NDC QUEENS MOTO WA KUOTEA MBALI MPIRA WA PETE, WAKABIDHI KOMBE LA USHINDI

Timu ya Mpira wa Pete ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), “NDC Queens,” leo, tarehe 21.02.2022 imekabidhi kombe la ushindi kwa Mkurugenzi Mwendeshaji, Dkt. Nicolaus Shombe, baada ya kuibuka mshindi wa pili kwenye bonanza la michezo la Ocean City Corporate Sports Day lililofanyika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tarehe 20.02.2022.  

Shughuli ya kukabidhi kombe hilo imefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa NDC, Posta jijini Dar es Salaam, hafla iliyo hudhuriwa na Menejimenti ya NDC pamoja na Timu ya Mpira wa Pete ya NDC.

Wakiongozwa na Kepteni wa kikosi hicho, Mhandisi. Rebecca Masalu, timu hiyo imekabidhi kombe na kuahidi kuendelea kufanya makubwa zaidi. “Tunashukuru na tuna ahidi ushindi kila tutakapo cheza,” Mha. Rebecca Masalu.

Nae Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe amewapongeza wachezaji pamoja na benchi la ufundi kwa ushindi walioupata

“Hii iwe chachu ya kuleta makombe mengi zaidi,” ameeleza Dkt. Shombe, Mkurugenzi Mwendeshaji, NDC.

Dkt Shombe pia alisisitiza kuwa, michezo ni sehemu ya kujenga afya na utimamu wa mwili hivyo wajitume zaidi kwani afya inapokuwa nzuri ufanisi wa kazi uongezeka na kuchochea ujenzi wa Shirika na Taifa kwa ujumla.  

Bonanza hilo lilihusisha taasisi mbalimbali kama TRA, Tanroads, K4 Security, Jan Group, Hasa, Caspian na taasisi nyingine nyingi, ambapo mfanyakazi wa NDC, Paula Kassange aliibuka mchezaji bora wa Mpira wa Pete kwa wanawake.

Akielezea uchezaji wa Paula Kassange kwa wahudhuriaji wa hafla ya kukabidhi kombe, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa NDC, Said Tunda alisifia uchezaji wa Paula akielezea uwezo wake wa kufunga magoli bila kuangalia “No look scoring,” likiwa ni jambo la nadra kutokea kwenye mchezo wa mpira wa pete.