Mkurugenzi Mtendaji wa NDC awasilisha Miradi Mikubwa ya Maendeleo kwa Kamati ya Bunge

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe, amewasilisha taarifa ya kina ya majukumu, muundo wa shirika pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya kitaifa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Mifugo na Kilimo, katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Dkt. Shombe alieleza kuwa NDC inaendelea kutekeleza dhamana yake ya kuanzisha na kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo yenye lengo la kukuza uchumi wa viwanda, kuongeza ajira na kuongeza thamani ya rasilimali za ndani kwa manufaa ya Taifa. Alibainisha mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo pamoja na mikakati inayochukuliwa na Serikali kupitia NDC kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.

Miongoni mwa miradi mikubwa iliyowasilishwa ni Mradi wa Liganga na Mchuchuma, unaotekelezwa wilayani Ludewa mkoani Njombe, ambao unalenga kuimarisha sekta ya viwanda vya chuma na nishati nchini. Mradi huu ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kupunguza utegemezi wa uagizaji wa chuma na malighafi kutoka nje ya nchi na kuwezesha Tanzania kujitegemea katika uzalishaji wa bidhaa za chuma.

Mradi wa Liganga na Mchuchuma unahusisha uchimbaji wa madini ya chuma katika eneo la Liganga na makaa ya mawe katika eneo la Mchuchuma, pamoja na ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 600 kwa kutumia makaa ya mawe. Aidha, mradi unajumuisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata chuma vinavyotarajiwa kuzalisha tani milioni 2.9 za chuma ghafi na takribani tani milioni moja ya bidhaa za chuma kila mwaka. Mbali na chuma, mradi huo pia unatarajiwa kuzalisha madini ya titanium na vanadium, yanayotumika katika viwanda.

Dkt. Shombe alieleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa matumizi ya viwanda na taifa kwa ujumla, huku kituo cha uzalishaji wa umeme cha megawati 600 kikitarajiwa kuunganishwa na maeneo ya mradi kupitia njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa 220 kV. Mradi pia unatarajiwa kuunda ajira zaidi ya 6,600 za moja kwa moja na zaidi ya 26,000 zisizo za moja kwa moja, hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Njombe na maeneo ya jirani.

Katika hatua nyingine, aliieleza Kamati kuwa Serikali tayari imeshatekeleza zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi zaidi ya 1,142 waliokuwa wanaishi katika maeneo ya mradi, hatua inayolenga kuondoa vikwazo vya uwekezaji na kuharakisha utekelezaji wake.

Mradi mwingine uliowasilishwa ni Mradi wa Magadi Soda Engaruka, unaotekelezwa mkoani Arusha. Mradi huu unalenga uchimbaji na uzalishaji wa magadi soda kwa kiwango kikubwa, malighafi muhimu inayotumika katika viwanda vya kutengeneza vioo, sabuni, karatasi, dawa, pamoja na mbolea.

Dkt. Shombe alieleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza utegemezi wa uagizaji wa magadi soda kutoka nje ya nchi, hivyo kuokoa fedha za kigeni na kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani. Aliongeza kuwa Serikali tayari imeanza kulipa fidia kwa wakazi wa maeneo ya mradi, ikiwa ni hatua ya msingi kuelekea utekelezaji kamili na kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo.

Mradi wa Magadi Soda Engaruka unatarajiwa kuzalisha hadi tani milioni moja ya magadi soda kwa mwaka, sambamba na kutoa ajira na kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.

Akihitimisha wasilisho lake, Dkt. Shombe alisisitiza kuwa NDC itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali, Bunge, wawekezaji binafsi pamoja na jamii zinazozunguka maeneo ya miradi ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya Taifa kwa ujumla.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *