Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limepokea ugeni kutoka Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) lililoongozwa na Kamishna wa Tume, Bi. Suzan Mlawi, katika ziara maalum ya kikazi. Ziara hiyo iliangazia mazungumzo na menejimenti pamoja na wafanyakazi wa NDC juu ya umuhimu wa wafanyakazi kufuata maadili ya Utumishi wa umma pamoja na utendaji, na uwajibikaji kazini.
Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna Mlawi alisema kuwa lengo kuu la ziara ni kufanya tathmini ya utendaji wa watumishi, uzingatiaji wa miongozo ya kiutumishi, utoaji wa likizo, upatikanaji wa mafunzo, vitendea kazi, na nidhamu kazini, ikiwemo matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.
“Tunawapongeza NDC kwa kudumisha maadili mema kazini na kuendeleza utendaji bora. Tuna matumaini kwamba juhudi hizi zinaendelea kuboresha utendaji na maadili ya watumishi,” alisema Kamishna Mlawi, akiongeza kuwa alifurahishwa na hali ya nidhamu na uadilifu ndani ya NDC.
Ziara hiyo pia ilihusisha viongozi wengine wa PSC ambao walisisitiza umuhimu wa uwazi, uadilifu, na uwajibikaji kazini. NDC ilieleza kuwa ziara hiyo ni fursa muhimu ya kujifunza na kuimarisha mifumo ya kiutumishi, kuhakikisha taasisi inabaki mfano bora wa utumishi wa umma.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa NDC, Bi. Esther Mwaigomole, aliwashukuru viongozi wa PSC kwa kufanya ziara hiyo na kuahidi kuwa NDC itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inafuata kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Ziara hii ni sehemu ya jitihada za Tume ya Utumishi wa Umma kutembelea taasisi mbalimbali za serikali, zikikumbusha umuhimu wa kuhakikisha taasisi za umma zinazingatia misingi ya utawala bora na uwazi.

