Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika
la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt Nicolaus Shombe amewataka wafanyakazi wa shirika
hilo kuhakikisha wanashirikiana katika kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili
kuhakikisha wanafikia ndoto ya shirika ya kuwa shirika bora na la mfano kwa kutekeleza miradi mbalimbali
ya kimkakati ya serikali pamoja na kushirikiana
na sekta binafsi katika kukuza sekta ya viwanda hapa nchini.
Dkt Shombe ameyasema hayo mara
baada ya kuwasili rasmi katika ofisi za Makao Makuu ya NDC na kuanza kazi ambapo
mara baada ya kuwasili alianza kwa kuzungumza na wafanyakazi wote wa shirika
hilo ikiwa ni siku chache tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa, Samia Suluhu Hassan kushika nafasi ya kuliongoza shirika
hilo.
Akiongea na wafanyakazi wa NDC
Dkt Shombe amewataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii na maarifa badala
ya kufanya kazi kwa mazoea pamoja na kutoa ushirikiano ili kuendana na kasi ya
serikali ya Awamu ya sita kupitia kauli mbiu ya Kazi iendelee.
“Ninawaombeni
sana ushirikiano wenu tukiwa kama familia moja, tushirikiane pamoja katika
kuhakikisha Shirika linasonga mbele. Tukishirikiana tutaweza kuzitatua
changamoto mbalimbali zinazotukabili kwa pamoja kutumia fursa tulizonazo
nitahakikisha tunatenge muda maalum ambao tutakuwa tunakutana na
menejimenti,wakuu wa Idara pamoja na wafanyakazi wote ili kusiwe na utofauti
mkubwa baina ya viongozi pamoja na watumishi wa kawaida lengo likiwa ni kujenga
teamwork ” Alisema Dkt Shombe.
Hata hivyo katika kuonyesha
kuwa amedhamiria kubadilisha utendaji kazi wa Taasisi katika kikao hicho Dkt
Shombe aliwataka wafanyakazi kuainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili
katika utendaji wao wa kazi ambapo mara baada ya kupokea changamoto hizo amehaidi
kuzitendea kazi mara moja huku akiwataka wafanyakazi kubainisha fursa
wanazoziona na mikakati ya kuzitumia kwa maendeleo ya viwanda nchini.
Kwa upande wake aliyekuwa
Kaimu Mkurugenzi wa NDC,ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Fedha Rhobi Sattima alimpongeza Dkt Shombe kwa
kuaminiwa na Rais na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC huku akisema
kuwa ana imani ataifanyia makubwa NDC.
“Mkurugenzi
ninakumbuka siku moja wakati uko Hazina kama Kamishina wa Mipango ulitusaidia
sana katika kuhakikisha kuwa taasisi inawezeshwa kifedha na nadhani ulifanyika kuwa
kama malaika kwani hatimaye leo umeteuliwa rasmi kuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa
Shirika Hongera sana kwani tunamatumaini makubwa na ujio wako”Alisema
Bi Rhobi Sattima.
Ujio wa Dkt Shombe kuwa
Mkurugenzi mpya wa NDC umepokelewa vizuri na wafanyakazi ambao wamehaidi kumpa
ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha anatimiza adhima ya shirika hilo ya
kuwa bora na imara hapa nchini litakalokuwa linaongoza katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda pamoja
na kuvutia na kujenga mazingira bora wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya
nchi.
Uteuzi wa Dkt Shombe kushika
nafasi ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC na Rais umefanyika mara baada ya
kufariki Dunia kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa NDC Prof Damiani Gabagambi ambaye
alifariki dunia Mwishoni mwa mwaka jana ambapo kabla ya kuteuliwa na Rais kuwa
mtendaji mkuu wa NDC Dkt Shombe alikuwa anashika nafasi ya Kamishina wa Mipango
ya Kitaifa kwenye Wizara ya Fedha na Mipango.