MWAMPOSA AKATAA UTUMWA

Mchungaji Boniface Mwamposa "Bulldozer", wa Kanisa la Arise & Shine Ministry, la Kawe jijini Dar es Salaam, amekataa kuwa mtumwa wa mbu kwa kununua lita 103.03 za viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu vyenye thamani ya shilingi 1,179,900/- milioni kutoka kiwanda cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), kilichopo kibaha mkoani Pwani, kiwanda kinachomilikiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).

Mchungaji Mwamposa amefikia uamuzi wa kununua viuadudu baada ya Maafisa kutoka kiwanda cha TBPL kutoa mafunzo kanisani kwake juu ya umuhimu wa kutumia viuadudu, mafunzo yaliyotolewa kwa waumini na kisha kunyunyuzia viuadudu katika bwawa linalo zunguka kanisa lake mnamo Novemba 28, 2020 hali iliyoleta matokeo chanya kwani mbu wamepungua kwa kiasi kikubwa hivyo kumfanya avutiwe na kuamua kuagiza lita 103.03 ambazo zimepelekwa kanisani kwake, Kawe jijini Dar es Salaam.

Licha ya kuwa ni Kiongozi wa Kiroho, Mchungaji Mwamposa wa Kanisa la Arise & Shine Ministry, anaungana na Watanzania wengine pamoja na Serikali kupitia Halmashauri zake katika kununua na kutumia viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu katika mazingira yao kupitia Kampeni ya Kitaifa yenye lengo la kutokomeza kabisa Malaria ifikapo mwaka 2025, kampeni inayoendeshwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambao ni waratibu, kupitia kiwanda chake cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) ambao ndio wazalishaji wa viuadudu na watoa mafunzo, kwa kushirikiana na Asasi isiyo ya Kiserikali ya Kumekucha Tanzania ambao jukumu lao ni kuamsha hamasa ya ununuzi wa dawa, kuongeza mauzo na kutangaza dawa kwa jamii.

Sambamba na hilo, Asasi isiyo ya Kiserikali ya Kumekucha Tanzania wameendelea kutoa elimu kwa wakazi wa Dar es Salaam hasa maeneo ya Mabwepande, Mbweni, Makongo Juu, Tabata pamoja na kutoa elimu kwa watumishi wa Kada ya Afya; Mazingira; Ustawi na Maendeleo ya Jamii na wafanyabiashara takriban 900 kupitia semina na kupitia makongamano yaliyo fanyika Mbagala pamoja na Mkuranga mkoani Pwani.

Hadi kufikia Novemba, 2020, timu ya kampeni ya kutokomeza Malaria imefika katika mikoa 11 ya Tanzania Bara ambayo ni Songwe, Mbeya, Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu, Geita, Morogoro, Ruvuma, Dar es Salaam na Shinyanga, ambapo jumla ya lita 16,285 zenye thamani ya 318,575,326/- milioni zimenunuliwa. huku Mkoa wa Mara na Songwe ikiahidi kuchukua lita 43,210 zingine kwa awamu ya pili zenye thamani ya 569,184,000\- milioni.

Kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu, Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) kilizinduliwa ramsi na Rais wa Awamu ya 4 Mh. Dkt. Jakaya M. Kikwete pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, 2 Julai 2015 Kibaha, Pwani.