MKUMBO AZINDUA BODI YA WAKURUGENZI NDC

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amezindua Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC)
Waziri wa Viwanda na Biashara  Prof. Kitila A. Mkumbo tarehe 08 oktoba 2021 amezindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) aliyoiteua Septemba 20, 2021 huku Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Dkt. Yamungu Kayandabila akiteuliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, 16 Septemba, 2021.

Katika kikao hicho cha uzinduzi wa bodi, Waziri Mkumbo aliwapongeza wajumbe wote kwa uteuzi walioupata na kuwasihi kuchapa kazi kwa ujenzi wa taifa.
"Hongera sana Dkt. Kayandabila kwa heshima ambayo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekupatia kwa kukuteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya NDC na wajumbe wote kwa heshima niliyowapa kwa kuwateua kuwa wajumbe wa Bodi. Hongereni sana." Prof. Kitila Mkumbo.

Aliendelea kueleza kuwa, "Pasipo na mashaka yoyote tunaamini uteuzi wenu utasaidia kwa kiwango kikubwa katika kulisimamia na kuliendesha Shirika la Taifa la Maendeleo NDC katika adhima yake ya kusimamia sekta ya viwanda hapa nchini pamoja na miradi ya kimkakati ya serikali."


Shirika la Taifa la Maendeleo ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa mujibu wa tangazo la Serikali, the National Development Corporation (Establishment) Order, G.N. No. 90 of 1969. Shirika hili limeendelea kuwepo chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma, Sura Na. 257 ya mwaka 2002. Jukumu kubwa la Shirika ni kuendeleza na kutekeleza miradi ya kiuchumi kwa kushirikiana na sekta binafsi. Baadhi ya majukumu ya Shirika ni kama yafuatayo: -

(a)            Kuanzisha, kuendeleza na kusimamia viwanda vya msingi nchini likishirikiana na sekta binafsi na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi.          

(b)            Kuchangia kasi ya mabadiliko ya mfumo wa uzalishaji nchini kwa kuanzisha na kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa mipya, na yenye uhusiano mkubwa na sekta/shughuli asilia za wananchi.

(c)             Kusaidia ushiriki wa wananchi wengi katika shughuli za kiuchumi; hii ikiwa ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa miundombinu na kubuni mifumo ya kisasa inayokubalika kwa uendeshaji wa biashara.

(d)            Kulinda maslahi ya nchi kwa kumiliki hisa katika miradi mikubwa na ya kimataifa, ili hatimaye kutoa fursa kwa wananchi wazawa kuzinunua na kumiliki na hivyo kuendesha uchumi rasmi na biashara za kimataifa;

(e)            Kuishauri Serikali kwenye mambo yanayohusu mendeleo ya viwanda pamoja na sera na mipango mikakati yake.


Wajumbe wa Bodi iliyozinduliwa ni : Bw. Nathaniel M. Nhonge kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Dkt. Abdulrahman S. Mwanga kutoka Tume ya Madini; Bi. Joharia H. Mwenda kutoka Ofisi ya Rais - Ikulu; Dkt. Pendo N. Bigambo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Bw. Edson M. Fidelis kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara; Dkt. Edwin P. Mhede kutoka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART); na Bw. Godfrey S. Ayubu kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi.