MPANGO WA NDC KUZALISHA VIUATILIFU NA MBOLEA ZA KIBAIOLOJIA WAIVA

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), kupitia kiwanda chake cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), cha Kibaha - Pwani, kipo mbioni kuzalisha viuatilifu vya kuangamiza wadudu dhurifu kwenye mazao pamoja na mbolea za kibaiolojia.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe wakati wa ziara ya kikazi ya Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne alipotembelea kiwanda cha TBPL, Kibaha.

Dkt. Shombe ameeleza kuwa NDC kupitia kiwanda chake cha TBPL wameshaanza kuzalisha viuatilifu vya majaribio na matokeo ni mazuri hasa katika zao la pamba.  

“Tumeshafanya majaribio na taasisi mbalimbali za tafiti pamoja na Wizara ya Kilimo na matokeo ni mazuri,” ameeleza Dkt. Shombe.

Dkt. Shombe amesema uzalishaji wa viuatilifu na mbolea utaliongezea Taifa kipato kwa kupunguza uagizwaji wa bidhaa hizo nje ya nchi na itasaidia kuongeza mnyororo wa thamani kuanzia uzalishwaji wa bidhaa hizo mpaka kumfikia mtumiaji.

Nae Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne amesema ana imani uzalishaji wa viuatilifu na mbolea utaanza mapema na kuleta tija kwa nchi hasa kwenye sekta ya kilimo.

Balozi Despaigne amesema kuwa wapo tayari kutoa msaada wa kiufundi kwa TBPL ili kuzalisha bidhaa zenye ubora. “Timu yetu ya wataalam imeshafika na kesho tunatarajia kuanza majadiliano na NDC,” ameeleza Balozi Despaigne.