NDC kuchochea uzalishaji wa magurudumu ya magari Tanzania

Tanzania inatarajiwa kuzalisha matairi milioni 20 kwa mwaka ifikapo mwaka 2023, hayo yamesemwa leo na Capt. Amri Said wakati wa utiaji sahihi Mkataba wa Upangaji wa eneo la Uwekezaji la KMTC kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kampuni ya Sayinvest Overseas Limited, shughuli iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa NDC, Posta jijini Dar es Salaam.

Utiaji huo wa sahihi umehudhuriwa na Menejimenti ya NDC ikiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji, Prof. Damian Gabagambi Pamoja na wawakilishi wa Sayinvest Overseas Limited wakiongozwa na mmiliki wake Capt. Amri Said.

Kiwanda hicho kinachotarajiwa kuzalisha matairi kati ya milioni 15 hadi 20 kwa mwaka kitafahamika kama General Tyre Tanzania Limited, kikiwa chini ya kampuni ya Kitanzania ya Sayinvest Overseas Limited na kitajengwa kwenye eneo Maalum la Uwekezaji la KMTC linalomilikiwa na NDC, lenye ukubwa wa Hekta 229.13 lililopo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Uanzishwaji wa kiwanda hiki utaambatana na uwekezaji wa teknolojia ya kisasa ambayo itachochea uzalishaji wa magurudumu imara na yenye ubora wa hali ya juu ambayo yataleta ushindani katika soko la dunia.

Shughuli za ujenzi wa kiwanda zinatarajiwa kuanza mwezi mmoja mara baada ya kutia sahihi Mkataba wa Upangaji ambapo NDC ndio mpangishaji wa eneo hilo.

Awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa miundombinu na ufungaji wa mitambo pamoja na vifaa vingine vinavyohusika huku awamu ya pili ikichukua mwaka mmoja kukamilika.

Inatarajiwa kuwa ndani ya miaka 3 kiwanda kitaanza uzalishaji rasmi na kitachochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa Watanzania ambapo itapunguza uagizwaji wa magurudumu ya magari kutoka nje ya nchi hivyo kuchochea biashara za ndani, kwani malighafi itakayotumika kuzalisha magurudumu hayo itatoka hapahapa nchini katika mashamba ya mpira yanayomilikiwa na NDC yaliyopo Tanga na Morogoro.

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ni taasisi inayo chochea na kuongoza Maendeleo ya Viwanda iliyoanzishwa mwaka 1962, ikijulikana kama Shirika la Maendeleo Tanganyika (TDC) kwa Sheria ya Bunge ili kufadhili miradi muhimu ya kimaendeleo na kuchukua nafasi ya Shirika la Kikoloni la Maendeleo (CDC) lililo anzishwa mwaka 1947/1948.