Sisi ni sehemu ya maendeleo ya jamii inayotuzunguka.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Viwanda vya Kuongeza Thamani wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Bw. Alfred Mapunda wakati wa kutoa msaada wa bidhaa za misitu kwa Shule ya Sekondari Mwanalugali ya Kibaha - Pwani kwa ajili ya kutengeneza samani za shule hiyo hasa madawati kwa ajili ya wanafunzi.
Bw. Mapunda aliendelea kueleza kuwa NDC imekua na desturi ya kurudisha kwa jamii kile inachokipata na kugusa maisha ya wananchi wa kada zote. "Mwezi 1 uliopita tuliwasaidia wakazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam kutokomeza mazalia ya mbu, leo tumeamua kuwapa motisha watoto wetu wapate mahali pazuri pa kujifunzia."
Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwanalugali, Marin Mariwa aliishukuru NDC kwa msaada huo na kuiomba pale watakapo bisha hodi wasichoke kuwafungulia mlango.
Alikazia kuwa shule yake inauhaba wa viti 160 na meza 190 hivyo wanaenda kupunguza changamoto iliyopo. Akizungumza kwa niaba ya walimu wengine, Mwl. Fatia Mwadini alieleza ukosefu wa madawati ulichangia utoro wa wanafunzi na kushusha taaluma shuleni kwao.
Fatia aliongeza kwa kusema msaada walioupata utawapa motisha wanafunzi watoro kurejea darasani. Kwa niaba ya wanafunzi ya Shule ya Sekondari Mwanalugali Felix Ernest aliishukuru NDC kwa msaada walioutoa kwani utaongeza ufanisi kwenye taaluma yao.
Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), limeendelea kuendelea Mpango wa Taifa wa Maendeleo pamoja na Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa kwa kuhakikisha inasaidia jamii kujikwamua kwa kupata elimu bora.