KIKAO CHA KWANZA CHA BODI YA KMTC CHAZINDULIWA

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah ameshiriki na kuzindua rasmi kikao cha kwanza cha Bodi ya kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma, KMTC Manufacturing Limited.

Dkt. Hashil amekihakikishia kiwanda hicho kuwa Wizara ya Viwanda ipo tayari na inaendelea kuiunga mkono KMTC ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ili kufikia malengo yake.

Aliongeza kuwa, maendeleo ya KMTC ndio maendeleo ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

“Bila viwanda hamna wizara ninayo isimamia, hivyo lazima tuhakikishe KMTC inafanya vizuri,” alisema Dkt. Hashil.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe amesema ili kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hamna budi kuweka mikakati madhubuti kwenye kiwanda cha KMTC.

Dkt. Shombe alimuhakikishia Katibu Mkuu kuwa NDC kama msimamizi mkuu wa kiwanda cha KMTC itahakikisha kiwanda hicho cha kimkakati kinazalisha bidhaa zenye tija kwenye soko la ushindani.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa KMTC, ndg. Leonard Mgoyo alimkaribisha Katibu Mkuu na ugeni wake kiwandani hapo na kuwaonesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na kiwanda hicho ikiwemo utengenezaji wa mashine kwa ajili ya viwanda vikubwa na viwanda vidogo vidogo ikiwemo watu binafsi.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *