Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt, Nicolaus Shombe,
amesema NDC ipo tayari na imejipanga kikamilifu kupokea wawekezaji wenye nia ya
kuwekeza kwenye Kongane ya Viwanda ya TAMCO iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Dkt.
Shombe amesema haya akiwa ameambatana na Menejimenti ya Shirika na baadhi ya
wafanyakazi wa NDC ambao walipata fursa ya kutembelea eneo hilo.
Dkt.
Shombe amesema Serikali inaendelea na ukamilishaji wa miundombinu mbalimbali ya
uwekezaji katika eneo hilo ikiwemo ujenzi wa barabara huku akiwakaribisha
wawekezaji walio tayari kuwekeza kwenye sekta ya nguo na mavazi, vifaa tiba na
dawa pamoja na uunganishaji wa magari na mitambo mbalimbali kuja kuwekeza
kwenye kongane hiyo.
Akikazia
hilo, ameeleza kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu
ya Kongane hiyo ili kujenga mazingira mazuri na salama kwa wawekezaji waliopo
na kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza katika eneo hilo.
Katika
ziara hiyo ambayo iltumika pia katika kutembelea viwanda mbalimbali vilivyoko
katika eneo la TAMCO, Dkt. Shombe amekitaka kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya
kuangamiza viluwiluwi wa mbu, Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), kilichopo
katika eneo hilo kuhakikisha kinatanua wigo wa masoko ya viuadudu ndani na nje
ya nchi ili kuongeza juhudi za kupambana na mbu waenezao Malaria na magonjwa
mengine kama Zika, Dengue, Chikungunya, Matende na Mabusha.
Sambamba
na hilo ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha wanakamilisha taratibu
zote za kuanza uzalishaji wa viuatilifu vya kupambana na wadudu wadhurifu
kwenye mazao kama pamba na korosho, ili kusaidai wakulima wapate kipato na
kuondoa changamoto ya mazao kuharibika shambani.
Imetolewa
na Idara ya Uhusiano, NDC.