
Tarehe 9 Disemba, 2021 Tanganyika inatimiza miaka 60 ya Uhuru kutoka kwa Wakoloni. Mambo yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania kuanzia Awamu ya Kwanza
chini ya uongozi wa Hayati Mwalimu Julias Kambarage Nyerere hadi Awamu ya Sita inayoongozwa na mheshimiwa Samia Suluhu Hasan ni makubwa kiasi kwamba hayawezi kuelezwa katika kitabu kimoja. Makala hii, inaelezea kwa ufupi mafanikio ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965 chini ya Sheria ya Bunge “The National Development Corporation Act, No 69 of 1964,” Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC),
lilichukua nafasi na majukumu yaliyokuwa yakifanywa na the Tanganyika Development Corporation (TCD), ambayo yalikuwa ni kuanzisha na kuendeleza Viwanda Mama na Viwanda vya Kuongeza Thamani kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kama mkono wa Serikali katika uwekezaji.
Baada ya vipindi kadhaa vya mageuzi, mwaka 1996, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Waraka wa Baraza la Mawaziri Na 6/96 iliipa NDC majukumu mapya ambayo ni kusimamia viwanda vya msingi, kusimamia miradi mipya kwa kushirikina na wabia katika kuanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali kama waraka huo ulivyotamka;
“NDC – Shirika la Kuendeleza na kusimamia viwanda vya msingi. Ndilo Shirika mama lililoanzisha mashirika/ makampuni/ viwanda vyote nchini. Liendelee kumilikiwa na Serikali kwa 100% lisimamie miradi mipya kwa kushirikiana na wabia, liendeleze utekelezaji wa miradi ambayo haijamalizika kama vile Mchuchuma Coal, Liganga Iron and Steel pamoja na mradi wa Soda Ash.”
NDC inatekeleza miradi inayogusa sekta zote muhimu kama Kilimo, Madini, Afya, Viwanda, Nishati na Biashara. Baadhi ya miradi hiyo ni; Migodi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma, Ngaka na Katewaka; Chuma cha Pua, Liganga, Mradi wa Magadi Soda, Monduli, Arusha. Vilevile NDC inasimamia Bandari Kavu ya Nafaka, ETC Cargo, Dar es Salaam na Mashamba ya zao la Mpira yaliyopo Tanga na Morogoro. Pia NDC inamiliki kiwanda cha kuzalisha vipuri vya mashine na mitambo mbalimbali kilichopo mkoani Kilimanjaro cha KMTC.
Mbali na hayo, NDC inamiliki Kongane za Viwanda ambazo ni TAMCO, Kibaha mkoani Pwani, Kange mkoani Tanga, KMTC mkoani Kilimanjaro na Nyanza mkoani Mwanza. Shirika linawakaribisha wawekezaji kuhodhi maeneo haya, kwa kuwa nafasi bado zipo.
KIWANDA CHA KUZALISHA VIPURI NA MITAMBO KMTC
NDC inamiliki kiwanda cha kuzalisha vipuri vya mashine na mitambo mbalimbali cha KMTC kilichopo mkoani Kilimanjaro. Ni kiwanda cha kimkakati chenye lengo la kuziba pengo la upatikanaji wa vipuri vya mashine na mitambo mbalimbali nchini kwa kupunguza uagizwaji wa bidhaa hizo. Kiwanda hiki kinazalisha mashine na mitambo inayotumika kuongeza thamani mazao ya kilimo na misitu. Miundombinu ya kiwanda hiki imeboreshwa kwa kujenga mtambo wa kuweka gamba la zink kwenye bidhaa za chuma ili kuzuia kutu. Bidhaa hizi zinahusisha vyuma vitakavyotumika kwenye mawasiliano, ujenzi, kilimo na kusambaza umeme na kupunguza uagizaji wa bidhaa hizi nje ya nchi. Kiwanda kimetoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja 90.
SEKTA YA AFYA
Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linamiliki kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuangamiza viluwiluwi vya mbu waenezao malaria. Kiwanda hiki kimejengwa kwenye Kongane ya Viwanda ya TAMCO, Kibaha mkoani Pwani na ni cha kipekee barani Afrika.
Tangu kuzinduliwa kwake rasmi mwaka 2017, jumla ya lita 824,655 za viuadudu vyenye thamani ya Shilingi 10,154,441,537 Bilioni za Kitanzania zimeuzwa ndani na nje ya nchi kwenye nchi ya Niger, Mozambique, Angola, Kenya, Namibia, Botswana na Eswatini, huku jitihada mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha malaria inatokomezwa kabisa Afrika.
