UTANGULIZI
Serikali kupitia
Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) inatekeleza mradi wa magadi uliopo Engaruka,
Wilayani Monduli katika Mkoa wa Arusha.
Mradi wa magadi ni moja kati ya miradi ya kimkakati iliyo muhimu katika kujenga
uchumi wa viwanda nchini kwa kuanzisha viwanda vya msingi na viwanda vingine
vitumiavyo malighafi magadi.
Utafiti na lengo
la kujenga kiwanda cha kuzalisha magadi ulianzia katika Ziwa Natron. Mwaka 2006
NDC iliingia ubia na Kampuni ya TATA Chemicals ya India kwa ajili ya kujenga
Kiwanda cha kuzalisha Magadi kutoka Ziwa Natron. Mradi huu ulipata upinzani
mkubwa kwa sababu za kimazingira na kiokolojia ikihusisha ndege aina ya
flamingo. NDC iliamua kutafuta chanzo kingine cha kuzalisha magadi ambapo
ilipelekea kupatikana kwa magadi katika Bonde la Engaruka. Bonde la Engaruka
lipo
umbali wa
takribani kilomita 58 kusini mashariki mwa Ziwa Natron. Hivyo utafiti wa awali
ulifanyika mwaka 2008 kwa NDC ikishirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania
(GST). Hii ilifuatiwa na Utafiti wa kina uliuofanyika mwaka 2010-2013 ambao
ulionesha kuwepo kwa magadi ya kutosha na kushauri ufanyike upembuzi yakinifu (techno-economic study) kwa ajili ya
kujenga kiwanda.
2 UPEMBUZI
YAKINIFU
Kazi ya upembuzi
yakinifu imefanywa na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania
(TIRDO) katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 na kuhitimishwa Mei 2021.
Upembuzi yakinifu ulihusisha, pamoja na mambo mengine, kuhakiki wingi wa magadi
soda yaliyopo, tathmini ya masoko ndani na nje ya nchi, tathmini ya athari kwa
mazingira, tathmini ya miundombinu inayohitajika na kufahamu gharama za ujenzi
wa kiwanda, sehemu ya kuweka kiwanda, teknolojia bora ya kuvuna magadi na soko
la magadi.
3 NJIA
ZILIZOTUMIKA KUFANYA UPEMBUZI YAKINIFU
Katika kufanya upembuzi
yakinifu, zilitumika njia mbalimbali. Hii ni pamoja na kufanya mapitio ya
takwimu na taarifa za nyuma zinazohusiana na eneo linalolengwa kwa ajili ya uchimbaji
wa magadi soda, kutembelea eneo la mradi katika Bonde la Engaruka na kufanya
uchunguzi wa kijiolojia (geological
mapping) na jiofizikia (geophysical
surveys). Njia zingine zilizotumika
ni pamoja na kupampu magadi kutoka kwenye
visima (pumping tests), uchunguzi
wa miamba choronge (re-logging of cores),
kuchukua sampuli za miamba na magadi (brine), usanifu (process design), uchakataji wa taarifa na takwimu (data analysis) na kufanya modeli (modelling).
4 MATOKEO
YA UPEMBUZI YAKINIFU
4.1 Uhakiki wa
Magadi Soda
Bonde la Engaruka
limefunikwa zaidi na mchanga au mawe (superficial deposits) ambao chanzo chake
ni volcano. Bonde hili limezungukwa na milima ya volcano kama vile Kerimasi,
Essimingor na Burko. Mito na vijito (vingi vikiwa ni vya msimu) vinayotelemka
kutoka milima jirani, hutiririsha maji katika Bonde la Engaruka kutoka pande
zote na hii inaongeza chumvi ya ziada (zinazotokana na miamba ya volkano)
katika magadi yaliyoko katika miamba inayobeba magadi soda. Upembuzi yakinifu
umebaini kuwa:
§
Bonde la Engaruka linayo matabaka (stratigraphic
units) yenye ukubwa mbalimbali yanayojumuisha udongo wa mfinyanzi, mchanga
laini (fine sand), mchanga mnene (coarse sand) na chumvi (salt layers) na
mapande makubwa ya chumvi (thick layer of crystalline salts) hususani yenye sodium carbonate na sodium bicarbonate.
§
Magadi (brines) yaliyomo katika matabaka yya udongo (sediments) yana
madini mengi ya sodium bicarbonate na sodium carbonate. Sampuli zilizochukuliwa
zimeonesha kuwa na madini ya sodium bircarbonate gramu 12.0 mpaka gramu 25.49
kwa lita na madini ya sodium carbonate gramu 125.93 mpaka 245.92 kwa lita.
§
Sampuli za miamba na udongo zilionesha Na+ and Ca2+ kutawala katika madini ya aegirine-augite, plagioclase, hedenbergite,
carbonates na chumvi mbalimbali hususani trona.
§
Jumla ya discharge katika
visima vilivyopampiwa (The combined discharge of all pumped boreholes) katika
uwezo wa mita za ujazo 171.805 kwa saa vilionesha drawdown ambayo ni ya kawaida na hii inaashiria kutakuwepo na
uzalishaji mzuri wa miamba au matabaka yenye magadi (indicating presence of good
productive aquifers).
Ukadiriaji uliofanyika mwaka
2013 ulionesha uwepo wa magadi (brine)
takriban mita za ujazo 4,680,000,000 yanayoongezeka (brine replenishment) kwa mita za ujazo 1,875,000 kwa mwaka. Katika
uhakiki uliofanywa na TIRDO umeonesha uwepo wa takriban mita za ujazo
3,294,704,894 za magadi (brine) zenye
sodium bircarbonate tani milioni 59
na sodium carbonate tani 664.24. Hata
hivyo kazi ya kuhakiki wingi wa magadi soda kwa ukamilifu katika Bonde la
Engaruka inahitaji kuchimba visima vingine. Baadhi ya visima vilivyoripotiwa
kuchimbwa awali na kuhusishwa katika utafiti havikuonekana na visima vingine
vikiwa na urefu mfupi kinyume na matarajio. Visima vitakavyochimbwa (exploratory cum production boreholes)
vitatumika kukamilisha utafiti na visima hivi pia vitatumiwa katika uzalishaji
wa magadi.
4.2 Mchanganuo wa Soko la Magadi Soda
Mwaka 2018 nchi ya China
ilikuwa ndio mtumiaji mkubwa wa magadi soda kwa takribani asilimia 41.6% ya
soko lote duniani. Bei ya mauzo ya Magadi Soda inaendelea kupanda duniani
kutokana na kuongezeka kwa mahitaji kuliko uzalishaji wake. Bei ya magadi soda
iliongezeka kwa asilimia 0.84% katika kipindi cha mwaka 2011-2018 mpaka kufikia
kiasi cha dola za Marekeni 301 kwa kila tani ya magadi soda katika mwaka 2018.
Kenya ndio nchi pekee inayouza magadi katika nchi za Afrika Mashariki. Soko
kubwa la Kenya lipo katika nchi ya India. Katika mwaka 2018 nchi za Afrika
mashariki zilikuwa na upungufu wa wa tani 60,000 kwa ajili ya mahitaji ya
ndani. Tanzania iliagiza tani 40,000 ikifatiwa na Uganda iliagiza tani 15,000.
Kufatana na viashiria vya kibiashara katika mwaka 2014-2018, kwa wastani bei ya
kuagiza magadi soda ilikuwa ni dola za kimarekani 302 kwa kila tani.
Kwa makisio ya uzalishaji wa
magadi soda utakaofanyika katika Bonde la Engaruka ni tani 500,000 kwa mwaka.
Uzalishaji huu utaweza kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi, ukanda wa Afrika
Mashariki na soko la kimataifa. Wastani wa asilimia 87 ya uzalishaji utakaofanyika
utatumika kwa ajili ya soko la nje ya nchi. Soko la ndani litaweza kutumia
kiasi cha asilimia 13 mpaka 30 kufikia mwisho wa mwaka 2030 baada ya
kuhamasisha viwanda vya ndani kutumia magadi haya. Watumiaji wakubwa wa madini
haya ni viwanda vya vioo, viwanda vya sabuni ambavyo vinatumia zaidi ya
asilimia 60 ya mahitaji ya sasa ya magadi soda. Kwa kuanzia uzalishaji wa
magadi utakuwa ni tani 500,000/= kwa mwaka na uzalishaji unaweza kuongezwa
baadae mpaka kufikia tani 1,000,000/= kutegemea na ukuaji wa soko la ndani na
nje ya nchi.
4.3 Tathmini ya Teknolojia ya Uvunaji wa Magadi
Tathmini iliyofanyika
ilipelekea kuchagua carbonation process
kuwa njia inayofaa katika uchenjuaji wa magadi katika Bonde la Engaruka.
