
Shirika
la Taifa la Maendeleo (NDC) linatarajia kushirikiana na Taasisi ya Uhandisi na
Usanifu wa Mitambo Tanzania (TEMDO) katika kubuni na kuzalisha mitambo
mbalimbali ya viwanda pamoja na vifaa ikiwemo vifaa tiba.
Haya
yamebainishwa katika ziara maalum yenye lengo la kujifunza pamoja na kuangalia
maeneo ambayo NDC inaweza ikashirikiana na TEMDO iliyofanywa na Menejimenti ya Shirika
la Taifa la Maendeleo (NDC) ya kutembelea makao Makuu ya TEMDO yaliyopo Njiro
jijini Arusha.
Akizungumza
kwa niaba ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo NDC,
Mratibu wa ziara hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Mipango
NDC, Dk Grace Aloyce amesema lengo la ziara hiyo ni kuangalia namna ambavyo NDC
inaweza ikashirikiana na TEMDO katika kuendeleza sekta ya viwanda kwa kuwa
taasisi zote zinahusika moja kwa moja katika maendeleo ya kukuza na kuendeleza sekta
ya viwanda hapa nchini.
‘’Tumeamua
kuja hapa TEMDO hasa kujifunza lakini pia kuja na mikakati ya namna ambavyo NDC
na TEMDO zinaweza zikakaa pamoja na kuainisha maeneo ambayo tunaweza kushirikiana
kiteknolojia pamoja na katika hatua nzima ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali”
alisema Dk Grace.
Dk
Grace pia alitumia fursa hiyo kuifahamisha Menejimenti ya TEMDO juu ya namna
ambavyo wanaweza wakashirikiana na NDC katika kutumia kiwanda cha KMTC Mashine
Tools LTD kinachomilikiwa na NDC kilichoko Moshi mkoani Kilimanjaro katika
kuzalisha vifaa mbalimbali mathalani uzalishaji wa vifaa tiba ikiwa ni moja
kati ya mpango ambao uko mbioni kutekelezwa na TEMDO kwa kuwa kiwanda hicho
kina uwezo na teknolojia ya kuzalisha vifaa hivyo.
Ikiwa
ni adhima ya Serikali ya kukiboresha kiwanda cha KMTC Dk Grace alibainishwa
kuwa Serikali kwa hivi sasa iko katika mchakato wa ujenzi wa tanuru la
kuyeyushia chuma (Foundry) ambapo ujenzi wa mitambo maalum ya kuzuia kutu (Galvanising)
ukiwa tayari umekamilika kwa asilimia 98.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TEMDO Mwandisi
Elisante Mjema akizungumza kwa niaba ya
Mkurugenzi Mkuu wa TEMDO, amesema wamekuwa wakishirikiana na NDC katika maeneo
mbalimbali lakini ziara ya leo itafungua fursa zaidi za nyanja za ushirikiano
baina ya taasisi hizi mbili mathalani katika mahitaji ya TEMDO kutaka kutumia
kiwanda cha KMTC katika uzalishaji wa vifaa mbalimbali ni makubwa mno.
“TEMDO
ina wabunifu,wasanifu na ina uwezo mkubwa wa kubuni vitu mbalimbali vya
kumsaidia Mwananchi ili linapokuja suala la kuzalisha kwa wingi tunashindwa kwa
kuwa hatuna uwezo huo lakini kiwanda kama KMTC kinaweza kuwa ni msaada mkubwa
kwetu hasa pale tuanapofikia katika hatua ya uzalishaji wa wingi wa Bidhaa
(Mass Production)” alisisitiza Mhandisi Elisante.
Katika
ziara hiyo Menejimenti ya Shirika la Taifa la Maendeleo NDC ilipata fursa ya
kuona ubunifu wa teknolojia mbalimbali pamoja na miradi inayotekelezwa na TEMDO
ikiwemo mradi ya uongezaji wa samani ya zao la Muhogo, Mradi wa utengenezaji wa
vifaa tiba pamoja na majokofu ya kuhifadhia miili katika hospitali mbalimbali
hapa nchini.