MIRADI YA LIGANGA, MCHUCHUMA MBIONI KUANZA


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ipo kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji wa Kampuni  baina ya Tanzania na China itakayoitwa Tanzania China International Mineral Resources Limited ambayo itafanya kazi ya kutekeleza Miradi mikubwa ya Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe, Mchuchuma iliyopo Wilayani Ludewa Mkoani Njombe.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geofrey Mwambe alipoungana na Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira kutembelea maeneo ya uwekezaji wa Makaa ya Mawe Mchuchuma Kata ya Nkomang’ombe na Chuma cha Liganga Kata ya Mundindi Wilayani Ludewa.

Mhe. Mwambe amesema serikali ipo kwenye hatua za mwisho za kuhakikisha miradi ya Mchuchuma na Liganga inaanza, hivyo  Serikali inaendelea kukamilisha mazungumzo ya kimkataba na Kampuni ya Schuang Hongda ya China na baada ya kukamilisha Serikali na Mwekezaji watalipa fidia kwa wananchi waliopisha miradi hiyo tayari kwa utekelezaji. “Utaratibu wa kulipa fidia upo tathmini imeshafanyika na mtathmini mkuu ameidhinisha kilicho baki ni kumalizia mazungumzo na huyu Mwekezaji, huu mradi unatekelezwa kati ya Serikali na Kampuni ya Schuang Hongda ya China na tunatengeneza Kampuni mpya itaitwa TANZANIA CHINA INTERNATIONAL MINERAL RESOURCES LIMITED kwa pamoja tutalipa hii fidia” Mhe. Geofrey Mwambe

Nae, Mhe. David Kienzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, Mkoani Iringa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira amesema Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma unatarajiwa kuzalisha tani milioni 428 na megawati 600 za umeme ambazo kati ya hizo Megawati 250 zitatumika kuyeyusha Chuma cha Liganga na megawati 350 zitaingizwa kwenye Umeme wa Gridi ya Taifa kupitia Makambako Mkoani Njombe.

“Sisi Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira tumefika Mchuchuma na Liganga kuona utajiri mkubwa wa Nchi uliopo kwenye miradi hii bahati njema Waziri wa Viwanda yupo hapa tunaenda kuishauri Serikali miradi hii ianze mapema ili kuinua uchumi wa Wananchi na Taifa letu” alisema Mhe. Kienzile. 

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ludewa Mhe. Joseph Kamonga licha ya kupongeza ziara ya Kamati ya Bunge Viwanda, Biashara na Mazingira waliyoifanya katika miradi hiyo amesema anaendelea kuiomba Serikali iwalipe fidia wananchi waliopisha maeneo hayo ili wawe huru kuendesha shughuli zao nje ya maeneo ya miradi.

“Natambua Serikali inatilia mkazo miradi hii ambayo itatoa fursa kubwa kwa Wananchi wa Ludewa na Taifa kwa ujumla ili kuwaweka huru Watu wetu naendelea kuiomba Serikali iwalipe fidia ambayo ni kama bilioni 11, eneo hili libaki kuwa mali ya Serikali na Wananchi wakafanye shughuli zao mahali pengine” alisema Mhe. Kamonga, Mbunge wa Ludewa.

Bi. Rhobi Sattima, Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), amesema kuwa Serikali imeipa kipaumbele Miradi ya Liganga na Mchuchuma hivyo Wananchi waendelee kuwa na uvumilivu wakati Serikali inaendelea kukamilisha mazungumzo na Mwekezaji ili kuleta tija kwa pande zote wakiwemo Wananchi wa Ludewa.

Mhe. Deo Mwanyika, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira amesema, Wabunge wa Mkoa wa Njombe wanaendelea kuishauri Serikali kutekeleza miradi hiyo kwa wakati ili kuleta tija kwa Taifa, huku Wananchi wa Kata za Nkomang’ombe na Mundindi ilipo miradi hiyo wakisema wameacha maeneo yao tangu mwaka 2015 bila kuyafanyia kazi huku wakiiomba Serikali kuwalipa fidia ili wakafanye shuguli zao nje na maeneo hayo.

Miradi ya kimkakati ya Liganga na Mchuchuma iliyopo mkoani Njombe inamilikiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.