
Mnamo
Julai Mosi 2020, Benki ya Dunia ilichapisha ripoti iliyo onesha kuwa Tanzania
imeingia katika nchi ya Uchumi wa Kipato
cha Kati, hiyo ilikuwa ni hatua kubwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya Uongozi wa Rais, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli na kwa taifa kwani
ilivuka malengo iliyojiwekea ya kufika Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025.
Miongoni mwa sababu zilizopelekea Tanzania kuingia
katika nchi ya Uchumi wa Kipato cha Kati inatajwa kuwa ni utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati
iliyobuni ajira kwa Watanzania wengi.
kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, (2025)
ukurasa wa 2, kipengele (1.2) inasema ”Uchumi wa
kipato cha kati umehusishwa na kuwa na nchi ambayo umaskini unapungua, uchumi imara unaojengwa na kuimarika
kwa uzalishaji viwandani unaimarika na wananchi wanapata maendeleo.”
Ili kuhakikisha taifa linaendelea kukuza uchumi
wake na kufikia malengo makubwa zaidi, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limeona
ni busara kuwanoa wafanyakazi wake katika Nyanja ya Uwekezaji hasa katika sheria
ya Uanzishwaji
na Usimamizi wa Miradi kwa Njia ya Ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (Public
Private Partnership) ili kuendana na
kasi ya Serikali katika kuhimiza uwekezaji na ukuaji wa pato la taifa na la mtu
mmoja mmoja kwani NDC ni miongoni mwa taasisi zinazo tekeleza miradi ya
kimkakati inayobuni ajira kwa watanzania wengi wa vipato tofauti tofauti.
Kwa siku mbili mfululizo kuanzia tarehe
22.07.2020 hadi 23.07.2020, wakufunzi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango
wakiongiozwa na Dr. John Mboya wameendesha Semina Elekezi kwa baadhi ya
wafanyakazi wa NDC wakiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika, Prof.
Damian Gabagambi, ili kuwajengea uwezo utakaowasaidia kulinufaisha taifa kupitia
rasilimali zake.
Semina hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa
Mikutano wa NDC, jijini Dar es Salaam ilihusu Masuala ya
Uanzishwaji na Usimamizi wa Miradi kwa Njia ya Ubia baina ya Serikali na Sekta
Binafsi (Public Private Partnership) na ilijikita hasa katika Sheria ya Ubia baina
ya Serikali na Sekta Binafsi (Public Private Partnership Act) ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka
2017.
NDC ikiwa ni mkono wa Serikali katika uwekezaji,
ina miradi kadha wa kadha katika sekta mbalimbali kama; kilimo, Afya, Madini,
na Nishati, hivyo mafunzo haya yalilenga kuwawezesha wafanyakazi kuelewa sheria
na miongozo ya ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi.
Kulingana na kifungu cha 4 (5) cha Sheria ya Uanzishwaji
na Usimamizi wa Miradi kwa Njia ya Ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (Public
Private Partnership) ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho 2017 ina ainisha sekta
kadha wa kadha zinazo angukia katika Ubia baina ya Serikali na Sekta binafsi
kama; Kilimo, Miundombinu, Viwanda, Madini, Afya, elimu, Mazingira, Biashara na
Uwekezaji, hivyo Shirika halikuwa na budi kuwawezesha wafanyakazi wake
kuelewa namna ya kutengeneza mazingira bora ya uwekezaji kwa kuvutia uwekezaji,
kukabiliana na changamoto mbalimbali na jinsi ya kuzitatua ili kusaidia taifa
kunufaika na rasilimali zake.
Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ni taasisi
inayo chochea na kuongoza Maendeleo ya Viwanda iliyoanzishwa mwaka 1962,
ikijulikana kama Shirika la Maendeleo Tanganyika (TDC) kwa Sheria ya Bunge ili
kufadhili miradi muhimu ya kimaendeleo na kuchukua nafasi ya Shirika la
Kikoloni la Maendeleo (CDC) lililo anzishwa mwaka 1947/1948.