
Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila
Mkumbo (Mb) ametoa maelekezo kwa ajili
ya kuimarisha sekta ya viwanda na biashara ili sekta hizo zichangie kwa
kiwango kikubwa katika ukuaji wa uchumi na kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa
Taifa wa Maendeleo wa III wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26, Ilani ya CCM ya uchaguzi 2020 na Maelekezo ya
Serikali ya Awamu ya Sita na Ushauri na
maoni maelekezo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza
uchumi wa Viwanda nchini.
Profesa Mkumbo ametoa maelekezo hayo
alipokutana na menejimenti ya wizara na wakuu wa taasisi zilizochini ya
wizara hiyo kwa lengo la kutoa mwelekeo
wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika kikao kilichofanyika tarehe 10/04/2021 katika ukumbi wa Chuo cha
Biashara jijini Dodoma.
Akiongea katika kikao hicho, Waziri alisema Dira
ya Maendeleo ya Mwaka 2025 inalenga kuona Tanzania inahitimu na kuondokana kuwa
nchi masikini inayotegemea kilimo na uchumi wa uzalishaji duni na kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ambapo wananchi wengi wajihusihe na kilimo cha
kisasa kinachofunganishwa na viwanda na huduma. Hivyo alisisitiza kuwa
ili kufikia dira hii wizara hiyo ina nafasi na mchango mkubwa katika kufanikisha azma hiyo.
“ Uchambuzi wa maudhui ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa III wa miaka
mitano 2021/22 – 2025/26 unaonesha wazi kabisa nafasi ya Sekta ya Viwanda na
Biashara…sisi kama Wizara tunatarajiwa kutoa mchango karibu kwa kila eneo la
matokeo tarajiwa.”
Alisema pia katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa III wa miaka mitano 2021/22
– 2025/26, malengo sita kati ya malengo mahsusi 12 yanahusu sekta ya viwanda na
biashara, kati ya vipaumbele vitano vya mpango huo vitatu vinahusu wizara
hiyo, katika Sekta 30 za mpango huo
Sekta 6 zinahusu Wizara na katika hatua
156 hatua 54 zinahusu
Wizara ya Viwanda na Biashara.
“Taasisi zote zilizochini ya Wizara ya Viwanda
zinamchango mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ili kufikia malengo
ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa taifa wa Maendeleo wa III wa
miaka mitano 2021/22 – 2025/26, malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020,
Maelekezo ya Serikali awamu ya sita. Hivyo nawasihi muendelee kufanya kazi kwa
mujibu wa Sheria Kanuni na taratibu zinazosimamia taasisi zenu katika utoaji wa
huduma bora kwa wananchi na si kuwa kikwazo”
Hata hivyo, Profesa Mkumbo alisema hakusudii
kutumia muda mwingi katika kutunga Sera, Sheria na mikakati na kuwa yeye
analenga katika utekelezaji na kuona matokeo ya utekelezaji huo kwa kuchochea
ukuaji wa haraka wa Sekta ya Viwanda na Biashara.
Pia aliwataka wataalamu wa Idara ya Sera na Mipango ya Wizara kusimamia
uhuishaji wa nyaraka mbalimbali za kisera na sheria ili ziende na wakati na kuakisi maudhui ya
Mpango wa tatu wa Maendeleo na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Akitoa maelekezo mahususi kwa upande wa sekta ya viwanda, Profesa Mkumbo
alitaka kuwa bayana na dhana na aina ya viwanda tunavyotaka kuviendeleza hapa
nchini, kuwa na kanzi data ya kisasa ya viwanda. Pia alielekeza katika kupima
maendeleo ya viwanda kwa kuzingatia kiwango cha uzalishaji na ajira, kuweka mazingira
namasharti rahisi katika kukuza na kuchochea viwanda vidogo vidogo vinavyotumia
teknolojia rahisi na ya kisasa na vilivyojikita vijijini na mijini,
Profesa Mkumbo pia alisisitiza mkazo katika kuwatambua, kuwawezesha na
kuwahudumia wawekezaji katika viwanda vikubwa na vyenye tija katika uchumi na
kuhuisha Mkakati wa Viwanda nchini, ikiwemo dhana ya EPZ na SEZ. Alisema
pia kusimamia kwa karibu miradi ya kielelezo iliyopo katika Mpango wa Maendeleo
wa Tatu wa Taifa ambayo ni mradi wa Chuma wa Mchuchuma na Liganga, Magadi Soda
wa Engaruka, ujenzi wa Kiwanda cha Sukari-Mkulazi na kanda Maalum za Uchumi na
Maeneo Maalum ya Uwekezaji
Profesa Mkumbo alisema pia kuimarisha utafiti na matumizi yake katika maendeleo
ya viwanda, ikiwemo kuwa na ushirikiano wa karibu na taasisi za utafiti na
elimu ya juu na kupanua na kuboresha mahusiano na ushirikiano na taasisi za
sekta binafsi.
