
Shirika la
Taifa la Maendeleo (NDC) linaungana na Familia ya Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Watanzania wote katika Kumbukizi ya miaka 21 tokea kifo
chake kilichotokea tarehe 14 Oktoba, 1999.
Uanzishwaji
wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) uliasisiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere mwaka 1965 kwa tamko la Rais (The Presidential
Order Number 5 of 1964) ambapo lilipewa majukumu na shughuli zilizokuwa zinafanywa
na Shirika la Maendeleo la Tanganyika (TDC), ambayo yalikuwa ni kuanzisha na
kuendeleza Viwanda Mama na Viwanda vya Kuongeza Thamani kwa kushirikiana na
taasisi binafsi.
Serikali
ilianzisha NDC ili kuwa na chombo cha Umma kitakacho buni, kuendeleza na
kusimamia utekelezaji wa miradi ambayo inatoa mchango mkubwa katika maendeleo
ya Taifa. Katika uanzishwaji wake NDC ndiyo iliyoanzisha viwanda vyote
vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali. NDC ilikuwa Shirika Hodhi (holding
corporation) la Serikali kwa makampuni na taasisi mbalimbali. Hii iliendana
na mfumo wa kiuchumi wa wakati huo uliotokana na Mlengo wa Ujamaa na Kujitegemea
ambapo Serikali ilimiliki njia kuu za kiuchumi, sera hii ilitokana na Azimio la
Arusha la 1967.
Tokea
uanzishwaji wake Shirika limeendelea kutekeleza miradi mbalimbali iliyoasisiwa
na Baba wa Taifa na limeanzisha miradi mipya kulingana na majukumu yake. Miradi hiyo inagusa Sekta zote muhimu kama Kilimo, Madini,
Afya, Viwanda, Nishati, Miundombinu na Biashara. Baadhi ya miradi hiyo ni;
Migodi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma, Ngaka na Kataweka; Chuma cha Liganga,
viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi. Vilevile, Shirika linasimamia Bandari Kavu ya
Nafaka - ETC Cargo, Dar es Salaam na Mashamba ya Mpira yaliyopo Morogoro na
Tanga.
Aidha,
Shirika linamiliki Maeneo ya Uwekezaji (Industrial Parks) ambayo ni; -
TAMCO-Kibaha; Kange -Tanga; KMTC-Kilimanjaro na Nyanza-Mwanza. Baadhi ya maelezo
ya miradi inayotekelezwa ni kama ifuatavyio:-
- KIWANDA CHA KUUNGANISHA MATREKTA AINA YA
URSUS
Kiwanda
hiki kipo Kibaha, Pwani na ni matokeo ya Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi
baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Poland. Mradi
ulizinduliwa rasmi tarehe 21 Juni, 2017 na Rais, Mhe. Dkt. John P. Magufuli
ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 ibara ya 85. Matrekta
hayo yanauzwa kwa pesa tasilimu na kwa mkopo usiokuwa na riba wala dhamana
hivyo umesaidia wananchi hasa wa kipato cha chini kumiliki matrekta na kuongeza
uzalishaji. Lengo la NDC na Serikali ni “kulipeleka jembe la mkono Makumbusho.
Matrekta haya pamoja na vifaa vyake bado yapo na yanauzwa
kwa bei nafuu.
2. KIWANDA
CHA KUZALISHA VIUADUDU VYA KUANGAMIZA MAZALIA YA MBU - TANZANIA BIOTECH
PRODUCTS LTD (TBPL)
Kiwanda
hiki kipo Kibaha, Pwani na ni cha kipekee, kwani kipo kimoja barani Afrika kikiwa
kiinamilikiwa na Serikali kwa 100% chini ya NDC, huku kikizalisha Viuadudu vya
kuua viluwiluwi vya mbu waenezao Malaria na magonjwa mengine Dengue, Zika,
Chikungunya, Matende na Mabusha. Katika ziara yake kwenye kiwanda hicho, tarehe
22 Juni, 2017 Mhe. Rais Dkt. John P. Magufuli aliagiza, Halmashauri zote nchini
zinunue dawa hizo ili kuweza kutokomeza kabisa Malaria. Kufuatia tamko hilo NDC
kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Kumekucha na wadau wengine
inaendesha kampeni ya kuhamasisha matumizi ya viuadudu nchini. Dawa
zinapatikana kwa bei nafuu
3. KIWANDA
CHA KUZALISHA VIPURI KMTC
Kiwanda
hiki kipo Moshi, Kilimanjaro na kilijengwa mwaka 1984. NDC chini ya Serikali ya
Awamu ya 5, imefufua kiwanda hiki na sasa kinazalisha mashine mbalimbali zikiwemo;
mashine za kusaga, kukoboa, kuranda mbao, vipuri vya matrekta, kubuni na kuunda
matela ya matrekta ya tani 5 kwa ajili ya kuwarahisishia usari wakulima.
4. MASHAMBA
YA MPIRA
Shirika
limeendeleza mashamba ya mpira yaliyopo Kihuwi (Tanga) na Kalunga (Morogoro) na
uzalishaji umeongezeka kutoka tani 10 kwa mwezi mwaka 2015 hadi tani 30 kwa
mwezi mwaka 2020, hivyo kupunguza uagizwaji wa malighafi hiyo nje ya nchi.
Mashamba haya yameajiri zaidi ya Watanzania zaidi ya 278.
5. MRADI WA
MAKAA YA MAWE NGAKA
Mradi upo
katika eneo la Ngaka, Mbinga, Mkoani Ruvuma na unatekelezwa na kampuni ya TANCOAL
Energy Limited ambayo ni ubia kati ya NDC na Intra Energy (Tanzania) Limited
(IETL) kampuni tanzu ya Intra Enegy Limited ya Australia. Mradi huu umechochea
ukuaji wa viwanda nchini kwa kuhakikisha upatikanaji wa makaa ya mawe ambayo ni
chanzo cha nishati inayotumika kwenye viwanda vya saruji na viwanda vinavyo zalisha
bidhaa mbalimbali ndani na nje ya nchi kama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Zambia.
6. MRADI WA
MAGADI-SODA
Mradi huu
uko eneo la Engaruka, Monduli, Arusha na umelenga kuzalisha Magadi Soda ambayo yatatumika
kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo rangi za nguo, vioo vinavyotumika kwenye
magari na ujenzi. Mradi huu ukikamilika utaliingizia Taifa mapato
na utaokoa
fedha zinazopotea kuagiza malighafi kutoka nje ya nchi.
7. MRADI WA
ENEO LA VIWANDA TAMCO, KIBAHA
Katika eneo
hili ukiacha kiwanda cha matrekta cha URSUS na cha Viuadudu (TPBL) ambavyo vimeelezwa
mwanzoni mwa makala hii, kuna viwanda ambavyo vimejengwa katika eneo hilo na
ujenzi wa vingine unaendelea. Baadhi ya viwanda katika eneo hilo ni;
(i)
HESTER BIOSCIENCE AFRICA
Kiwanda
hiki kipo katika hatua za mwisho za ujenzi, huku kikitarajiwa kuzalisha chanjo za
wanyama (Animal Vaccines) na kupunguza gharama za uagizaji wa chanjo
hizo nje ya nchi. Vilevile Kiwanda kitazalisha ajira za moja kwa moja zipatazo
200 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 1,000.
(ii)
KIWANDA CHA GF TRUCKS VEHICLE
ASSEMBLERS
Kiwanda
hiki kimekamilika na kimeanza kuunganisha magari aina ya FAW Trucks na mitambo
yake. Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha magari 1,000 kwa mwaka na kimetoa ajira
za moja kwa moja 150 kwenye awamu ya kwanza ya utekelezaji. kiwanda hiki kitatatua
changamoto iliyopo ya kuagiza magari na mitambo mbalimbali nje ya nchi.
(iii)
KIWANDA CHA VIFUNGASHIO - GLOBAL
PACKAGING TANZANIA LIMITED (GPTL)
Kiwanda cha
vifungashio Global Packaging (T) Limited, Kilizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzani Mhe. Dkt. John P. Magufuli mwezi Juni, 2017. Kiwanda hiki
kinazalisha vifungashio vyenye ujazo tofauti tofauti ambavyo vinauzwa ndani na
nje ya nchi, huku kikiwa kimetatua changamoto ya kuagiza vifungashio nje ya
nchi na kimetengeneza ajira takribani 120,000.
8. ATAMIZI
YA VIJANA WABUNIFU
Shirika
linafanya atamizi ya vijana wenye mawazo bunifu katika Sekta ya Viwanda, lengo
ni kuwajengea uwezo wawekezaji wa ndani ili wanufaike na rasilimali za nchi kwa
kuwekeza kwenye viwanda vya kimkakati vya kitaifa. Kwa sasa Shirika limefanya
atamizi ya vijana wabunifu kutoka kampuni ya EDOSAMA ambapo kwa kushirikiana na
NDC wamefanikisha uanzishwaji wa kampuni ya Green Gold Treasury Limited ambayo
inajihusisha na uongezaji wa thamani ya mazao ya misitu.
Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linakumbuka mchango wa Baba wa
Taifa katika ujenzi wa Taifa, Daima utabaki
ndani ya mioyo yetu.