bidhaa hizo na masoko endelevu. Aidha, washiriki katika banda hili watapata
fursa ya kushiriki Mikutano ya Kibiashara kwa njia ya mtandao (Zoom Meetings) ili kuunganishwa na wadau wa
biashara ya mazao ndani na nje ya Nchi kwa lengo la kuunganishwa na masoko
pamoja na Teknolojia mbalimbali.
Pia
kutakuwa na mtaa wa madini utakaowashirikisha Wadau wote wa Sekta ya Madini ambao
ni pamoja na Wachimbaji Wadogo na Wakubwa, Watafiti na Masonara ili kupanua
fursa za masoko katika Sekta hii muhimu katika uchumi; na kutoa taarifa
mbalimbali kuhusu rasilimali hiyo kwa watembeleaji wa Maonesho. Pamoja na;
Pamoja
na mtaa wa viwanda vidogo vidogo na wajasiriamali kwa ajili ya kutoa fursa ya
kuonesha na kuuza bidhaa zao na kupata masoko ya ndani na nje ya nchi.
Pamoja uwepo wa changamoto ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona (Covid -19) unaoikabili dunia, hadi sasa nchi zipatazo saba (7) zimethibitisha kushiriki. Nchi hizo ni pamoja na China, Ghana, Kenya, Pakistan, Syria, India na Umoja wa Falme za nchi za Kiarabu (UAE). Makampuni yapatayo 54 kutoka nje ya nchi na 2,803 ya ndani ya nchi yamethibitisha kushiriki.
Hivyo,
naendelea kuwahamasisha Jumuiya ya Wafanyabiashara, Taasisi za Umma na Binafsi
pamoja na watoa huduma mbalimbali kutoka ndani na nje ya Nchi kujiandikisha
kushiriki Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, ili kutumia
jukwaa hili. Serikali imeandaa mazingira yatakayomwezesha mfanyabiashara
kujenga mtandao mpana wa biashara.