SEKTA YA NISHATI NA MADINI
Mradi wa Magadi Soda Engaruka uko eneo la, Monduli, Arusha na umelenga kuzalisha Magadi Soda yenye matumizi mbali mbali ya viwandani na nyumbani. Ndani ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, NDC inajivunia kukamilika kwa Upembuzi Yakinifu wa Mradi huu uliofanywa na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO), huku tathmini ikionesha kuna idadi ya lita za ujazo 3,294,704,894 ya Magadi Soda ambayo ni malighafi muhimu katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kwenye sekta za nguo, ujenzi, dawa na karatasi.
Sambamba na hilo, NDC inajivunia mchango wake katika ukuaji wa uchumi nchini kupitia Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka, Ruvuma unaoendeshwa kwa ubia baina ya NDC na Intra Energy (T) Limited. Mgodi huu unatoa nishati ya Makaa ya Mawe inayotumika kuendesha viwanda vya uzalishaji wa saruji, nondo, vigae, ujenzi na viwanda vingine hivyo kuchangia ajira na ukuaji wa mapato. . Pia makaa haya ya mawe yanauzwa kwenye nchi ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Zambia na hivyo kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
SEKTA YA UWEKEZAJI
NDC inamiliki Kongane za Viwanda maeneo mbalimbali nchini ikiwepo Kibaha - Pwani, Kange – Tanga, KMTC – Kilimanjaro na Nyanza – Mwanza. Kongane ya TAMCO, Kibaha yenye ukubwa wa ekari 201, imeendelezwa ikiwepo ujenzi wa miundombinu ya bara bara na usanifu wa barabara na industrial shades. Eneo la TAMCO limegawanywa katika maeneo matatu ya viwanda vya nguo, viwanda vya dawa na viwanda vya magari. Viwanda vilivyo jengwa hapo ni;
Hester Bioscience Africa
Kiwanda hiki ni mahususi kwa ajili ya uzalishaji wa chanjo za wanyama na mifugo mbalimbali. Chanjo zinazo zalishwa na kiwanda hiki zinauzwa ndani ya nchi na nje ya mipaka ya Tanzania na kimesaidia kupunguza gharama za uagizwaji wa chanjo hizo kutoka nje ya nchi. Kiwanda kimetoa ajira 200 za moja kwa moja kwa Watanzania na takriba ajira 1,000 zisizo rasmi.
Kiwanda cha GF Trucks Vehicle Assemblers
GF Trucks Vehicle Assemblers ni kiwanda cha wazawa kinachojihusisha na uunganishaji wa magari ya aina mbalimbali. Kwa sasa wanaunganisha magari aina ya
FAW ambayo yanatumika katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa miradi mikubwa ya nchi. Kiwanda hiki kimesaidia kupuguza uagizwaji wa magari nje ya nchi.
Kiwanda cha Vifungashio Global Packaging
Kiwanda cha vifungashio Global Packaging, kimejengwa kwenye Kongane ya Viwanda TAMCO. Kiwanda hiki ni cha ubia baina ya Wande Printing na NDC ambapo kwa pamoja wanaunda kampuni ya Global Packaging.
Kiwanda hiki kinazalisha vifungashio vyenye ujazo tofautitofauti ambavyo vinauzwa ndani na nje ya nchi, huku kikiwa kimetatua changamoto ya kuagiza vifungashio nje ya nchi na kimetengeneza ajira takriban 120,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
SEKTA YA KILIMO
Kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, tunajivunia mchango wa NDC kwenye Sekta ya kilimo kupitia matrekta yanayounganishwa Kibaha, Pwani. NDC imeshauza matrekta 766 yaliyolima jumla ya ekari 450,000 kwa kipindi cha miaka 3 hivyo kuchangia kwenye upatikanaji wa chakula nchini na ukuaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja.
Vile vile, NDC inamiliki mashamba ya zao la mpira yaliyopo Muheza, Tanga na Mang’ula, Morogoro. Mashamba hayo yametoa malighafi inayotumika kwenye viwanda vinavyo zalisha bidhaa za mpira ndani na nje ya nchi. Mashamba hayo pia yametoa ajira takriban 266 kwa wazawa wanaozunguka mashamba hayo hivyo kuchangia ukuaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja.
Jiunge nasi kuijenga Tanzania ya Viwanda.