NDC, TBPL na TANTRADE KUSHIRIKIANA KUTOKOMEZA MALARIA

Timu ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) pamoja na Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), wamefanya kikao cha ushirikiano cha namna ya kusambaza na kutangaza viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu ndani na nje ya nchi.

Kikao hicho kilichofanyika Makao Makuu ya NDC, Dar es Salaam, kimeendeshwa na Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Bi. Rhobi Sattima akishirikiana na Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Bi. Latifa Mohamed Khamisi.


Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Bi. Latifa Mohamed Khamis, akichangia wakati wa kikao cha ushirikiano baina ya NDC, TBPL na TANTRADE

Moja ya ajenda ya kikao hicho ilikua ni kuhakikisha mbu anatokomezwa kabisa nchini na kuifanya Tanzania nchi isiyo na malaria.

Ili kuendana na hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Bi. Latifa ameeleza, sasa ni wakati wa NDC kwenda kidijitali kwa kujisajili kwenye soko mtandao ili viuadudu hivyo viweze kuwafikia watu wengi zaidi kwa uharaka na usalama.

Pamoja na hili, Bi. Latifa ameihakikishia NDC kuwa TANTRADE itashirikiana nao kutafuta masoko ya nje kupitia balozi na makongamano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Bi. Rhobi Sattima amesema kuwa NDC ipo tayari kuhakikisha wanatumia fursa za masoko zilizopo kuhakikisha malaria inatokomea.