Wakuu
wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, wakiongozwa na
Mwenyekiti wao Prof. Emmanuel Mjema ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Elimu ya
Biashara (CBE) wamefanya ziara katika taasisi za TEMDO, CAMARTEC, SIDO za
jijini Arusha na kiwanda cha KMTC kinachomilikiwa na Shirika la Taifa la
Maendeleo (NDC) cha mkoani Kilimanjaro, pamoja na Shirika la Utafiti na Maendeleo
ya Viwanda Tanzania (TIRDO), kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali yanayofanywa
na taasisi hizo.
Ziara
hiyo inakuja baada ya kuona uhitaji wa kufahamiana zaidi ili kuona namna bora ya
kubadilishana teknolojia, ujuzi na namna bora wanayoweza kushirikiana katika
ujenzi wa Tanzania ya viwanda.
“Kila
taasisi ilianzishwa kwa sheria yake, ila tumeona haja ya kutafuta namna bora ya
kushirikiana,” amesema Prof. Mjema. Aliendelea kueleza kuwa taasisi kama TEMDO
na CAMARTEC wana bidhaa nyingi wanazo zalisha ila hazifahamiki hivyo kuna haja
ya wao kusaidiana katika kutengeneza mpango mkakati wa biashara zao.
Hata
hivyo taasisi hizo zimekua zikishirikiana katika nyanja mbalimbali kama
uhaulishaji wa teknolojia, uliopo baina ya TIRDO na NDC, CBE na SIDO kupitia
mpango wa Kaizen, CAMARTEC, TEMDO na NDC, huku TANTRADE ikihusika kufungua
fursa za masoko ya bidhaa zinazo zalishwa na taasisi hizo kupitia maonesho ya
kitaifa na kimataifa.
Awamu
ya pili ya ziara hiyo itahusisha taasisi za BRELA, TBS, Wakala wa Vipimo, FCC,
CBE pamoja na FCT.