Tumeamua kushirikiana kwa ukaribu ili kuhakikisha tunachimba makaa ya mawe mkoani Njombe.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka wakati wa ziara yake kukutana na menejimenti ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), kufahamu miradi mbalimbali ya NDC na namna anavyoweza kushirikiana na NDC kwa ukaribu ili kuvuta wawekezaji kuwekeza nchini, kikao kilichofanyika makao makuu ya NDC, jijini Dar es Salaam.
Kwenye ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe ameambatana na wawekezaji wazawa, kampuni ya Qwihaya ya mkoani Njombe walio na nia ya kuwekeza kwenye miradi ya NDC.
Alieleza kuwa kwa sasa shughuli ya kuchonga barabara inayopita kwenye mlima Kimelembe wilayani Ludewa inaendelea vizuri ambapo wakandarasi 3 wapo kazini ili kuhakikisha kazi inaisha kwa wakati uliokusudiwa na kufungua milango kwa wawekezaji zaidi kufika kwenye miradi iliyokusudiwa.
Aliendelea kueleza sasa ni wakati wa WanaNjombe kufaidi matunda ya ardhi yao kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za ujenzi wa kilomita nyingine 50 za barabara ya Njombe – Ludewa kwa kiwango cha zege.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthoy Mtaka, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe alimueleza mkuu huyo wa mkoa miradi inayosimamiwa na Shirika ikiwemo kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibaiolojia, Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) cha Kibaha – Pwani, kiwanda cha kuzalisha vipuri vya mashine na mitambo mbalimbali, KMTC cha mkoani Kilimanjaro, maeneo ya uwekezaji yaliyopo Kibaha, Tanga, Kilimanjaro na Mwanza.
Alikazia kuwa kwa mkoa wa Njombe, NDC ina miradi ya chuma pamoja na makaa ya mawe, miradi ya Liganga, Mchuchuma, Maganga Matitu na Ketewaka.
Dkt. Shombe alimueleza Mhe. Anthony Mtaka milango ipo wazi kwa wawekezaji wazawa na wa nje wenye nia ya kuwekeza Tanzania kwani NDC ni mkono wa Serikali kwenye uwekezaji.