Uchenjuaji huu unajumuisha matumizi ya gesi ya kaboni dioksidi katika magadi
(brine) yaliyochujwa ambapo sodium
carbonate (Na2CO3) hubadilishwa kwenda kwenye sodium bicarbonate
(NaHCO3). Kwa kutumia hydro-cyclone and filtration chumvi ya Sodium bicarbonate hutengwa kutoka katika
solution (mother liquor). Chumvi iliyopatikana huoshwa, kukaushwa na kiasi
fulani huwezwa kuingizwa katika soko kama sodium
bicarbonate. Lakini sehemu kubwa sodium
bircabonate hubadilishwa kuwa magadi soda.
4.4 Usanifu wa
Mradi wa Magadi Soda
Usanifu wa mradi ulifanyika
kuhusiana na aina ya mitambo (machinnery) inayohitajika kwa ajili ya uzalishaji
wa magadi soda. Hii inajumuisha uchaguzi wa ukubwa wa mitambo ya uchenjuaji na
usanifu wa mfumo wa kupampu magadi (brine
pumping system), mabwawa ya
kuhifadhia (settling/storage ponds)
pamoja na kubainisha mfumo wa nguvu
ya uzalishaji (steam and power generation
systems). Pia imehusisha kutambua makisio ya gharama za vifaa
vitakavyotumika.
Makisio ya
gharama za kiwanda zinazojumuisha nishati ya uzalishaji (steam and power generation
systems), kupampu magadi (brine pumping) na umeme kutoka TANESCO ni takribani dola za kimarekani
milioni 307. Gharama hizi hazihusishi kujenga majengo ya kiwanda na miundombinu
yake. Usanifu uliofanyika ni wa awali; front-end
engineering design (FEED). Kiwanda halisi kitahitaji usanifu wa kina wa kiwanda na mitambo uchenjuaji,
utengenezaji wa sehemu kuu za kiwanda (fabrication of major units), kusanifu
ujenzi (design and construction of foundations for the major units) na
usimikwaji wa mitambo (installation of all units and accessories). Utekelezaji
wa shughuli hizi unashauriwa kuwa ni wa turnkey
project.
4.5 Tathmini ya Mahitaji ya Kiwanda (Plant Utilities)
Makadirio ya matumizi ya maji
katika kiwanda ni mita za ujazo 903 kwa siku. Utafiti wa vyanzo vya maji
ulifanyika katika mito (surface water),
maji ya ardhini (groundwater) na uwezekano wa kuvuna maji ya mvua katika maeneo
ya karibu na mradi. Mto Engaruka na Chemchem za Lositete vilipendekezwa kuwa
vyanzo cha maji yatakayotumiwa katika mradi wa Engaruka. Vyanzo hivi viko
katika pande tofauti za eneo la mradi, kila chanzo kitakuwa na njia yake na
miundombinu yake kufikia eneo la mradi. Hivyo usanifu (engineering designs) ulifanywa kutoka kwa kila chanzo hadi kwenye
eneo ya mradi. Gharama ya usambazaji wa maji inakadiriwa kuwa takribani dola za
kimarekani milioni 1.86. Inapendekezwa nishati ya kuendeshea mradi kutoka gridi
ya kitaifa ya TANESCO na makaa ya mawe.
4.6 Eneo la
Ujenzi wa Kiwanda na Usanifu wa Miundombinu
Vigezo vya kuchagua eneo linalofaa
kwa ujenzi wa kiwanda ni pamoja na sababu za kiikolojia, historia ya mafuriko
ya eneo la mradi, hali ya kijiolojia ya eneo hilo na ripoti kutoka kwa tafiti
nyingine zilizofanyika katika eneo la mradi. Majengo ya makazi yalisanifiwa
kulingana na uongozi na kada ya wafanyakazi (staff cadre hierarchy). Katika
eneo lililopendekezwa, huduma mbalimbali za kijamii zilizingatiwa. Makadirio
(estimated bill of quantities) kwa ajili ya majengo ya kiwanda na mji
(township) ni takribani dola za kimarekani milioni 15.3.
4.7 Usafirishaji
wa Magadi Soda
Utafiti wa
usafirishaji wa magadi soda umeonesha kuwa, kwa usafirishaji mzuri wa mizingo
na mitambo wakati wa kipindi cha kwanza cha mradi na wakati wa uzalishaji
inapendekezwa kuwa: barabara ya lami ya kilomita 18 ijengwe kutoka makutano ya
Kiwanda cha Engaruka hadi eneo la uchenjuaji. Barabara hii itagharimu takribani
dola za kimarekani milioni 8.22, Kuboresha barabara ya Mto wa Mbu hadi Loliondo
angalau hadi kufikia kwenye makutano ya Engaruka, Kuboresha kwa kiwango cha
lami cha barabara ya km 95 kutoka Moshi hadi Longido kama njia mbadala iwapo
kuna dharura
yoyote
itakayogharimu takribani dola za kimarekani 43.4 milioni. Ujenzi wa reli kutoka
Arusha hadi eneo la kiwanda. Ujenzi wa reli ndio njia bora zaidi ya
usafirishaji iliyo nafuu itakayowezesha magadi soda yanayozalishwa kuhimili
ushindani wa kibiashara katika soko la ndani na nje ya nchi.
4.8 Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Kijamii
(ESIA)
Tathmini ya athari kwa
mazingira na kijamii ilifanyika kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za mazingira za
Tanzania na Benki ya Dunia na Viwango vya Utendaji vya Shirika la Fedha la
Kimataifa (IFC). Wakati wa tathmini, athari za mradi kwa mazingira na kijamii
na kiuchumi na kitamaduni zinazohusiana na mradi uliopendekezwa ziligunduliwa
na hatua za kuzuia au kupunguza makali yake zilipendekezwa. Hizi ni pamoja na
athari kwa matumizi ya ardhi (kwa mfano, kuzuia njia za miguu, korido za
wanyamapori, vitalu vya uwindaji, maeneo ya malisho, upotezaji wa ardhi ya
malisho); ajali kutokana na kuongezeka kwa magari barabarani; athari kwa
rasilimali za maji, mimea na wanyama, ubora wa hewa na maji na makazi ya asili.
Kwa hivyo, usimamizi wa athari hasi zilizoainishwa utahitaji utekelezaji wa
hatua muhimu za kupunguza pamoja na chaguzi zinazoweza kutolewa kama
ilivyoelezewa katika Mpango wa Usimamizi wa Mazingira na Jamii (ESMP).
4.9 Tathmini
ya Mradi
Upembuzi yakinifu umechambua
na kupendekeza kazi zinazofaa za biashara na muundo wa shirika, viwango vya
utunzaji, mahitaji ya ustadi, na makadirio ya gharama za rasilimali watu.
Muundo (organization structure) uliopendekezwa una idara 5: Huduma za
Uzalishaji na Ufundi (Production and Technical Services); Mauzo (Sales), Uuzaji
na Usafirishaji (Marketing and Logistics); Ugavi wa Rasilimali, Upelembaji na
Ufuatiliaji (Monitoring and Evaluation); Afya, Usalama na Mazingira; na, Huduma
za Kampuni (Corporate Services). Jumla ya wafanyakazi 223 wataajiriwa katika
mradi wa magadi wa Engaruka.
Mradi wa magadi soda ni mradi
mkubwa (mega project ) ambao utahitaji jumla ya dola za Kimarekani milioni
367.1 kuuendesha. Inapendekezwa kuwa mradi uwe wa ubia unaojumuisha Serikali
kupitia NDC na Mwekezaji mahiri hususani mwenye mitaji mikubwa, teknolojia na
uzoefu wa uzalishaji wa magadi kwa umiliki wa uwiano wa 49:51. Uwekezaji
utakuwa katika mfumo wa equity utakaowezesha kupatikana kwa vifaa vya mradi,
miundombinu pamoja na namna ya ulipaji wa deni ili kuhakikisha kuwa mradi
unaanza ifikapo mwaka 2025. Inashauriwa ulipaji wa deni/ A debt to equity ratio/uwiano
wa 67:33 kwa ajili ya kufadhili mradi. Mradi wa magadi unategemewa kutekelezwa
kwa faida (financially viable and bankable):
§
Thamani ya Sasa ya Mradi/ Net Present Value (NPV) itakuwa dola za
Marekani milioni 335.1
§
Kiwango cha Kurudisha/Internal Rate of Return (IRR) ni 19.7%.
§
Kipindi cha Kulipa/Payback Period ni miaka 5.
5 HITIMISHO
Taarifa ya
upembuzi yakinifu imefikia hitimisho kuwa mradi wa magadi soda wa Engaruka
unalipa na kutekelezeka kwa kuzingatia vipengele vya teknolojia, uchumi, faida
katika maendeleo ya jamii na mazingira. Hii ikiwa na maana kuwa faida tarajiwa
zinazidi gharama zinazohitajika kuendeleza na kuendesha mradi na hivyo mradi
una faida kiuchumi. Magadi ni rasilimali itayoweka msingi wa kuwepo kwa viwanda
mama nchini. Aidha, magadi yatachochea uanzishwaji wa viwanda vingine vya
kemikali.