Tunataka ifike mahali tuseme tumepambana
na kuua mbu kwa dawa iliyo tengenezwa na kiwanda kinacho simamiwa na Shirika la
Taifa la Maendeleo (NDC), kwani kinga ni bora kuliko tiba.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa
Mara, Mh. Adam Malima pindi akipokea lita 3,885 za viuadudu vya kuangamiza
mazalia ya mbu vyenye thamani ya shilingi milioni 52 za Kitanzania, kutoka
Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kupitia kiwanda chake cha Tanzania Biotech
Products Limited (TBPL), cha mkoani Pwani, wakati wa hafla fupi ya makabidhiano
iliyofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Alisisitiza kuwa, lengo lao ni kuona
mkoa wa Mara unakua wa mfano katika harakati za kupambana na Malaria, si Mara
tu bali Tanzania kwa ujumla ili ulimwengu mzima uje kujifunza mbinu iliyotumiwa
na Tanzania kupambana na ugonjwa huo.
Alikishukuru kiwanda (TBPL) kwa utayari
wao wa kuwakopesha viuadudu hivyo, lakini mahitaji yao hasa ni lita elfu 20
ambazo ameahidi ndani ya miezi michache wataagiza tena ili kuhakikisha zoezi
hilo linakua endelevu na kuhakikisha mkoa wa Mara unakua mkoa wa mfano ndani na
nje ya mipaka ya Tanzania.
Kwa kutia mkazi alisema kuwa, ana amini njia
ya kutumia viuadudu ina ufanisi mkubwa kuliko njia nyingine kwani nchi zilizo
tokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria walitumia njia hii, hivyo yeye ni muumini
mkubwa wa viuadudu. “Watanzania tutambue, njia hii ina tija kuliko njia
nyingine,” amesema Malima.
Aliendelea kueleza, matumizi ya viuadudu
yanapaswa yatengenezewe mpango wa kitaifa ili Tanzania ipambane ipasavyo na
Malaria kwani kwa mkoa wake huu ni mwaka wa 3 mfululizo wamekua wakipambana
kufanya mkoa wa Mara utambulike kwa mambo mazuri ikiwemo kutokomeza kabisa
Malaria. “Tunataka mkoa wetu utambulike kwa mambo mazuri ikiwemo kutokomeza
Malaria kwa kutumia viuadudu,” amesema Malima.
Kwa kulipa uzito suala hilo alieleza
kuwa watakwenda Wizarani ili waombe kuwekewa bajeti ya viuadudu kwani ana amini
kinga ni bora kuliko tiba na kuwasihi Waratibu wa Malaria kufuata masharti ya
dawa ili kuhakikisha wanafikia lengo la kupambana na ugonjwa huo, “tunataka
kuona Malaria imeshuka misimu yote ya mwaka,” alisisitiza.
Nae Mratibu wa Malaria mkoa wa Mara,
Daktari Damian Masolwa alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa uzalendo wake wa
kuamini matumizi ya viuadudu kuwa ni njia sahihi na ameahidi mkoa wa Mara utakua
mkoa wa mfano katika kutokomeza Malaria. “Nitasimamia hili zoezi kwa ukaribu
zaidi na nina imani tutatokomeza Malaria,” amesema Masolwa.
Aliendelea kueleza kuwa mkoa wake bado
una kiwango kikubwa cha Malaria ila ana amini ujio wa dawa hizo utapunguza
kabisa kiwango cha Malaria.
Kwa kuonesha ufanisi wa viuadudu hivi,
Afisa Mhamasishaji kutoka Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Kumekucha Tanzania,
wanao shirikiana na NDC katika kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya viuadudu,
Charlotte Nziku alieleza kuwa viuadudu hivyo vipo vya aina mbili, vile vinavyo
wekwa kwenye maji machafu (Gliselesf) na kwenye maji masafi (Bactivec) na havina
madhara kwa binadamu na viumbe wengine kwani vinalenga kumuangamiza kiluwiluwi
wa mbu pekee.
Aliendelea kusisitiza kuwa Watanzania
waone fursa katika viuadudu hivi kwani wanaweza kuwa mawakala na kurahisisha
upatikanaji wa viuadudu hivi kwa urahisi kuliko kutegemea kufuata kiwandani.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi
Mwendeshaji wa NDC, Prof. Damian Gabagambi, Mkurugenzi wa Fedha wa NDC, Rhobi
Sattima alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mh. Adam Malima kwa utayari na
uzalendo wake wa kununua viadudu hivyo, pia alimpongeza kwa moyo wake wa kujali
afya za wananchi wake kwa kuamua kuunga mkono juhudi za kutokomeza Malaria.
Akiupongeza mkoa wa Mara kwa jitihada
zake za kupambana na Malaria, Rhobi Sattima alitoa rai kwa mikoa mingine kuunga
juhudi za kupambana na ugonjwa huu. “kiwanda chetu kina uwezo mkubwa wa
kuzalisha dawa,” alieleza.
Alisema, lita 3,885 walizo toa ni mwanzo
tu kwani wataleta nyingine kama Mkuu wa Mkoa alivyo eleza na amesema zoezi hilo
limeshafanyika katika mikoa ya Mbeya, Songwe na Mwanza na mipango yao ni kufika
nchi nzima. “Tutaendelea na zoezi hili kwani uwezo tunao,” alisisitiza Rhobi Sattima.
Inatarajiwa kuwa lita hizo 3,885
zitagawanywa katika Wilaya zote za mkoa wa Mara wenye ukubwa wa Kilomita za
Mraba 21,760, ikiwemo Wilaya ya Bunda, Butiama, Musoma Vijijini, Musoma Mjini,
Rorya, Serengeti na Tarime.
Ikumbukwe kiwanda hiki cha kuzalisha
viuadudu mahususi kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu, Tanzania Biotech
Products Limited (TBPL), kilizinduliwa
ramsi na Rais wa Awamu ya 4 Mh. Dkt. Jakaya M. Kikwete pamoja na Waziri Mkuu wa
Ethiopia Hailemariam Desalegn, 2 Julai 2015 Kibaha, Pwani.