
Katibu Mkuu Wizara ya
Uwekezaji Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah ameonesha kuridhishwa na
hatua inayofanywa na Shirika la Taifa la Maendeleo, (NDC), katika kuendeleza na
kukuza kilimo cha zao la mpira hapa nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya
Uwekezaji Viwanda na Biashara ameyasema haya katika muendelezo wa ziara
zake mara baada ya kufanya ziara maalum ya kutembelea na kujionea shughuli
mbalimbali zinazofanywa katika Shamba la Serikali la Mpira lililiko wilayani
Muheza, Mkoani Tanga ambalo linalosimamiwa na kuendeshwa na NDC.
Dkt. Abdallah amesema
ameridhishwa na mikakati mbalimbali inayofanywa na NDC kukuza uzalishaji wa zao
hilo hapa nchini ikiwemo uandaaji wa miche kwa ajili ya kuendeleza zao hilo
ambapo akiwa shambani hapo alipokea taarifa kuwa tayari kiasi cha miche ya
mpira 1,500 imeshaandaliwa ili kupandwa ikiwa ni hatua inayofanywa na NDC
katika kuhakikisha inaendeleza upandaji na uboreshaji wa shamba hilo hapa
nchini.
"Nimefurahishwa
na hatua mnazofanya za kuongeza miche kwa ajili ya kupanda miti mipya ambapo
nilipotembelea Kalunga niliona kiasi cha miche laki moja na kumi elfu
imeshaandaliwa tayari kwa kupandwa na hapa leo nimeambiwa mna miche 1,500 ni
hatua nzuri katika kuboresha na kuongeza ukubwa wa mashamba yetu.”
Awali Mkurugenzi
Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe akimkaribisha Katibu Mkuu alizungumzia
juu ya mikakati mbalimbali inayofanywa na NDC kuboresha shamba hilo
ikiwemo kuongeza kasi ya upandaji wa miche.
Dkt. Shombe alitoa
taarifa ya uvamizi ambao umekuwa ukifanywa na wananchi ambao kwa hivi sasa
wamevamia sehemu ya shamba hilo kwa kufanya shughuli za kibinadamu ikiwemo
shughuli za kilimo pamoja na makazi.
Kuhusiana na suala la
uvamizi wa shamba hilo Dkt. Abdallah akiongea na Uongozi wa kijiji cha Kwaisaka
kilichoko kata ya Tongwe wilayani Muheza ambapo shamba hilo lipo Dkt. Abdallah
aliutaka Uongozi wa kijiji kupitia kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho hicho, Hamis
Rajabu Hussein kuhakikisha wanawaelimisha wananchi kuacha tabia ya kuvamia
maeneo ya Serikali yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli maalum na kuamua
kuendesha shughuli zao za maisha ikiwemo kilimo pamoja na makazi kwa kuwa
kufanya hivyo ni kinyume na sheria na taratibu nchi.
Dkt. Abdallah pia
ametaka kufanyika kwa uhakiki wa mipaka ya kuzunguka shamba hilo hali
itakayopelekea mipaka yake kujulikana na hivyo kuepusha changamoto ya wananchi
kuingia eneo hilo na kuendesha shughuli zao za kilimo pamoja na makazi.
Kwa upande wa
Mwenyekiti wa kijiji cha Kwaisaka, Hamis Rajabu Hussein amekiri kuna tabia ya
wananchi kuvamia eneo hilo na kwamba amepokea maelekezo ya Katibu Mkuu na
atakuwa anawaelimisha wananchi wa kijiji hicho kuacha kuvamia na kuanzisha
shuguli za kilimo na makazi katika eneo hilo kwa kuwa ni eneo maalumu
lililotengwa na Serikali kwa ajili ya uzalishaji wa zao la mpira na lazima lilindwe
kwa manufaa ya kizazi cha leo na cha kesho.
"Kuhusu suala la
uvamini tutakuwa tuna wapa wannchi elimu na kuhakikisha hawavamii maeneo ya
umma yaliyotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.”
Kaimu
Mkurugenzi wa Viwanda vya Kuongeza Thamani NDC, Esther Mwaigomole (mwenye
tshirt ya kijani), akimuonesha Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na
Biashara Dkt. Hashil Abdallah namna utomvu unavyogemwa katika shamba la mpira
Kihuhwi.
Ziara ya Katibu mkuu
wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ni muendelezo wa ziara ambazo
anazifanya katika kutembelea miradi mbalimbali ya Serikali ambapo mapema wiki
iliyopita wakiwa pamoja na Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu
Kijaji walipata fursa ya kutembelea shamba la mpira la Kalunga lililoko
Kilombero mkoani Morogoro ambalo pia linamilikiwa na NDC.