NI MAPAMBANO YA ARDHINI NA ANGANI

Malaria lazima itokomee
Katika kuhakikisha malaria inatokomea kabisa Tanzania, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kiwanda chake cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), kinacho zalisha viuadudu vya kuangamiza viluwiluwi vya mbu wameendesha semina ya mafunzo kwa wakazi wa Mbwate, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani. 

Semina hiyo ya mafunzo ilikua na lengo la kuwafundisha wakazi wa Mbwate namna ya kutambua mazalia ya mbu na jinsi ya kutokomeza kabisa mbu kwa kuangamiza kikazi chake kwa kutumia viuadudu, semina iliyo endeshwa na maafisa kutoka NDC na TBPL, Mudathir Mungia na John Tusiwe. "Lengo la semina hii ni kutambua mazalia ya mbu na jinsi ya kumtokomeza kabisa," alieleza Mungia. 

Katika hatua hiyo, Mungia alieleza kuwa, kwa wastani mbu jike ambaye ndio chanzo cha malaria hutaga mpaka mayai 2000 kwa kipindi cha uhai wake wa siku 21 mpaka 30, hivyo tunapaswa kutumia viuadudu kutokomeza kabisa uzao wake. Kuongezea katika hilo, mtaalam kutoka kiwanda cha TBPL, John Tusiwe alieleza kuwa matumizi ya viuadudu hayana athari zozote kwa mazingira wala viumbe wengine, "ni salama na havina madhara," alieleza Tusiwe. 

Katika kujibu maswali ya wananchi waliotaka kufahamu matumizi ya dawa hizo, Tusiwe aliwaeleza kuwa, dawa hizo hutumika sehemu ambazo maji yanatuama au sehemu ambazo maji yanahifadhiwa yawe maji machafu au maji masafi. "Hata kwenye ile ndoo yako ya maji nyumbani, mbu anaweza kutaga mayai," alieleza Tusiwe. 

Juma Hassan, Mwenyekiti wa Mtaa huo aliwashukuru wakazi wa eneo lake kwa mwamko waliouonesha wa kujitokeza na kujifunza namna ya kuangamiza mazalia ya mbu katika makazi yao. Alieleza kuwa, fursa ya elimu waliyoipata haikutokea kimiujiza bali ni jitihada zilizofanywa na NDC pamoja na TBPL ya kuamua kuacha viyoyozi na kuja kwa wananchi. "Wameacha viyoyozi na kuamua kuja kutokomeza malaria pamoja na sisi," alieleza Juma Hassan, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbwate. 

Baada ya kikao hicho, mwenyekiti huyo wa mtaa aliwaalika warudi tena na safari hii warudi na kasi ya '4G' akiwa na maana waje rasmi kwenda maeneo yenye mazalia ya mbu ili wayatokomeze pamoja. 

Lengo la NDC kupitia kiwanda chake cha kuzalisha viuadudu, TBPL ni kuhakikisha malaria inabaki kuwa historia Tanzania na barani Afrika.