“ Pia kuimarisha ushirikiano na OR-TAMISEMI katika maendeleo ya viwanda vidogo
vidogo, tunataka kuona uwezekano wa kuwaongeza majukumu maafisa biashara wa
Halmashauri ili pia wasimamie viwanda vidogo vidogo katika maeneo yao kwa
kushirikiana na SIDO.”
Kwa upande wa sekta ya biashara, Profesa Mkumbo aliweka msisitiza katika suala
la kujenga imani kwa wafanyabiashara kupitia, uwazi na mawasiliano chanya ya
mara kwa mara. “Tunataka tunapokutana na wafanyabiashara tufanye mazungumzo
yenye tija ya kubadilisha mikakati ya kukuza biashara na masoko, badala
mikutano hiyo kutumika tu kama jukwaa la kusikiliza malalamiko ya
wafanyabiashara.”
Alisema pia kuendelea kuzipitia kanuni za mamlaka za udhibiti zinazoonekana
kukwamisha biashara, kuchochea na kuhamasisha tabia ya kujali wateja miongoni
mwa watendaji wa Serikali wanaohudumia sekta mbalimbali za biashara.
Profesa Mkumbo alisema pia kuipitia na kufanya tathimini ya utekelezaji wa “Blue
Print” kwa lengo la kuona maeneo ambayo bado hayajatekelezwa na kusimamia
utekelezaji wake kikamilifu na kwa haraka, kushirikiana na OR-TAMISEMI,
kuchambua na kuchakata kwa umakini maoni ya wabunge na wadau wengine kuhusu
haja ya kuwa na Mfuko mmoja wa Mtaji kwa ajili ya wajasiriamali na wafanya
biashara wadogo.
Alisema pia kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa sera ya maendeleo ya sekta
binafsi, ikiwemo biashara ndogo zinahitaji upendeleo maalumu ili kukua na
kuweka msisitizo wa pekee katika kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania ndani ya
nchi na nje ya nchi na kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa maeneo maalum ya
kibiashara hususani kwa maeneo ya mipakani. Pia, kuona namna ya kuimarisha eneo
maalumu la kibiashara la Kariakoo ambalo kihistoria limekuwa likifanya vizuri
na kuwalinda walaji.
Aidha, Profesa Mkumbo amesisitiza haja ya watendaji wa wizara na wataasisi
kubadilisha mtizamo katika utendaji kazi na kuwa na “corporate thinking” na
tabia ya kujali wateja kwa kuzingatia kuwa wadau tunaowahudumia ni wafanyabiashara.
Pia amewalekeleza wataalamu
wa wizara hiyo kuhakikisha wanatoa ushauri wa kitaalamu wenye ushahidi wa
kisayansi na ameahidi atatoa ushirikiano mkubwa kwa wafanyabiashara
Aidha,
Profesa Mkubwa alisikiliza maoni na changamoto mbalimbali zinazozikabili
taasisi hizo kutoka kwa Wakuu wa Taasisi kutoka TBS, WMA, BRELA, TANTRADE,
SIDO, NDC, EPZA, FCC, FCT, WRRB, TIRDO, CAMARTEC, TEMDO na CBE na kuahidi
kuzitatua.