Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Innocent Bashungwa amelitaka Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kuharakisha mchakato wake wa kuanzisha kiwanda cha kuzalisha vifaa tiba kama barakoa na gloves, kinachotarajiwa kujengwa katika Eneo la Viwanda la TAMCO, Kibaha mkoani Pwani.
Ameyasema hayo mapema leo jijini Dar es Salaam wakati wa Kikao cha Wadau kujadili upatikanaji na uzalishaji wa Vifaa Kinga kwa ajili ya kujikinga na COVID -19.
Ameitaka wizara yake pamoja na TMDA kukaa na NDC ili kufanikisha jambo hilo kwa haraka. “Mkae na NDC ili mimi na Waziri Ummy tupate “timeline” tujue kiwanda hicho kitaanza lini uzalishaji,” amesema Bashungwa.
Amewasihi NDC kuzalisha barakoa aina ya N-95 kama alivyoelezwa awali na Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango wa NDC, Esther Mwaigomole.
Nae Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa ugonjwa wa COVID -19 ni janga na fursa kwa wazalishaji. “mtumie hii kama fursa ya kuongeza uzalishaji wa ndani,” amesema Ummy.
Pia amesema kuwa uzalishaji ukiongezeka utaongeza ajira kwa Watanzania na kuongeza mnyororo wa thamani na kupunguza uagizwaji wa bidhaa zisizo na ubora kwani nchi itatumia vyombo vyake vya ndani kupima ubora wa bidhaa.