MAJADILIANO YA MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA YANAENDELEA

Imeelezwa kuwa, majadiliano baina ya Timu ya Serikali ya Majadiliano (GNT) na muwekezaji wa miradi unganishi ya Liganga na Mchuchuma yanaendelea ili miradi hiyo ianze na kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa.

Hayo yameelezwa na Waziri mwenye dhamana ya Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo wakati akiwasilisha ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, jijini Dodoma. 

Prof. Mkumbo ameelezwa kuwa lengo la miradi hiyo ni kuanzisha Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma, kuanzisha Kituo cha Kufua Umeme cha Megawati 600, kuanzisha Kiwanda cha Kufua Chuma na kuanzisha Mgodi wa Chuma wa cha Liganga. 

Katika kufafanua zaidi, Kaimu Mkurugenzi MWendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Bi. Rhobi Sattima, amesema Mradi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma na Mradi wa Chuma cha Liganga inatekelezwa na kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources Limited (TCIMRL), ambayo ni kampuni ya ubia baina ya NDC (20%) na Schuan Hongda Group Limited (SHG) yenye asilimia 80 ya nchini China.

https://ndc.go.tz/news/miradi-ya-liganga-mchuchuma-mbioni-kuanza-1

Aliendelea kueleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unatokana na maamuzi ya Baraza la Mawaziri kupitia Wakara wa Baraza la Mawaziri Namba 6/96 ya mwaka 1996, Baraza la Mawaziri Namba 14/2007 ya mwaka 2007, Baraza la Mawaziri Namba 14/2010/11 ya mwaka 2011, kwa kutambua miradi hii ni msingi wa viwanda mama kwenye nchi yetu. 

Pia alieleza umuhimu wa miradi hiyo katika kuchangia Pato la Taifa katika kupunguza tatizo la ajira nchini, "miradi hii itakapo anza, italinufaisha taifa kwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 6414, pamoja na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000," ameeleza Rhobi Sattima. Mbali na hilo miradi hii pia itasaidia kupunguza uagizwaji wa bidhaa za chuma kutoka nje ya nchi. Si hivyo tu, Megawati zitakazo zalishwa kwenye miradi hiyo itasaidia kupunguza tatizo la umeme nchini. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dunstan Kitandula, ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kuharakisha zoezi la ulipwaji wa fidia kwa wananchi wanaozunguka miradi hiyo. 

Ikumbukwe, tarehe 26 Juni 2021,  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubua Mkutano wa 12 wa Baraza la Biashara Tanzania, kikao kilicho fanyika jijini Dar es Salaam, Rais Samia alieleza kuwa miradi ya Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma inayomilikiwa na NDC, iliyopo Wilayani Ludewa mkoani Njombe kuwa na tija kwa taifa siku za usoni.

"Kuhusu Mchuchuma na Liganga, nimeshatoa maelekezo. Serikali inaendelea na mazungumzo na wawekezaji kuona tatizo ni nini. Serikali inaweza kujitoa hadi wapi, muwekezaji ajitoe hadi wapi, na kwa sasa duniani chuma kimepanda bei, ni wakati wa kuharakisha mradi ufanye kazi," alieleza Rais Samia.