WASHINDI MEI MOSI WAULA

Wafanyakazi wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), waliofanya vizuri kwa mwaka 2021/22 wamekabidhiwa zawadi zao leo hii kwa kutambua mchango wao katika ujenzi wa Taifa kupitia NDC, hafla iliyofanyika Makao Makuu ya NDC, jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi zawadi hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika, Dkt. Grace Aloyce amewapongeza wote waliopata zawadi na kuwasihi wafanyakazi wote wa NDC kuendeleza juhudi na bidii katika kazi.

“Tukifanya kazi sote kwa bidii tutafikia malengo yaliyopo kwenye Mpango Mkakati wetu,” ameeleza Dkt. Grace.

Akizungumza kwa niaba ya Mshindi wa Jumla, ambaye ni ndugu Alphonce Lufunda, Mseli Nyika aliwashukuru wafanyakazi wote kwa kutambua mchango wa ndugu Lufunda au maarufu kama Babu, akiitwa hivyo na wafanyakazi walio wengi, na kusema kuwa Babu amekuwa ni mtu wa kujituma na kuhakikisha anatekeleza majukumu yake ipasavyo bila kusukumwa.

Mbali na zawadi ya mshindi wa jumla, washindi wengine walio kabidhiwa zawadi ni Hamida Shabani kutoka Idara ya Fedha, Florian Mramba kutoka Idara ya Utafiti na Mipango, Robina Karumuna kutoka Idara ya Viwanda Mama, Dorice Rutina kutoka Idara ya Viwanda vya Kimkakati vya Kuongeza Thamani, Pulkeria Shao kutoka Idara ya Utendaji na Jacob Maganga aliyepata zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe.