Nimefurahi
kutembelea eneo hili muhimu la Mtaa wa Viwanda la TAMCO, ambapo ni eneo muhimu
katika ujenzi wa viwanda.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo baada wakati wa
ziara ya kutembelea Kongane ya Viwanda ya TAMCO, Kibaha mkoani Pwani inayo
milikiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Ameeleza
kuwa eneo hilo la uwekezaji la TAMCO limegawanyika kwenye maeneno makubwa
matatu; eneo la ujenzi wa viwanda vya magari, ujenzi wa viwanda vya madawa na
ujenzi wa viwanda vya nguo.
Prof. Mkumbo
ameeleza katika katika maeneo hayo matatu, eneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda
vya nguo ndio kubwa na mpango mmoja wapo wa eneo hilo ni kuona uwekezaji wa
kiwanda kitakacho zalisha nguo zinazotumika kwenye Sekta ya Afya unafanyika.
“Tumeshakamilisha
mpango wa eneo hili na tunakaribisha wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza katika Sekta
ya Nguo,” ameeleza Prof. Mkumbo.
Ameendelea
kueleza kuwa lengo la Serikali ni kuona nguo zote zinazotumika kwenye Sekta ya
Afya zinazalishwa hapahapa nchini ili kuleta tija kwenye sekta hiyo kwa kuona
nguo zinazo tumika kwenye huduma za afya zinapatikana kwa urahisi na kwa wakati.
Pia
akagusia eneo la ujenzi wa viwanda vya kuunganisha magari ambapo tayari kuna
viwanda viwili, kiwanda cha GF Assemblers, kinacho unganisha magari aina ya FAW
na kiwanda cha matrekta kinacho milikiwa na Serikali kupitia NDC.
Licha
ya uwepo wa viwanda hivyo, Prof. Mkumbo ameeleza kuwa Serikali inatarajia ifikapo
mwakani kuwe na uwekezaji mwingine wa kuunganisha magari katika eneo hilo.
“Tunatarajia
ifikapo mwakani, magari aina ya TATA yaanze kuunganishwa kwenye eneo hili,”
amesema Prof. Mkumbo.
Eneo
la tatu ni kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya madawa ambapo kuna kiwanda cha
kuzalisha dawa za kibaiolojia (viuadudu) kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu,
Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), kiwanda kinacho milikiwa na Serikali kwa
100% pamoja na kiwanda cha kuzalisha chanjo za wanyama cha Hester Bioscience
Africa.
Mbali
na hivyo pia kuna kiwanda cha kuzalisha vifungashio cha Global Packaging (T) Limited,
kiwanda kinachomilikiwa kwa ubia baina ya Sekta Binafsi na NDC.
Nae Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la
Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe ameeleza kuwa jukumu kubwa la
NDC ni kuendeleza na kusimamia viwandana kwa niaba ya Serikali.
“NDC ni mkono wa Serikali katika uwekezaji na
tunaendelea kufanikisha lengo hilo kwa kusimamia ujenzi wa viwanda katika kongane
hiyo ya TAMCO,” ameeleza Dkt. Shombe
Pia ameeleza kuwa uwekezaji uliofanyika
katika kongane hiyo umeleta tija kwani umesaidia kwenye utengenezaji wa ajira
kwa Watanzania.
Kongane ya viwanda ya TAMCO ina jumla ya
viwanda 5 vikiwemo vya kuunganisha vyombo vya moto, viwanda vya madawa na
kiwanda cha kuzalisha vifungashio vya mazao mmbalimbali.