Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limetia saini mikataba miwili ya ushirikiano na kampuni ya LABIOFAM kutoka Cuba, yenye lengo la kuimarisha uzalishaji wa mbolea hai na kuhamisha teknolojia ya kisasa kwa wataalamu wa Tanzania.
Mikataba hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa mbolea rafiki kwa mazingira inayotokana na teknolojia ya kibaolojia kutoka Cuba, na kuiwezesha Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa bidhaa hiyo kwa matumizi ya ndani na soko la kikanda. Aidha, kupitia uhamishaji wa teknolojia, wataalamu wa Kitanzania watanufaika kwa mafunzo ya kitaalamu yatakayowezesha uendelevu wa mradi huo ndani ya nchi.
Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humprey Polepole akiwa kwenye hafla ya kusaini mikataba ya uzalishaji mbolea hai.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe alisema: “Ushirikiano huu ni hatua kubwa katika safari ya Tanzania kuelekea mapinduzi ya viwanda na kilimo hai.”
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole, ambaye ameeleza kuridhishwa na hatua hiyo muhimu katika kudumisha mahusiano kati ya nchi hizi mbili. “Mikakati kama hii inaakisi dhamira ya mataifa yetu kuendeleza ustawi wa wananchi wake kupitia teknolojia na maarifa.”
Nae Mkurugenzi wa LABIOFAM S.A Bw. Julio Gonzalez amesema uhaulishaji wa teknolojia utafanyika kwa bidhaa zote zinazo tarajiwa kuzalishwa na kiwanda cha TBPL.
Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Veraakiwa kwenye hafla ya kusaini mikataba ya uzalishaji mbolea hai.
Mkataba huu unatarajiwa kuchochea mapinduzi katika sekta ya kilimo, kwa kutoa mbolea salama kwa matumizi ya wakulima wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Aidha, unakuza maarifa ya kitaalamu, ajira kwa vijana, na kusaidia jitihada za kupunguza matumizi ya kemikali hatarishi katika uzalishaji wa chakula.