SERIKALI KUONGEZA MKAZO UZALISHAJI MPIRA


Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa wakulima waliopo maeneo yenye hali ya hewa kama ya Mang’ula Kilombero kulima zao la Mpira ili kukidhi mahitaji ya soko la 99.7% ambalo kwa sasa mauzo ya zao hilo ni 0.03%

Waziri Kijaji ameyasema hayo alipotembelea Shamba la Mpira la Kalunga lililopo Kata ya Mang’ula Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro kuangalia jitihada zinazofanywa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) katika kuendeleza uzalishaji wa zao hilo la Mpira ambalo ni zao la kimkakati linalotumika kutengeneza bidhaa kama matairi, viatu na gloves.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah alieleza kuwa NDC imeweka utaratibu wa kuondoa miti ya zamani iliyopandwa kipindi cha Serikali ya Awamu ya Kwanza mwaka 1978 na imeisha muda wake na kupanda mpya ili kuhakikisha miti hiyo inatoa faida iliyokusudiwa ya mpira, mbao na utunzaji wa mazingira kwa utoaji wa hewa ya ukaa.

Naye, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC Dkt. Nicolaus Shombe amesema NDC imejipanga kupanda miche laki mbili ya mpira na inakamilisha taratibu za kuthibitishwa kuwa mzalishaji na msambazaji wa mbegu za zao la mpira ili kuhamasisha wananchi kulima zao hilo nchini na kukidhi mahitaji makubwa ya soko ndani na nje ya nchi

Vilevile, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Bw. Christopher Wangwe ameahidi kuongeza eneo la shamba la Kalunga kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mlimba na amepanga kila shule kupanda miche 50 na kila mwanafunzi apande mche mmoja nyumbani ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo linalotoa malighafi za viwandani na kuongeza ajira katika halmashauri hiyo.

Naye, Msimamizi wa Shamba Bwana Egata Makanja amesema zao hilo linaweza kustawi katika mazingila yenye mvua kati ya milimita 2000 hadi 2500 na linaweza kupandwa na mazao mengine ya chakula mwanzoni na mtj huanza kuvunwa ukiwa na miaka mitano kwa kipindi cha miaka 30.