SERIKALI KUANZISHA MITAA YA VIWANDA

Kiwanda cha matairi, General Tyre kubadilishwa matumizi
Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo ameeleza Serikali ipo katika mchakato wa kubadilisha eneo la kiwanda cha matairi cha General tyre kilichopo Arusha kuwa mtaa wa viwanda "Industrial Park" kutokana na kiwanda hicho kutokidhi mahitaji ya kuendelea kufanya uzalishaji wa matairi kulingana na teknologia na uhitaji wa soko.
Prof. Mkumbo aliyasema hayo wakati alipofanya ziara katika kiwanda hicho kilichosimama na kuacha kufanya uzalishaji kwa muda wa zaidi ya miaka 10 kutokana na teknolojia ya uzalishaji wa kiwanda kupitwa na wakati pamoja na matairi yaliyokuwa yamezalishwa kukosa soko ambapo amesema kuwa lengo la kufanya eneo hilo kuwa mtaa wa viwanda ni kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuleta ajira kwa watanzania hasa wananchi wa Arusha.
Prof. Mkumbo ameeleza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara ipo katika mchakato wa kuanzisha Mitaa ya viwanda nchi nzima na imeanza kwa kuchagua maeneo machache ambayo itaanzishwa mitaa mikubwa ya viwanda itakayoweza kuleta tija nchi nzima na kuchochea uchumi ambayo itaanzishwa katika mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Kilimanjaro, Mwanza na Arusha pia kuna timu inaendelea kufunya utafiti kwenye mikoa ya kusini.
Aidha, Prof. Mkumbo amewatoa hofu wananchi walioasubilia kufufuliwa kwa kiwanda kilichopoteza zaidi ya ajira 400 kuwa kupitia Uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wanaenda kuboresha na kutumia eneo hilo vizuri kwa kuweka mtaa mkubwa wa viwanda utakaochochea maendeleo makubwa ya uchumi kwa wananchi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake, Leonard Mgoyo msimamizi wa kiwanda kutoka Shirika la Taifa la Maendeleo NDC alieleza kuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho waliachishwa kazi Agosti 2009 lakini tangu mwaka miaka ya 1998 kiwanda hakijawahi kufanya uzalishaji kufikilia angalau asilimia 50 ya uwezo wake japo uwezo upo ila tatizo ni mabadiliko ya teknologia na mitambo kuwa ya kizamani pia kilichozalishwa hakikuhitajika kabisa sokoni.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini Mrisho Gambo alibainisha kuwa Arusha kuna changamoto kubwa ya ajira na wanaamini mkakati wa kufufuka kwa eneo la kiwanda hicho kutatoa mwanga wa Serikali ya awamu ya sita ili wananchi wa Arusha waweze kupata ajira