NDC KUZALISHA VIFAA TIBA

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lipo mbioni kuanzisha kiwanda cha kuzalisha vifaa tiba (barakoa, gloves pamoja na vifaa tiba vingine) katika eneo la viwanda TAMCO, mkoani Kibaha,  ikiwa ni jitihada za Shirika katika kupambana na ugonjwa wa Corona pamoja na kuendeleza sera ya Tanzania ya Viwanda.

Hayo yamesemwa mapema leo na Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango wa NDC, Esther Mwaigomole wakati wa Kikao cha Wadau kujadili upatikanaji na uzalishaji wa Vifaa Kinga kwa ajili ya kujikinga na COVID -19  kilicho ongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Innocent Bashungwa na Waziri wa Afya, Mh. Ummy Mwalimu jijini Dar es Salaam mapema leo.

Nae Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Innocent Bashungwa amewasihi NDC kushirikiana na Wizara yake (Wizara ya Viwanda) na TMDA ili wapate mrejesho wa haraka juu ya maendeleo ya kiwanda hicho.

“Mkae na NDC ili mimi na Waziri Ummy tupate timeline tujue kiwanda hicho kitaanza kuzalisha lini barakoa na N -95 pamoja na gloves zinaanza kuzalishwa hapa nchini,” amesema bashungwa.

Nae Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa ugonjwa huu ni janga na fursa kwa wazalishaji. “mtumie hii kama fursa ya kuongeza uzalishaji wa ndani,” amesema. Pia amesema kuwa uzalishaji ukiongezeka utaongeza ajira kwa Watanzania na kuongeza mnyororo wa thamani.