WAZIRI MKUMBO AZINDUA TELA

Tela hilo linazalishwa na KMTC ya mkoani Kilimanjaro

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) amekuzindua Tela la kubeba mizigo lililotengenezwa Tanzania kupitia kiwanda cha KMTC cha mkoani Kilimanjaro, kiwanda kilicho chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), kufuatia ushirikiano baina ya NDC, Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) pamoja na Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Miitambo Tanzania (TEMDO) ambapo NDC ilitoa wazo bunifu, TEMDO walihusika katika usanifu wa michoro na CAMARTEC kufanya majaribio ya kitaalamu. 

Uzinduzi huo umefanyiaka leo Julai 07, 2021 kwenye viwanja vya Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam - DITF (Saba saba)  ambapo Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo aliambatana Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb).

 

Prof. Kitila Mkumbo wakati akizindua Tela hilo ameeleza kuwa ni la kipekee pia lina uwezo wa kubeba uzito wa tani tano za mizigo, lina ubora na ufanisi ulithibitishwa na Shirika la viwango TBS. Wakati huo akatumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi kununua ili iwe ni sehemu ya kuamini na kutumia bidhaa zetu za ndani na Kwa kufanya hivyo watakuwa wamejenga na kuendeleza uchumi wa Viwanda sambamba na kukuza ubunifu unaofanywa na Watanzania wenzetu.

 

Nae, Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Bi. Rhobi Sattima ametaja mchango wa tela kwa upande wa kukuza uchumi ambao  ni Kupunguza gharama za kusafirisha mazao na mizigo kwa wakulima, Kuongeza kipato, Gharama ndogo za uendeshaji kutokana na ubora wake na Mapinduzi kwenye Sekta ya kilimo kwani mkulima anaweza kuzalisha bila ya kuwa na changamoto ya usafirishaji wa mazao na pembejeo.