
Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Prof. Damian Gabagambi
amefanya ziara ya kikazi kiwanda cha kuunganisha magari cha GFA
Assemblers kilichopo kibaha mkoani Pwani na kujionea kazi nzuri inayofanywa na
kiwanda hicho kipya.
Katika
ziara hiyo, amefurahishwa na karidhishwa na GFA Assemblers kwa kuunganisha
magari hapa nchini. Nae Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho, Ndg. Ezra Mereng amesema
kuwa kwa sasa wanaunganisha magari aina ya FAW lakini malengo yao ni kuunganisha
magari mengi ya kampuni mbalimbali ili kuendana na ushindani wa soko.
Wakiwa
wameanza kazi ya kuunganisha magari wiki moja iliyopita, kiwanda hicho
kimeshapata oda ya magari 10 kutoka hapa
nchini ikiwa ni mafanikio makubwa kwa kiwanda hicho. “Tumeanza kuunganisha
magari wiki moja iliyopita na tayari tumeshapata oda ya magari 10,” amesema Bw. Mereng, Meneja Mkuu wa kiwanda hicho.
Gari
zinazo unganishwa kiwandani hapo hupitia hatua 9 ndani ya eneo la uunganishaji na hatua ya
mwisho uhusisha upimaji wa ubora wa gari ikiwemo kuangalia uwezo wa breki,
ufanyaji kazi wa mfumo wa umeme wa gari pamoja na makosa ya kiufundi ambayo
yangeweza kutokea wakati wa uunganishaji wa gari.
Magari
hayo huunganishwa na Watanzania ambao wamepata ujuzi hapa nchini ikiwa ni
jitihada za kukabiliana na suala la ukosefu wa ajira hapa nchini. Mpaka sasa
kiwanda hicho kimetoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 70 huku lengo
likiwa ni kuongeza ajira kwa Watanzania wengi zaidi siku za usoni.
Nae
Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Prof. Damian Gabagambi amewapongeza wafanyakazi
wa kiwanda hicho na kuwasihi kufanya
kazi kwa bidii ili kujenga uchumi wa taifa, “nawasihi mfanye kazi kwa bidii
kwani kazi ndio msingi wa maendeleo kwa taifa,” amesema Prof. Gabagambi. Pia amekipongeza
kiwanda hicho kwa maono yao ya kuunganisha magari makubwa kwani kwa sasa taifa
lina miradi mingi ya kimaendeleo inayohusisha ujenzi hivyo magari hayo
yatapunguza uagizwaji wa magari kutoka nje ya nchi.
“Niwapongeze kwa kulenga muda muafaka wa kuzalisha magari haya kwani kwa sasa sekta kubwa ni sekta ya ujenzi, hivyo kuna uhitaji mkubwa wa magari haya,” amesema Prof. Gabagambi.
Kwa
siku za usoni, kiwanda hiki kitakuwa ni chachu kwa kiwanda cha KMTC kilichopo
mkoani Kilimanjaro ambacho ni mahususi kwa ajili ya kuzalisha vipuri vya
mashine na mitambo mbalimbali kwani kitasaidia kiwanda cha KMTC kupata soko la
vipuri vyake na kusaidia kujenga uchumi wa ndani kwa kutumia malighafi zinazo
zalishwa hapa hapa nchini.
Kiwanda
cha GFA Assemblers kimejengwa kwenye Eneo la Uwekezaji la TAMCO lililopo
Kibaha, mkoani Pwani, eneo hilo linamilikiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo
(NDC) likiwa ni mahususi kwa ajili ya uwekezaji katika Sekta ya Viwanda vya
aina mbalimbali.
Kwa
sasa eneo hilo lenye ukubwa wa hekari 201.63 lina kiwanda cha Kuzalisha
Viuadudu mahususi kwa ajili ya Kuangamiza Mazalia ya mbu, Tanzania Biotech
Products Limited (TBPL), Kiwanda cha Kuzalisha Vifungashio vya Mazao, Global
Packaging Tanzania Limited (GPTL), Kiwanda cha Kuzalisha Chanjo za Wanyama,
Heister BioScience, Kiwanda cha Kuunganisha Matrekta aina ya URSUS.
Mbali
na eneo la TAMCO, NDC inamiliki maeneo mengine ya uwekezaji yaliyopo Tanga - kange
Industrial Estate lenye ukubwa wa hekari 22.4, Kilimanjaro - KMTC Industrial
Estate lenye ukubwa wa hekari 229.13, Mwanza - Nyanza Industrial Estate lenye
ukubwa wa hekari 11.
Shirika la Taifa la Maendeleo
(NDC) ni shirika linalomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. lilianzishawa mara
ya kwanza mwaka 1965 kwa tamko la Rais yaani (The Presidential Order Number 5
of 1964) kuchukua majukumu na shughuli za lililokuwa Shirika la Maendeleo la
Tanganyika, yaani, “the Tanganyika Development Corporation.”